Saturday, September 30, 2017

1 October 2017,Watu 30 wahofiwa kufa katika ajali ya ndege Kongo DR

Ndege ya usafirishaji inayomilikiwa na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeanguka leo karibu na mji mkuu Kinshasa na kuuwa makumi ya watu. Hayo yameelezwa na duru za kijeshi nchini humo.

Ndege hiyo ya usafirishaji aina ya Antonov ilipata ajali mara baada ya kuruka na ilikuwa imebeba makumi ya watu. Ndege hiyo imeanguka katika eneo la Nsele umbali wa kilomita 100 mashariki mwa Kinshasa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Afisa mmoja wa eneo hilo amesema kuwa hakuna mtu aliyenusurika katika ajali hiyo. Jeshi la Congo limetangaza kuwa ndege hiyo iliyokuwa na rubani raia wa Russia, ilikuwa imebeba magari mawili, silaha na wanajeshi. Limesema ndege hiyo ilikuwa na watu kati ya 20 na 30 wakati ilipoondoka katika uwanja wa ndege wa Ndolo mjini Kinshasa.

Mtu mmoja aliyeshuhudia ndege hiyo ikipata ajali amesema ilikuwa majira ya asubuhi kwa wakati wa Kongo alipoiona ndege ikianguka lakini hakukuwa na moshi kutoka kwenye ndege hiyo.

Wakala wa Shirika la Usafiri wa Anga la Kongo amesema kuwa ndege hiyo ilishindwa kuruka inavyotakikana katika uwanja wa ndege wa Ndolo na imeanguka katika eneo jirani la Nsele.

30 September 2017,Radio iliyokosoa mauaju ya wakimbuzi wa Burundi yafungwa DRC

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesimamisha matangazo ya radio moja inayomilikiwa na Chama cha Wafanyabiashara wa Burundi, kwa kukosoa mauaji ya wakimbizi Warundi waliouawa hivi karibuni na wanajeshi wa DRC.

Eddy Claude Nininahazwe, Mkurugenzi wa CCIB FM+ amesema idhaa hiyo imefungiwa matangazo kwa kupeperusha tahariri iliyokosoa vikali mauaji hayo sambamba na kimya cha vyombo vya dola kuhusu ukatili huo.

Baraza Taifa la Mawasiliano la Kongo DR limehalalisha hatua ya kufunga idhaa hiyo kwa miezi mitatu kuanzia Jumatatu ijayo, likisema kuwa ilikiuka maadili na kanuni za uandishi wa habari.

Septemba 15, waandamanaji 36 ambao walikuwa ni wakimbizi kutoka Burundi walipigwa risasi na kuuawa na wanajeshi katika mji wa Kamanyola mkoani Kivu ya Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Serikali ya Burundi imetaka kufanyika uchunguzi wa kina huku ikiwaomba viongozi wa Kinshasa wawasilishe maelezo kuhusu mauaji hayo.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, wakimbizi wa Burundi elfu 44 wamepewa hifadhi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

30 September 2017, Wakulima watatu wauawa Morogoro

Morogoro. Wakulima watatu wakazi wa Kata ya Kolero wilayani Morogoro wameuawa kwa kupigwa walipokamata mifugo iliyokuwa inalishwa kwenye mazao yao.

Diwani wa Kata ya Kolero, Eligius Mbena amesema Alhamisi Septemba 28 ng’ombe zaidi ya 140 waliingizwa kwenye mashamba ya wakulima katika Kijiji cha Kidodi na kula mazao.

Ng’ombe hao ambao inadaiwa ni mali ya mfugaji mmoja inaelezwa wameharibu zaidi ya eka tano za mazao ya mahindi, kunde na mbogamboga yaliyokuwa yakikaribia kukomaa.

Diwani huyo amesema baada ya wakulima kuona kundi la ng’ombe waliamua kuwasiliana na mtendaji wa kata ambaye alituma mgambo na kwa kushirikiana na wananchi waliondoa mifugo hiyo na kuipeleka ofisi ya kata.

“Baada ya mgambo kufika wale vijana waliokuwa wakilinda ng’ombe walikimbia ndipo wananchi na mgambo walipowaswaga ng’ombe hadi ofisi ya Kata ya Kolero kwa hatua zaidi,” amesema.

Amesema kwa utaratibu waliojiwekea, ng’ombe wanapokamatwa kwenye mashamba hutozwa faini ya Sh10,000 kwa kila mmoja. Mbena amesema mtendaji ndivyo alivyofanya kwa mifugo hiyo iliyokamatwa.

Amesema baada ya mhusika kulipa faini na kukabidhiwa ng’ombe wake, wananchi waliondoka na wakiwa njiani walishambuliwa.

Amewataja waliouawa kuwa ni Richard Edward, Riziki Juma na Antoni Matei ambao ni wakulima na wakazi wa Kata ya Kolero.

“Ninachosikitika ni kwamba, taarifa za mauaji haya tumezitoa katika mamlaka zote za wilaya na mkoa tangu Alhamisi Septemba 28 lakini hadi leo Jumamosi hakuna hatua iliyochukuliwa japo mwenye mifugo tunamjua na tumewatajia polisi,” amesema Mbena.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo alisema hawezi kuzungumzia lolote kwa kuwa masuala ya mauaji yanahusu Jeshi la Polisi na si ofisi yake.

“Msemaji wa matukio yote ya mauaji ni RPC si mimi,” alisema Chonjo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leons Rwegasira alisema wamepata taarifa hizo na wametuma timu kufuatilia.

“Tuna taarifa kwamba kuna watu wameuawa Kolero lakini bado hatujapata kwa usahihi kwa kuwa timu yetu ndiyo imekwenda huko,” amesema.

30 September 2017,Zaidi ya wakimbizi 60 wa Rohingya wafariki ,40 hawajulikani walipo baada ya mashua kuzama

Zaidi ya wakimbizi 60 kutoka jamii ya Rohingya wafariki baada ya mashua yao kuzama wakijaribu kukimbia mauaji Myanmar

Mashua ilikuwa ikiwasafarisha wakimbizi kutoka jamii ya Rohingya imeripotiwa kuzama n kusababisha vifo vya watu zaidi ya 60.

Msemaji wa shirika la kimataifa la wahamiaji Joel Millman  amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa mashua ilikuwa ikiwasafirisha waislamu wa jamii ya Rohingya waliokuwa wakikimbia mauaji Myanmar imezama na kusabaisha maafa hayo.

Mashua hiyo imeripotiwa kuzama katika usiku wa Alhamisi.

Taarifa zinafahamisha kuwa watu wengine zaidi ya 40 hawajulikani walipo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na watu walionusurika katika ajali hiyo, katika mashua hiyo kulikuemo watoto zaidi ya 30.

30 September 2017, Kesi ya Malkia wa ndovu kusikilizwa siku nne mfululizo

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga kusikiliza kwa siku nne mfululizo, kesi ya kuhujumu uchumi inayowakabili washtakiwa watatu akiwemo raia wa China.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Salvius Matembo, Philemon Manase na raia wa China anayedaiwa kuwa ni Malkia wa Pembe za Ndovu, Yang Feng Glan (66) ambao kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya kuhujumu uchumi kwa kujihusisha na biashara haramu ya Meno ya Tembo yenye thamani ya Sh 13 bilioni, kinyume cha sheria.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu

Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shahidi baada ya pande wa utetezi na ule wa mashtaka kuiomba mahakama hiyo isikilize ushahidi kwa siku nne mfululizo.

Hata hivyo maombi hayo yalikubaliwa na Hakimu Shahidi ambaye alisema kuwa kesi hiyo itaendelea na ushahidi wa upande wa mashtaka kuanzia Oktoba 17 hadi 20.

Awali, Wakili wa Serikali Paul Kadushi aliiambia mahakama hiyo kwamba kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi lakini mashahidi wawili ambao walipaswa kutoa ushahidi wao jana, wapo mkoani kikazi, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanakabilia na kesi ya uhujumu uchumi kwa kujihusisha na biashara ya Meno ya Tembo yenye thamani ya Sh 13 bilioni.

Friday, September 29, 2017

29 September 2017,Arsenal yasonga mbele Europa ligi

Michuano ya Uefa Europa Ligi imepigwa usiku wa kuamkia leo kwa michezo mbalimbali hatua ya Makundi.

Klabu ya Arsenal ikiwa ugenini Imeshinda mabao 4-2 dhidi ya Bate Borisov, Everton imetoka sare ya bao 2-2 na Apollon, Ac Millan imeshinda 3-2 dhidi ya Rijea, Lyon pia wamefanikiwa kutoa sare na Atlanta baada ya kufungana bao 1-1.

Nice imeichapa Vitese mabao 3-0, Mainz imefungwa bao 1-0 na Hoffeinheim, Partizan imechapwa na Dynamo magoli 3-2 na Maccab Tel Aviv imetoka sare na Villareal 0-0.

Fc sheriff imetoshana nguvu na Koeben kwa sare ya kutofungana 0-0, Lugan imeambulia kipigo cha bao 2-1 dhidi ya FC FCSB ,Plesen imeichakaza Hapoel bao 3-0.

FC Cologne imefungwa bao 1-0 na FK Crvena Zvezda, Salzburg imeshinda bao 1-0 dhidi ya Marseille, Oestersunds FK imeichapa Hertha Berlin bao 1-0, Konyaspor imetakata kwa ushindi wa bao 2-1 na Vitoria de Guimaraes.

AEK Athens imetoshana nguvu na Austria Wien ya bao kwa kufungana bao 2-2.

29 September 2017, Watu saba wafariki ,sita kujeruhiwa kwa mlipuko wa bomu nchini Somalia

Maafisa usalama nchini Somalia wanasema mlipuko wa bomu la kwenye gari katika mji mkuu Mogadishu umewaua takriban watu saba na kuwajeruhi wengine sita.

Msemaji wa utawala wa Mogadishu Abdifatah Omar Halane ameiambia Sauti ya Amerika-VOA kwamba gari lililipuka Alhamisi karibu na kituo cha basi chenye harakati katika wilaya ya Hamarweyne.

“Kilichotokea ni bomu la kwenye gari lilipiga basi dogo watu saba wameuwawa na wengine sita kujeruhiwa Halane ameiambia VOA”.

Mashahidi kadhaa wameiambia VOA kwamba waathirika walikuwa ni raia wa nchini humo kutoka katika kituo cha basi na eneo la karibu.

Lengo maalum la mlipuko huo bado haliko bayana lakini walioshuhudia wanasema magari ya majeshi ya usalama ya serikali yalikuwa yanapita wakati mlipuko ulipotokea.

Hakuna aliyedai kuhusika na shambulizi.

29 September 2017,Shule 11 kati ya Shule 300 zilizokuwa zimefungiwa zaanza usajiri

WAMILIKI wa Shule binafsi 11 kati ya shule zaidi ya 300 zilizofungiwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala wamejitokeza kukamilisha usajili pamoja na taratibu nyingine ili waweze kuendelea kutoa elimu.

Shule hizo za awali na msingi ni zile zilizofungiwa tangu Agosti 16 mwaka huu baada ya kubainika kujiendesha kinyume cha sheria ikiwemo kukosa usajili na kutokuwa na eneo la kutosha kuendeshea shule hizo.

Mbali na hayo shule hizo pia zilibainika kubadilisha matumizi ya usajili kwani kuna ambazo zilisajiliwa kama ‘Day care’ lakini wamiliki wakabadilisha na kuzifanya kuwa ‘Nursery’ jambo ambalo ni kinyume cha usajili hivyo kupelekea kufungiwa mpaka hapo wamiliki watakapofuata utaratibu.

Akizungumza na gazeti hili jana Ofisa Habari wa Manispaa hiyo, Tabu Shaib alisema shule 11 tayari zimeanza kusajili ili kuendelea na ufundishaji. Alisema shughuli hiyo ni endelevu na sasa inafanywa na wenyeviti wa kata katika maeneo yote. Aliwataka wamiliki ambao wanajua kuwa shule zao haziendeshwi kwa kufuata sheria.

29 September 2017,Hofu kubwa yaongezeka juu ya hali ya kibinadamu magharibi mwa Afrika ya Kati

Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imeeleza wasiwasi mkubwa ilionao kutokana na kuzidi kuwa mbaya hali ya kibinadamu katika maeneo ya magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Najat Rochdi, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ametangaza kuwa, hali ya kibinadamu katika maeneo ya magharibi mwa nchi hiyo si ya kuridhisha.

Bi Najat Rochdi, amebainisha kuwa, kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu wa Septemba kwa mara nyingine tena hali ya kibinadamu katika maeneo hayo imezidi kuwa mbaya na kwamba, maelfu ya raia wamelazimika kuyahama makazi yao na kuwa wakimbizi baada ya makundi ya wabeba silaha kufanya mashambulio katika miji ya Niem na Bocaranga kwa lengo la kuidhibiti.

Afisa huyo wa Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ametahadharisha kwamba, endapo kutazuka tena mapigano katika maeneo ya magharibi mwa nchi hiyo basi hitajio la misaada ya kibinadamu katika hayo litaongezeka maradufu.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika dimbwi la mapigano na machafuko mwaka 2013 baada ya kuondolewa madarakani rais wa nchi hiyo, François Bozizé. Katika mapigano hayo maelfu ya watu waliuawa wengi wao wakiwa ni Waislamu na wengine wengi kuwa wakimbizi.

Hivi karibuni pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitahadharisha kuwa, yumkini Jamhuri ya Afrika ya Kati ikatumbukia tena katika mgogoro na machafuko makubwa ambayo yatavuruga jitihada za kurejesha amani na uthabiti katika nchi hiyo.

Thursday, September 28, 2017

28 September 2017,SIMBA:Tutaichakaza Yanga bila kujali uwanja tutaochezea

MABOSI wa Simba wamecheka sana baada ya kuusikia mpango ya Yanga wa kutaka kulihamishia pambano lao la watani litakalopigwa Oktoba 28, kuja kuchezwa jijini Mwanza, kisha wakaamua kuwajibu kuwa si CCM Kirumba tu, hata kama wanataka kwenda nje ya nchi wao freshi tu.

Mabosi hao wa Wekundu wa Msimbazi, wamesema wapo tayari kucheza na Yanga popote wanapotaka, lakini wajue wazi kuwa kipigo chao katika mchezo huo kipo palepale.

Simba na Yanga zinatarajiwa kucheza mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu Oktoba 28 ambapo Yanga watakuwa wenyeji na juzi kati walifichua kuwa wana mpango wa kuhamishia pambano hilo Kirumba, Mwanza.

Hii ni kutokana na Uwanja wa Taifa kuwa katika matengenezo na Uwanja wa Uhuru uliokuwa umepangwa awali utumike kwa mechi hiyo, kutowaridhisha na hasa suala zima la kukusanya mapato.

Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten, alisema wako katika mchakato wa kuiomba Bodi ya Ligi kuhamisha mchezo huo akidai Uhuru ni mdogo kulinganisha na mechi yenyewe ilivyo kubwa.

Lakini mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Said Tulliy, amesema wao kama Simba wako tayari mchezo huo kufanyika uwanja wowote hapa nchini kwa sababu wanaamini Yanga haiwezi kutoka salama mbele yao.

“Si Kirumba tu, hata kama Yanga watataka tukacheze nao nje ya nchi ni freshi tu kwa sababu sisi hatuna wasiwasi nao kwa kikosi tulichonacho na namna msimu huu tulivyojiandaa kuwatia adabu,” alisema Tulliy.

Tulliy alisema Simba ina mashabiki kila kona ya Tanzania hivyo hawana wasiwasi wowote.

“Tuko tayari kucheza uwanja wowote ule hivyo Yanga wakitaka tucheze Kirumba sawa kwani Simba tuna mashabiki wengi sana kila mkoa, tunao hata nje ya nchi, hivyo watani zetu wasitapetape, tutawafuata popote,” alisema Tulliy.

Tulliy aliyasema hayo kwenye mkutano na wanahabari uliofanyika jana Jumatano jijini hapa ambao ulizungumza pia ishu nzima ya Kocha Joseph Omog, Simba wakisisitiza kuwa bado yupo sana Msimbazi tofauti na habari zinazovumishwa kuwa yupo mbioni kutimuliwa kazi.

Katika kuonyesha kuwa mechi hiyo ya watani haitapigwa jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amenukuliwa akisisitiza kuwa mchezo huo hautaweza kuchezwa Uwanja wa Taifa kwa vile uwanja huo unaendelea kukarabatiwa na utakamilika baada ya miezi mitatu.

Waipigia hesabu Stand

Katika hatua nyingine Simba imeanza kuzipigia hesabu pointi tatu za Stand United watakaocheza nao Jumapili hii kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Mratibu wa Simba, Abbas Ally, alisema wachezaji wote wapo fiti kuelekea mchezo huo, huku Shiza Kichuya akirejea kikosini baada ya kuumia katika mchezo uliopita dhidi ya Mbao FC.

Naye Msemaji wa Simba, Haji Manara, alisema timu hiyo inatarajiwa kuondoka kesho (Ijumaa) kuelekea Shinyanga kwa ajili ya mpambano huo.

“Tunakwenda Shinyanga kwa lengo la kupata pointi tatu muhimu tunajua tuko ugenini lakini tutapambana kuhakikisha tunapata ushindi,” alisema Manara.

28 September 2017, Wakimbizi laki moja wa Nigeria watimuliwa Cameroon

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limekosoa vikali hatua ya Cameroon kuwafukuza nchini wakimbizi zaidi ya laki moja raia wa Nigeria.

Gerry Simpson, Mkurugenzi Mkuu wa masuala ya wakimbizi wa shirika hilo amesema mbali na jeshi la Cameroon kuwatimua wakimbizi na raia wanaotafuta hifadhi wa Nigeria kutoka nchini humo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, pia limewatesa na kuwakandamiza wengine wengi miongoni mwao.

Amesema kitendo hicho cha kuwarejesha wakimbizi hao nyumbani ambako walikimbia mauaji na mateso ya kundi la kigaidi la Boko Haram huenda kikasababisha moja ya migogoro mikubwa kabisa ya kibinadamu duniani.

Waziri wa Mawasiliano wa Cameroon amekataa kuongea na waandishi wa habari kuhusu kadhia hiyo ya kutimuliwa wakimbizi wa Nigeria.

Haya yanajiri katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa hivi karibuni ulionya kwamba karibu watu milioni 8.5 katika maeneo yaliyoathiriwa na mashambulizi ya Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa Nigeria wanahitaji misaada ya kibinadamu.

Shirika la Kushughulikia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema nalo limewahi kurekodi visa vya kutimuliwa na kukandamizwa wakimbizi wa Nigeria walioko katika nchi jirani ya Cameroon.

28 September 2017,Maalim Seif aelezea hali ya Afya ya Lissu

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ameeleza maendeleo ya afya ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), baada ya kumtembelea hospitalini Nairobi, Kenya.

Akihojiwa na Redio ya Idhaa ya Kiswahili Deutsche Welle (DW) ya Ujerumani jana, Maalim Seif alisema Lissu anaendelea vizuri na hajapoteza mwelekeo.

“Jana (juzi) nilimtembelea Lissu na nilipata moyo sana, kwa kweli anaendelea vizuri ukizingatia mtu ambaye alipigwa risasi zaidi ya 30, anapata nafuu haraka haraka.

“Bado hajapoteza mwelekeo akili yake ipo timamu, ametuhakikishia haya yaliyotokea hayatamrudisha nyuma katika kuwatetea wanyonge.

“Anazungumza vizuri, yuko makini sana anajua anachokisema na mimi nimepata moyo jinsi nilivyomuona,” alisema Maalim Seif.

Alisema kutokana na mambo yanayoendelea nchini, lazima kuwapo na mjadala wa taifa kuona tumekosea wapi na kujirekebisha.

“Mambo kama haya kutokea Tanzania ni jambo ambalo kila Mtanzania lazima aingiwe na wasiwasi kwa sababu hakuna hata mmoja na hasa mwanasiasa ambaye ana usalama wa maisha yake.

“Kama taifa tuzungumze kuona tumekosea wapi na kujirekebisha,” alisema.

Kuhusu uchunguzi wa tukio hilo, alisema hata kama vyombo vya dola vya ndani vitafanya si aibu kwa nchi kutafuta msaada kwa wengine.

“Yako mambo mengine yaliyotokea huko nyuma na bado hatujaaambiwa yalikwenda vipi, tunaambiwa tu uchunguzi unaendelea. Ni vizuri wananchi waone matokeo ya uchunguzi huo…si aibu kwa nchi kutafuta msaada kwa wengine,” alisema.

Lissu alipigwa risasi zinazokadiriwa kufikia 32, Septemba 7, mwaka huu, alipokuwa akirejea nyumbani kwake Area D mjini Dodoma baada ya kutoka kuhudhuria kikao cha Bunge na kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake.

28 September 2017,SMZ:Yabainisha mambo manne yatajayoimarisha Mahakama ya kadhi

Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imebainisha mapendekezo manane iliyoyawasilisha kwenye Baraza la Wawakilishi ambayo yatatumika kuimarisha Mahakama ya Kadhi, huku ikipendekeza kufutwa kwa sheria iliyounda mahakama hiyo.

Katika mapendekezo yake, SMZ imeyataja baadhi ya mambo inayotaka kuyatumia kuboresha mahakama hiyo kuwa ni pamoja na mamlaka ya Mahakama ya Kadhi, ushahidi, kanuni na taratibu za utendaji kazi, muda wa utumishi wa viongozi wakuu wa mahakama hiyo, uwezo wa mahakama, uwepo wa mrajisi wa mahakama na lugha itakayotumika.

Katika mapendekezo yake, Serikali inapendekeza kufutwa kwa Sheria namba 3 ya mwaka 1985 iliyounda mahakama hiyo ikitaka kuanzisha sheria mpya pamoja na kuweka masharti mengine. Mapendekezo hayo yaliwasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi ‘Gavu’ katika mkutano wa saba wa Baraza la Wawakilishi unaoendelea Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Akiwasilisha mapendekezo hayo, Issa alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kuonekana sheria inayotumika hivi sasa ina upungufu mwingi wa kisheria.

Alisema licha ya ukosefu wa kanuni nzuri za kuendesha mahakama hiyo, sheria haielekezi utaratibu wa usuluhishi ambao ungesaidia kupunguza idadi ya kesi zilizopo mahakamani na pia haiwapi uwezo makadhi kuwashughulikia watu wanaodharau au kutotoa ushahidi unaotakiwa.

“Wengi wanaopata matatizo makubwa katika suala la upatikanaji wa haki katika Mahakama ya Kadhi ni wanawake na watoto hasa baada ya ndoa zao kuvunjika, hivyo tunaamini kuja kwa muswada huu kutasaidia makundi hayo kupata haki zao stahiki na kwa wakati,” alisema Issa.

28 September 2017, Wabunge wa Uganda watwangana makonde Bungeni

Kwa siku ya pili mfululizo, Wabunge wa Uganda wamerushiana makonde Bungeni wakati wa kujadiliwa muswada wa sheria inayotaka kuondoa kikomo cha umri wa kugombea urais nchini humo.

Kadhalika Spika wa Bunge Rebecca Kadaga ameagiza kutolewa kwa nguvu nje ya majengo ya Bunge Waziri mmoja na Wabunge 25 wanaodaiwa kuzusha vurumai hapo jana, aghalabu yao wakiwa wa upinzani.

Hapo jana wabunge wa chama tawala NRM na wale wa upinzani waliligeuza Bunge kuwa uwanja wa masumbwi na kutwangana makonde huku wengine wakirushiana viti.

Haya yanaarifiwa huku Kamisheni ya Mawasiliano ya nchi hiyo (UCC) ikisimamisha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge.

Godfrey Mutabazi, Mkurugenzi Mkuu wa UCC amesema idhaa au runginga yoyote itayopeperusha matangazo ya Bunge mubashara itajiweka katika hatari ya kupokonywa leseni, chini ya ibara ya 41 ya Sheria ya Kamisheni hiyo ya mwaka 2013.

Museveni mwenye umri wa miaka 73, ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miongo mitatu, kisheria hafai kuwania tena urais katika uchaguzi mkuu wa 2021 kwa sababu katiba ya Uganda imeainisha miaka 75 kuwa kikomo cha umri wa mtu anayetaka kugombea urais.

Wednesday, September 27, 2017

27 September 2017,PLUIJM: Nilazima wachezaji wangu wacheze kwa kiwango cha juu dhidi ya Azam

KOCHA wa Singida United,Hans Van Pluijm amesema ili kupata pointi tatu dhidi ya Azam FC ni lazima wachezaji wake wacheze kwa kiwango cha juu.
Kocha huyo alisema wanafahamu rekodi ya Azam kutoruhusu bao lolote mpaka sasa hivyo ni lazima washambuliaji wake wafanye kazi ya ziada ili kuvunja ukuta wao.
"Ili ushinde mechi unatakiwa kufunga mabao, na hilo halijalishi unacheza na timu ya aina gani. Azam hawajaruhusu bao lakini kama tunataka kushinda ni lazima tuwafunge," alisema.
"Utakuwa ni mchezo mgumu, lazima tucheze kwa kiwango cha juu zaidi ya tulivyofanya kwenye michezo iliyopita, tujitume zaidi," alifafanua.


27 September 2017, Kisiwa cha Zanzibar, kivutio namba moja ulimwenguni kwa watalii

Kisiwa cha Zanzibar ni kisiwa kilichojaaliwa na maliasili ya kila namna.

Kisiwa hicho ni sehemu ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Kisiwa cha Zanzibar huvutia watalii wengi ulimwenguni hasa kutokana na miundominu yake ya kipekee na utandawazi ulioletwa na waarabu,wazungu,wahindi na waafrika wenyewe.

Mahanjumati na wanyama kisiwani humo ni kati ya vitu vinavyokiongezea kisiwa hicho umaarufu.

27 September 2017,CHADEMA yamtumbua katibu wake Moshi

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Kilimanjaro, kimezifuta barua walizoandikiwa madiwani sita wa Halmashauri ya Moshi, wakitakiwa kujieleza kwa usaliti.

Mbali na kufuta barua hizo zilizokuwa zimeandikwa na Katibu wa Chadema Wilaya ya Moshi, Emmanuel Mlaki chama hicho kimemsimamisha uongozi katibu huyo.

Madiwani hao akiwamo Mwenyekiti wa Halmashauri, Michael Kilawila walitakiwa kujieleza kwa madai ya usaliti kwa kumchagua makamu mwenyekiti wa halmashauri kutoka NCCR-Mageuzi.

Chadema na NCCR-Mageuzi ni vyama washirika katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), unajumuisha pia CUF na NLD.

Taarifa iliyotolewa leo na Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema imesema barua zilizoandikwa na Mlaki ni batili na ameagiza ziondolewe katika rekodi za chama hicho.

“Tunautangazia pia umma kuwa Emmanuel Mlaki amesimamishwa uongozi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake na tunautaka umma kusitisha mawasiliano rasmi ya chama kupitia kwake.”

27 September 2017, Wanawake nchini Saudia Arabia wataanza rasmi kuendesha magari 2018

Mwanamke wa Saudia katika kampeni ya kukaidi wanawake kutoendesha magari.

Saudi Arabia itawaruhusu kwa mara ya kwanza wanawake kuendesha magari kwa mujibu wa amri iliyotolewa na mfalme wa nchi hiyo.

Vyombo vya habari vimeripoti Jumanne kuhusu amri hiyo ya kifalme ambayo inataka leseni za kuendesha magari zitolewe kwa wote wanaume na wanawake.

Aidha nchini  hio sasa ndio  nchi pekee ambapo inawazuia wanawake kuendesha magari.

Shirika la habari la Saudi Arabia -SPA limeripoti kuwa amri hiyo itaanza kutumika rasmi mwezi Juni mwaka 2018.

Wanawake nchini Saudia Arabia wataanza rasmi kuendesha magari 2018

Mwanamke wa Saudia katika kampeni ya kukaidi wanawake kutoendesha magari.

Saudi Arabia itawaruhusu kwa mara ya kwanza wanawake kuendesha magari kwa mujibu wa amri iliyotolewa na mfalme wa nchi hiyo.

Vyombo vya habari vimeripoti Jumanne kuhusu amri hiyo ya kifalme ambayo inataka leseni za kuendesha magari zitolewe kwa wote wanaume na wanawake.

Aidha nchini  hio sasa ndio  nchi pekee ambapo inawazuia wanawake kuendesha magari.

Shirika la habari la Saudi Arabia -SPA limeripoti kuwa amri hiyo itaanza kutumika rasmi mwezi Juni mwaka 2018.

27 September 2017, Maalim Seif awaunganisha madiwani wa CUF

Mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbarouk amesema mgogoro wa madiwani wa CUF umemalizwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Mbarouk alisema Maalim Seif alikaa na madiwani hao jijini Dar es Salaam na kuwaamuru waingie kwenye vikao vya Halmashauri ya Jiji la Tanga ili kuwaletea maendeleo wananchi.

Mbunge huyo ambaye wiki iliyopita alituhumiwa na baadhi ya madiwani waliosimamishwa kuhusika kumchochea Meya wa Jiji la Tanga, Mhina Mustafa (Selebosi) kuwapa adhabu hiyo, alikanusha tuhuma hizo.

CUF ina madiwani 20 ambao kati yao, 12 waliamua kuingia kwenye vikao vya Baraza la madiwani mwaka jana na kutuhumiwa kukisaliti chama, lakini baadaye wenzao wanane nao waliingia huku wakilalamika kutengwa na kunyimwa stahiki zao.

Naye Naibu Meya wa Jiji la Tanga, Mohamed Haniu (CUF) alisema kitendo cha madiwani 20 wa CUF kuingia kwenye vikao kimesababisha wenzao na wale CCM kuelekeza nguvu zaidi kwenye maendeleo.

Tuesday, September 26, 2017

26 September 2017, Mtoto wa siku moja atupwa chooni Wilayani Ilemela Jijini Mwanza, wananchi wafanikiwa kumukoa akiwa hai

Mtoto mchanga wa kike anayekadiliwa kuwa na umri wa siku moja ameokotwa kwenye shimo la choo kinachotumika katika mtaa wa Lumala Kata ya Kawekamo Wilayani Ilemela mkoani Mwanza akiwa hai baada ya kutupwa na mzazi wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema baada ya muda mchache kupita toka kichanga hicho kutupwa kwenye shimo hilo la choo, polisi walipata taarifa na kwenda kusaidia kumtoa mtoto huyo ambaye sasa amepelekwa hospitali ya Sekou Toure kwa matibabu zaidi.

"Inadaiwa kuwa baada ya muda mchache kupita toka mtoto alipotupwa, palikuwa na mtu aliyekwenda kujisaidia chooni ndipo akiwa chooni alisikia sauti ya mtoto mchanga akilia toka ndani ya shimo la choo. Inasemekana kuwa baada ya mtu huyo kusikia sauti hiyo ya mtoto akilia, alikwenda kutoa taarifa kwenye uongozi wa serikali za mtaa ambapo uongozi wa mtaa ulifika mahali hapo kisha ulitoa taarifa kituo cha polisi" alisema Msangi na kuongeza;

"Askari baada ya kupokea taarifa hiyo walifanya ufuatiliaji wa haraka hadi eneo la tukio na kushirikiana na wananchi waliokuwepo eneo hilo na kufanikiwa kutoa kichanga hicho cha mtoto toka ndani ya shimo la choo kikiwa hai. mtoto amepelewa hospitali ya mkoa ya sekou toure kupatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri. Polisi wapo katika upelelezi na msako katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mwanza, ili kuweza kubaini mzazi/wazazi wa mtoto huyo ambao wamefanya ukatili huo dhidi ya mtoto, ili baadae waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao na iwe fundisho kwa wengine".

Kamanda Msangi ametoa wito kwa wazazi na walezi kuacha tabia ya kutenda ukatili dhidi ya watoto ikiwepo vitendo vya kutupa watoto kwani ni kosa la jinai na endapo mtu atabainika kufanya hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake

26 September 2017,Madaktari bingwa kumi ,kwa masaa kumi wamuokoa Lissu

Jumla ya madaktari bingwa 10 walitumia saa 10 kwa ajili ya kunusuru maisha ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma hadi Uwanja wa Ndege kabla ya kusafirishwa Nairobi.

Muda huo ulijumuisha tangu Lissu alipopigwa risasi saa 7:30 mchana Septemba 7, 2017 akiwa nyumbani kwake mtaa wa Area D mjini hadi aliposafirishwa kwenda Nairobi nchini Kenya saa 6:17 usiku.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk James Kiologwe akizungumza na Mwananchi amesema lilikuwa tukio lenye changamoto zake.

“Nina timu nzuri kwa maana nina uongozi mzuri wa hospitali ya mkoa lakini nina madaktari na watoa huduma ambao wana ‘commitment’ ya hali ya ajabu,” amesema.

Amesema wakati tukio hilo linatokea yeye alikuwa mbali kidogo na hospitali lakini baada ya kupata taarifa na kufika alikuta tayari Lissu ameshaanza kuhudumiwa.

“Tulikuwa na timu ya zaidi ya watu 20 ambao walishiriki kwa njia mbalimbali. Unajua kuna ushiriki wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja. Kwenye macho ya watu huwa anaonekana daktari pekee lakini ukweli ni kwamba hawezi kufanya kazi pekee yake lazima wawepo watu wengine,”amesema.

Amesema kati ya timu hiyo 10 walikuwa ni madaktari bingwa katika fani mbalimbali walikuwa kazini wakati huo ambao Lissu anafikishwa hospitalini baada ya kuumia. Pia katika timu hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya ambaye ni mtaalam bingwa wa usingizi alishiriki hadi saa 6.17 usiku Uwanja wa Ndege wa Dodoma kabla ya Lissu kwenda jijini Nairobi nchini Kenya.

Hata hivyo, amesema walikuwa na vitendea kazi vya kutosha na ndio maana walisema kuwa wanaweza kumhudumia mgonjwa huyo.

“Jambo hilo halikuwa na nia ya kuwatuliza watu hapana, bali lilikuwa linamaanisha kuwa uwezo tunao kweli,”amesema

“Ni kweli tukio kama lile lilikuwa na changamoto zake. Changamoto ya kwanza ni tukio ambalo limewagusa watu wengi sana kisaikolojia.

Watu wengine wangependa kumuona mgonjwa kwa hiyo mwananchi anaweza kukimbia kuja kumuona,” amesema.

Hata hivyo, amesema hawakuweza kuwaruhusu kwa sababu za kiutaratibu ambapo kwa muda huo madaktari wanahitaji zaidi kuokoa maisha ya mgonjwa. “Suala la kumuona na kujua ameumiaje wakati huo hauwezi kumsaidia kwa wakati huo halikuwa muhimu.

Niwashukuru sana wananchi wa Dodoma pamoja na viongozi walikuwa ni wasikivu unapowapa maelekezo walikuwa wanatekeleza,”amesema.

Amesema walipata ushirikiano wa hali ya juu kutoka kwa watu mbalimbali wakati wa tukio hilo jambo ambalo liliwasaidia katika utekelezaji wa kazi hiyo.

26 September 2017,Wafungwa 34 wametoroka gerezani mashariki mwa Kongo

Afisa mmoja nchini DRC anasema wafungwa 34 wametoroka gerezani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC baada ya kuuvunja ukuta wakati wa mvua mkubwa iliyokuwa inanyesha.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Asociated Press-AP waziri wa sheria wa jimbo la kivu kusini Pasaline Basezage alisema Jumatatu kwamba takriban wafungwa 27 waliotoroka Jumapili jioni walikuwa wamekutwa na hatia kwa makosa ya uhalifu wa ngono na vitendo vingine vya ghasia.

Gereza la Mwenga lililopo kiasi cha kilometa 130 kusini ambalo lilikuwa linawashikilia wafungwa 42 wakati huo.

Afisa wa gereza la Mwenga, Desire Masumbuko alisema majeshi ya usalama yamewakamata wafungwa wanne waliotoroka.

Afisa Masumbuko aliwataka wakazi kuwa katika hali ya tahadhari na kushirikiana katika kuwasaka wafungwa waliobaki.

Maelfu ya wafungwa wameshawahi kufanikiwa kutoroka gerezani kote nchini Congo tangu mwezi Mei wakati wanachama wa dhehebu moja la kikristo walipovamia gereza moja mjini Kinshasa.

Walioshuhudia wanasema maelfu ya wafungwa walitoroka.

26 September 2017, Wakazi wa Bukavu, Kongo waandamana juu ya ukosefu wa usalama

Wakazi wa mji wa Bukavu, katikati ya mkoa wa Kivu Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamefanya maandamano makubwa kulalamikia machafuko yanayoendelea katika mkoa huo.

Katika maandamano hayo inaelezwa kuwa mtu mmoja amefariki na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya kufyatuliwa risasi na polisi wa serikali.

Habari zinaarifu kwamba, maandamano hayo yaliyofanyika katika eneo la watu masikini la Panzi, mjini Bukavu yalikabiliwa na polisi wa kutuliza ghasia ambapo imetangazwa kuwa mtu aliyeuawa kwa kupigwa risadi ni mwanafunzi aliyekuwa na umri wa miaka 14.

Watu walioshuhudia wamesema kuwa, waandamanaji sambamba na kuchoma moto matairi ya magari, walifunga barabara sambamba na kukitia moto kituo kidogo cha polisi cha eneo hilo la Panzi.

Awali uongozi wa kata ya Mwenga ya mkoa wa Kivu Kusini, ilitangaza habari ya kutoroka jela wafungwa 34 kutoka jela ya katikati ya eneo hilo, Jumapili iliyopita ambapo polisi ilifanikiwa kuwatia mbaroni wafungwa watatu kati yao.

Machafuko na ukosefu wa amani vinaendelea kushuhudiwa katika maeneo ya mashariki na kaskazini mwa Kongo kwa zaidi ya miaka ishirini sasa.

Kushindwa jeshi na kikosi cha wanajeshi wa Kofia Bluu wa Umoja wa Mataifa kuwaangamiza wanamgambo kumezidisha hali ya mchafukoge mashariki mwa nchi hiyo.

Monday, September 25, 2017

25 September 2017,Trump avutana wa wanamichezo Marekani juu ya wimbo wa taifa

Wachezaji wa Timu za Baltimore Ravens na Jacksonville Jaguars za marekani wameonyesha kutofurahia utofauti uliopo kati ya Rais Dolnald Trump na wanamichezo,kwa kushindwa kuheshimu wimbo wa taifa wa marekani ukipigwa katika uwanja wa Wimbley ikiwa ni inshara ya kuonyesha Umoja wa kumpinga Trump dhidi ya wanamichezo.

Shahid Khan kiongozi wa Timu ya JacksonVille Jaguars aliungana na wachezaji kupinga yanayofanywa na Rais Trump.

Trump ameandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii kulaani walichokifanya wachezaji kukaidi kuheshimu wimbo wa taifa.

25 September 2017,Mwakyembe amepiga marufuku tuzo za muziki , mashindano ya Miss nchini

Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Harrison Mwakyembe amepiga marufuku mashindano ya Miss Tanzania na tuzo za muziki kutokana na ubabaishaji wa waandaaji wa mashindano ya tasnia hizo.

Mwakyembe amesema mashindano ya Miss Tanzania yamegubikwa na ubabaishaji kwenye utoaji wa tuzo na kumekuwa na tabia ya kuchelewa kuwapa washindi zawadi wanazoahidiwa jambo linaloleta usumbufu.

Waziri huyo ameongeza kuwa watakaotaka kuandaa mashindano hayo ni lazima zawadi wanazoahidi kuwapa washindi zipekwe ofisini kwake.

”Kwa sasa tunanakaa chini na wadau wa burudani juu ya mashindano hayo ila tunataka tuzo ziwe na (guaranteed sustainability) muendelezo wa uhakika na sio kufanyika kwa kubahatisha”, alisema Mwakyembe.

Kwa mara ya mwisho mashindano ya za Miss Tanzania yalifanyika mwaka 2016 ambapo ilichukua takribani miezi 6 kwa Kamati ya shindano la Urembo la Miss Tanzania kumpatia mshindi zawadi yake.

Kwenye tuzo za muziki waziri Mwakyembe amesema tuzo hizo zinahitaji marekebisho kwani zilikuwa zikitegemea watu wachache kiasi kwamba wakinuna basi hakuna tuzo.

25 September 2017,Zaidi ya misikiti na makanisa 50 Palestina imevunjwa na Israel

Walowezi wa Kizayuni wamevunja misikiti na makanisa yasiyopungua 53 katika kipindi cha miaka minane (8) iliyopita katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Kituo cha upashaji habari cha Palestina jana (Jumapili) kilitangaza kwamba, kwa mujjibu wa ripoti za karibuni kabisa, tangu mwaka 2009 hadi hivi sasa, walowezi wa Kizayuni na wanajeshi wa Israel wamefanya uhalifu mkubwa katika maeneo matakatifu ya Waislamu na Wakristo huko Palestina.

Wataalamu wa mambo wanasema kuwa, katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, utawala wa Kizayuni wa Israel umetangaza vita rasmi vya kidini dhidi ya Wapalestina bila ya kujali itikadi na dini zao.

Ni jambo lililo wadhiha kwa watu wote, kwamba utawala wa Kizayuni hauheshimu mafundisho ya dini yoyote ile, hususan pale yanapokwenda kinyume na fikra za Kizayuni.

Jana Jumapili pia, Wazayuni walishambulia vitongoji kadhaa vya Wapalestina vikiwemo vya al Khalil na Qalqilya na kuwateka nyara Wapalestina wasiopungua 14.

Kila siku wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni wa Israel wanavamia maeneo ya Wapalestina na kuwateka nyara vijana wa taifa hilo madlumu bila ya makosa yoyote.

Takwimu za taasisi mbalimbali za Palestina zinasema kuwa, hivi sasa kuna Wapalestina 6400 katika jela za kuogofya za Wazayuni huku 62 kati ya Wapalestina hao wakiwa ni wanawake na 300 wengine ni watoto wadogo.

25 September 2017,Askari nane wa UN wameuawa, watano kujeruhiwa katika mripuko nchini Mali

Wanajeshi watatu wa Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA wameuawa katika mripuko wa bomu uliotokea kaskazini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Taarifa ya MINUSMA imesema askari wengine watano wa umoja huo wamejeruhiwa katika shambulizi hilo lililotokea alfajiri ya leo.

Habari zinasema kuwa, askari hao wa Umoja wa Mataifa walikuwa wanasindikiza msafara wa magari yaliyokuwa yakitokea mji wa Anefis kuelekea Gao, magharibi mwa nchi.

Hata hivyo taarifa hiyo ya MINUSMA haijaainisha uraia wa wanajeshi hao wa UN waliouawa katika mripuko huo.

Koen Davidse, Mkuu wa Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa: "Tunatoa mkono wa pole kwa familia za wahanga wa hujuma hii ya kinyama. Tutafanya juu chini kuhakikisha kuwa haki inapatikana."

Hayo yamejiri siku chache baada ya Mali kufungua kambi mpya kwa ajili ya majeshi ya nchi tano za Afrika ambayo yatakuwa na jukumu la kupambana na wanamgambo katika eneo la Sahel Afrika.

Licha ya Ufaransa kuwa na askari wengi nchini humo, lakini imeshindwa kurejesha usalama na amani na badala yake makundi ya wanamgambo yenye mafungamano na mtandao wa al-Qaida yamekuwa yakijiimarisha kijeshi kila uchao nchini humo

25 September 2017,Watanzania walionusulika na ajali Uganda kurejea Nchini

Majeruhi watano walionusurika kwenye ajali ya gari iliyopoteza maisha ya Watanzania 13 nchini Uganda mapema wiki hii wanarejea kesho.

Majeruhi hao walihusika kwenye ajali ya gari iliyohusisha basi dogo la kukodi aina ya Toyota Coaster lenye namba za usajili T 540 DLC wakati wakitokea nchini Uganda kuhudhiria harusi ya daktari binti wa Kitanzania, Dk Annette Teu na mumewe Dk Treausuer Ibingira ambaye ni raia wa Uganda.

Baada ya ajali hiyo Watanzania hao watano walilazwa kwenye Hospitali ya Nsambya iliyopo jijini Kampala ambapo juzi jioni waliruhusiwa kutoka hospitalini hapo. Akizungumza na Gazeti hili kwa njia ya simu kutokea jijini Kampala, Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Grace Mgovano alifafanua kuwa walifikia nyumbani kwake na kwa sasa wanajiandaa kwa safari yao hiyo ya kesho.

Alisema, wanaendelea vema na wamepata ahueni kubwa ikilinganishwa na ilivyokuwa mwanzo na kuongeza kuwa wakiwasili Dar es Salaam wataendelea na taratibu za kuonana na madaktari kwa uangalizi wa kawaida. Grace aliwataja Watanzania hao kuwa ni Erasto Teu, Esther Alex, Severia Sanga, Irene Lyatuu na Dativa Shayo.

Sunday, September 24, 2017

24 September 2017, Lissu aizuia familia yake kuandika barua ya Matibabu Serikalini

Familia ya mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu, imesema imezuiliwa kuandika barua kwa ajili ya kuiomba serikali kugharamia matibabu ya mbunge huyo kwa madai amehaidi suala hilo atakuja kulishughulikia yeye mwenyewe hivi karibuni.

Hayo amebainisha kaka wa mbunge huyo ambaye pia ni msemaji wa familia, Alute Mughwai baada ya kupita siku kadhaa tokea serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kutoa kauli yao ya kusema mgonjwa ni mbunge ambaye anayehitaji matibabu zaidi lakini kwa kuwa yupo nje ya utaratibu wa serikali na ili serikali iweze kushiriki ni lazima yawepo maombi ya kufanya hivyo.

"Majira ya saa nne hivi niliweza kuzungumza na Mhe. Tundu Lissu akiwa hospitalini Nairobi baada ya kumjulia hali nilimueleza taarifa ya Mhe. Waziri kwamba tuandike barua ili aweze kupata matibabu kwa gharama za serikali, akanijibu kuwa jambo hilo atalizungumzia yeye mwenyewe siku za hivi karibuni. Kwa sababu yeye anaamini ni mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye anahaki zote anazostahili kulipwa, kama mbunge ikiwa ni pamoja na kupatiwa matibabu endapo ataugua au atapatwa na maradhi", amesema Alute.

Pamoja na hayo, kaka wa Lissu ameendelea kwa kusema "Mpaka hivi sasa jeshi letu la polisi halijaweza kumkamata mshtakiwa yeyote juu ya tukio la Lissu wakati jambo hilo lilitokea mchana kweupe na watu wengi walishuhudia. Sasa mazingira hayo yametupa wasiwasi kama tukio hilo litachunguzwa kikamilifu, hatuna wasiwasi na uwezo wa polisi wetu kufanya huo uchunguzi lakini shida yetu ni utayari".

Aidha, Alute amesema wameshamuandikia barua Mwanasheria Mkuu wa serikali ili waweze kupatiwa msaada wa kiuchunguzi zaidi dhidi ya tukio hilo lililomtokea ndugu yake.

"Barua tumeandika Septemba 16, mwaka huu kwenda kwa Mwanasheria Mkuu wa serikali maana ndiyo mamlaka inayopaswa kuchukua hatua za kuombwa msaada wa kiupelelezi kwa niaba ya serikali yetu huko nje ya nchi, na hiyo barua nimeinakili kwa Mhe. Waziri Sheria na Mambo ya Katiba", amesisitiza Alute.

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alishambuliwa na risasi nje ya nyumba yake mjini Dodoma wakati akitokea Bungeni na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 na mwishowe kukimbiziwa katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.

24 September 2017, Uchaguzi mkuu waanza Ujerumani

Ujerumani wameanza kuelekea kwenye masanduku ya kupigia kura hii leo katika uchaguzi wa taifa ambao unatazamiwa kumpa ushindi kwa muhula wa nne Bi Angela Merkel kama Kansela wa nchi hiyo.

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa leo asubuhi kuanzia saa mbili na vitakuwa wazi hadi jioni saa 12 kwa majira ya Ujerumani. Raia wasiopungua milioni 61. 5 waliotimiza masharti ya kupiga kura wanashiriki katika uchaguzi wa leo.

Kansela wa Ujerumani anagombea nfasi hiyo kwa muhula wa nne huku akijaribu kuhifadhi nafasi ya chama chake cha Christian Democrat (CDU), ambacho kinatambulika kama kundi kubwa zaidi katika bunge la taifa la Ujerumani, "The Bundestag."

Katika uchaguzi wa leo, Angela Merkel anachuana vikali na Martin Schulz ambaye ni kiongozi wa chama cha Social Democrats cha mrengo wa kushoto-kati (SPD) ambaye ni mkuu wa zamani wa bunge la Ulaya.

24 September 2017,ARUSHA:Diwani ajiuzuru mbele ya Rais Magufuli

Katika hali ambayo haikutarajiwa, Diwani wa Kata ya Kimandolu Jiji la Arusha (Chadema), Mchungaji Rayson Ngowi akiongozwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ametangaza kumuunga mkono Rais John Magufuli na kwa kuachia nafasi yake.

Alifanya hivyo jana mbele Rais Magufuli wakati madiwani 10 wa Chadema waliojiuzulu nafasi zao kwa nyakati tofauti kwenye halmashauri tatu za Arusha na kujiunga na CCM walipoitwa wakati Rais alipokuwa akihutubia baada ya kutunuku kamisheni kwa maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Hatua hiyo inafanya jiji la Arusha linaloongozwa na Chadema kupoteza kata mbili.

Madiwani wengine waliojitambulisha mbele ya Rais Magufuli ni wale waliojiuzulu katika halmashauri za Meru na Arusha Vijijini.

Mchungaji Ngowi ndiye aliyekuwa wa kwanza kupanda jukwaani na kuanza kumwagia sifa Rais Magufuli, “Mwanzoni nilikuwa sikuelewi lakini sasa nakuelewa sana. Nataka Watanzania wote wakuunge mkono. Tunaona jitihada zako za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya asali na maziwa. Tuko pamoja na nashukuru sana kwa kunipokea.”

Mwingine aliyepanda jukwaani ni aliyekuwa Diwani wa Muriet, Credo Kifukwe ambaye alisema, “Nimeamua kumuunga mkono Magufuli kutokana na kazi nzuri alizofanya na kila mwenye akili timamu anaona. Huko tulikokuwa ilikuwa mambo ya pingapinga hawataki kuona mazuri yanayoendelea, nimeamua kurudi CCM hapa kazi tu.”

Baadaye Rais Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM alisema, “Hawa wananchi wanataka maendeleo kuliko majina ya vyama na maendeleo hayajali wewe ni CCM , Chadema au CUF.”

Hata hivyo, alionyeshwa kushangazwa na madiwani hao kuacha haki zao zikiwamo masilahi mengine na kuamua kujizulu nafasi zao na kuwakaribisha CCM.

Pia, aliutaka uongozi wa CCM kuwapitisha madiwani hao kuwania tena nafasi hizo ili wakashindane na vyama vingine.

24 September 2017, Viongozi wa Myanmar wahukumiwa juu ya mawauaji yanayotokea nchini humo

Mahakama ya Kimataifa ya Kudumu ya Watu wa Malaysia imetoa hukumu dhidi ya serikali ya Myanmar kutokana na kutenda jinai za mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.

Mahakama hiyo ambayo kuanzia siku ya Jumatatu hadi Ijumaa ya jana ilikuwa ikichunguza vitendo vya ukandamizaji wa serikali ya Myanmar na mauaji dhidi ya Waislamu hao, imeipata na hatia serikali ya Naypyidaw kwa kuhusiaka na jinai hizo.

Uamuzi wa mahakama hiyo uliotolewa na majaji saba imesema kuwa, serikali ya Myanmar umetenda jinai za kivita dhidi ya Waislamu wa Rohingya na hivyo viongozi wake wanapaswa kuwajibishwa.

Baada ya hukumu hiyo, Daniel Feierstein Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Uchunguzi wa Mauaji ya Kizazi sambamba na kuthibitisha kwamba kumetokea mauaji ya kizazi dhidi ya Waislamu wa Rohingya yaliyofanywa na serikali ya Myanmar amesema kuwa, mahakama hiyo imetoa uamuzi kwamba serikali ya nchi hiyo imefanya mauaji ya kimbari kwa makusudi dhidi ya Waislamu.

Karibu Waislamu laki nane wa jamii ya Rohingya wamekimbilia Bangladesh kutokana na mashambulizi makali yanayofanywa na askari wa serikali kwa wakishirikiana na Mabudha magaidi wa nchi hiyo na hadi sasa ripoti zinaonyesha kwamba, mauaji hayo bado yanaendelea.

Kwa mujibu wa ripoti zilizotolewa hivi karibuni, zaidi ya Waislamu elfu sita wameuawa kuanzia tarehe 25 Agosti mwaka huu na wengine wanaokaribia elfu tisa kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya kinyama.

Saturday, September 23, 2017

23 September 2017, Raia 6, 000 wa Kongo wamekimbilia Zambia kutokana na kuhofia usalama wao nchini humo

Vikosi vya serikali ya DRC vimekuwa vikiwaua raia, hali iliyosababisha wananchi wengi kukimbilia kaskazini mwa Zambia.

Zambia inahofia kuzuka migogoro kwani ni zaidi ya wakimbizi 6,000 wameikimbia DRC ndani ya mwezi mmoja.

Kwa mujibu wa habari,wakimbizi waliofika Zambia wamehojiwa na kusema kuwa wanaikimbia DRC kutokana na mauaji yanayofanywa na vikosi vya serikali nchini humo.

Mwakilishi mkuu wa UNHCR Zambia amesema kuwa serikali ya nchi hiyo imekuwa ikiwatesa wananchi kwa kuwaua,kuwachomea manyumba yao,ubakaji na vilevile kuvamia maghala ya chakula.

Viongozi wa Afrika Kusini wana nia ya kumteua kiongozi mstaafu atakayeweza kusaidia kutatua migogoro nchini Congo.

23 September 2017,Mwanamke moja mkoani Shinyanga afikishwa rumande baada ya kumchinja mumewe

MKAZI wa Kata ya Tinde katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Zena Mohamedi (28) anashikiliwa na Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kumuua mumewe, Bakari Salehe (35) kwa kumchinja shingo kwa madai ya wivu wa kimapenzi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Simon Haule alisema tukio hilo limetokea juzi saa 2.30 usiku wakati mwanamke huyo akiwa na mume wake nyumbani kwao, simu ya mwanamume iliita ndipo akaichukua mkewe huyo na alipoipokea akasikia sauti ya mwanamke, na ndipo ugomvi na majibizano yalipoanzia.

Kamanda Haule alisema baada ya ugomvi huo kuzuka, ndipo mwanamke alipochukua kitu chenye ncha kali na kumchinja shingo mume wake na kusababisha kupoteza maisha, na mwili wake tayari umehifadhiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.

“Chanzo cha tukio hili ni wivu wa kimapenzi ambapo mwanamke mara baada ya kuita simu ya mumewe aliikimbilia kuipokea, na aliposikia sauti ya mwanamke mwingine kwa hisia zake akaona tayari ni hawara wa mume wake, ndipo wakaanza kupigana hadi kusababisha kifo,” alisema Haule.

Hata hivyo, Kamanda Haule alisema jeshi hilo linamshikilia mwanamke huyo kwa mahojiano zaidi na uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani kujibu shitaka la mauaji lililotokea na kutumia kitu chenye ncha kali. Aidha, kamanda alitoa mwito kwa wananchi kuacha tabia za ugomvi wakutumia vitu vyenye ncha kali.

23 September 2017, Wanafunzi 214 wa shule za msingi na sekondari wilayani Ukerewe mkoani Mwanza na Mara wapata mimba

WANAFUNZI 214 wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza na Rorya Mkoa wa Mara wamebainika kuwa na ujauzito katika kipindi cha Januari mwaka huu hadi sasa na hivyo kulazimika kukatisha masomo na kushindwa kutimiza ndoto zao.

Kati ya hao, Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza waliopata mimba ni 126 wakati Wilaya ya Rorya Mkoa wa Mara ni wanafunzi 88 waliokuwa wakisoma katika shule mbalimbali za msingi na sekondari.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ukerewe, Frank Bahati aliyasema hayo jana wilayani humo katika ziara iliyolenga kuangalia mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu, KKK pamoja na kuangalia hali ya uboreshaji wa miundombinu ya shule kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (P4R).

Bahati alisema wanafunzi waliopata ujauzito, 118 ni wa shule za sekondari na nane ni wa shule za msingi na tayari kesi zimefunguliwa mahakamani dhidi ya wahusika. Alisema kutokana na tatizo hilo wamekuwa wakibuni njia mbalimbali za kukabiliana na tatizo hilo ikiwemo kufanya operesheni na kuwakamata wahusika na kuwafikisha katika vyombo vya kisheria, lengo likiwa ni kuboresha elimu katika wilaya hiyo.

“Hizi mimba ni kiwango kikubwa ambacho kinatishia kwa mustakabali wa taaluma ya Wilaya yetu, hivyo tunatoa elimu ya afya kwa shule za msingi na sekondari...pia tuna utaratibu wa kuwapima ujauzito mara kwa mara,” alieleza.

Pia alisema wanafanya vikao vya mara kwa mara na kamati za shule, wazazi, walezi, waalimu na jamii inayozunguka shule na kuwaelimisha kuhusu malezi bora pamoja na kuwahamisha kutoa ushirikiano kwa kuwataja wanaowapa wanafunzi ujauzito.

“Kumekuwa na ukimya wa kutotaka kuwataja wanaowapa mimba wanafunzi na kupotosha ukweli kati ya muhusika, mzazi na mwanafunzi...hivyo bado tatizo ni kubwa na tumekuwa tukichukua hatua za ziada kushughulikia tatizo hili.

Sisi kama Halmashauri tumekusudia kuwalinda wanafunzi wetu,” alisema. Pia alisema zaidi ya Sh milioni 500 zilizotolewa na serikali kupitia Mradi wa P4R zimesaidia kuboresha miundombinu na kujenga mabweni katika shule za Sekondari Pius Msekwa na Bujingo zilizopo wilayani humo na hivyo husaidia kupunguza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu.

Aidha, alisema kupitia mpango wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) umesaidia kupunguza tatizo la wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi bila kujua KKK. Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Estomih Chang’ah alisema tatizo la mimba katika wilaya hiyo linasikitisha na kuhuzunisha na linachangiwa na malezi ya kifamilia kuwa dhaifu kutokana na shughuli za uvuvi.

“Maeneo yetu mengi ni visiwa, hivyo wananchi wanatoka umbali mrefu... kama tungekuwa na hosteli na mabweni ya kutosha tungepunguza tatizo hili. Pia tumefungua kesi zaidi ya 10 mahakamani dhidi ya wanaowapa mimba wanafunzi na zipo katika hatua mbalimbali,” alisema mkuu wa wilaya.

Akizungumza katika kikao cha madiwani wilayani Rorya, Diwani wa Viti Maalumu, Edna Charles alisoma taarifa ya idadi ya wanafunzi waliopata ujauzito katika kipindi cha mwaka mmoja, na kueleza kuwa katika robo ya kwanza wanafunzi 25 walipata mimba, ya pili wanafunzi 17, ya tatu wanafunzi 23 na katika robo ya nne wanafunzi 23 walipata mimba na kufanya idadi ya wanafunzi 88

Friday, September 22, 2017

23 September 2017, Waislamu wa Ulaya walalamika juu ya ubaguzi na miamala mibaya

Matokeo mapya ya uchunguzi wa Shirika la European Union Agency for Fundamental Rights (FRA) unaonyesha kwamba, idadi ya Waislamu ambao wanabaguliwa na kufanyiwa miamala mibaya katika jamii ya Ulaya, imeongezeka sana.

Hadi sasa Waislamu wa Ulaya wanahisi kubaguliwa na kutengwa kutokana na imani yao ya kidini.

Uchunguzi huo uliofanyika mwaka jana wa 2016 katika nchi 15 wanachama wa Umoja wa Ulaya kwa kuwahoji Waislamu 10500 waliohajiri kuingia nchi hizo, unaonyesha kwamba idadi ya Waislamu wanaoubaguliwa katika jamii hiyo ya EU imeongezeka sana.

Kizazi cha pili cha wahajiri barani Ulaya kinatajwa kuwa waathirika wakubwa zaidi kuliko kizazi cha kwanza.

Matokeo ya uchunguzi huo yanaonyesha kwamba, mbali na ubaguzi huo, karibu asilimia 27 ya Waislamu barani Ulaya wamekiri kufanyiwa ukatili na kuudhiwa.

Kuhusiana na suala hilo wanawake Waislamu hususan wanaovaa hijabu barani humo wanaonekana kulengwa moja kwa moja na mashambulizi ya kimwili na kuudhiwa pia.

Kwa mujibu wa Ismail Haghi Yaouwzjan, ambaye ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Tübingen nchini Ujerumani: "Makundi yenye misimamo mikali ya kufurutu ada katika nchi za Magharibi yanaamini kuwa, ongezeko la uhajiri wa Waislamu wanaokwenda barani Ulaya, linaweza kubadili muundo wa kale wa kijamii barani humo.

Ni kwa ajili hiyo ndio maana yanawaona wahajiri hao kuwa ni tishio la usalama na hivyo kuamua kukabiliana nao." Mwisho wa kunukuu. Ukweli ni kwamba kama yalivyoonyesha matokeo ya uchunguzi huo, chuki dhidi ya Uislamu na ubaguzi kuwalenga Waislamu, limebadilika na kuwa suala nyeti kwa Waislamu wanaoishi barani humo.

Licha ya kutolewa na baadhi ya viongozi wa Ulaya matamshi ya kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu na madai yao ya kuwalinda Waislamu wanaoishi nchi hizo, lakini kivitendo kumeendelea kushuhudiwa mashinikizo na ubaguzi mkubwa dhidi ya wafuasi wa dini hiyo katika nchi za Ulaya hususan Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.

Kuendelea mwenendo wa vitendo vya chuki na ubaguzi dhidi ya Waislamu, kumesababisha ongezeko la ukosoaji wa asasi za haki za binaadamu ikiwemo kamisheni ya kupambana na ubaguzi ya Umoja wa Mataifa ndani ya nchi hizo.

Aidha chuki dhidi ya Uislamu katika nchi kubwa za Ulaya sambamba na vitendo kama vile vya kuwabambikizia kesi, kuyavunjia heshima matukufu yao, kueneza propaganda chafu dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla na kadhalika kuwafanyia vitendo mbalimbali vya ubaguzi wa kijamii, kiuchumi na hata kuwafukuza katika maeneo ya kazi, ni miongoni mwa hujuma za kidini zinazowakabili Waislamu wa barani Ulaya.

Kadhalika kuzuiliwa kupewa ajira au kuwekewa masharti magumu, kukiwemo kuzuiliwa kujistiri kwa hijabu wanawake wa Kiislamu wanapokuwa kazini, ni sehemu nyingine ya vikwazo vinavyowakabili Waislamu hao. Katika hali hiyo, wimbi la wahajiri na hujuma ya maelfu ya wakimbizi kwenda barani Ulaya ambapo akthari yao ni Waislamu, limeenda sambamba na wimbi la chuki dhidi ya wahajiri, wageni na hatimaye chuki dhidi ya Uislamu, ambapo mbali na upinzani juu ya suala la uwepo wa Waislamu barani humo, kumeshuhudiwa ongezeko kubwa la mashinikizo dhidi ya Waislamu wanaoishi nchi hizo.

Propaganda za makundi ya mrengo wa kulia na yenye misimamo mikali ya chuki kama vile PEGIDA la nchini Ujerumani, chama cha Kitaifa cha nchini Ufaransa na chama cha Uhuru cha nchini Uingereza zimekuwa na taathira kubwa katika kupigilia msumari wa chuki na ubaguzi kuwalenga Waislamu.

Hivi sasa hakuna matumaini yoyote ya kupatikana mabadiliko juu ya hali hiyo, bali kujiri mashambulizi ya kigaidi katika baadhi ya nchi za Ulaya kumezidisha mashinikizo dhidi ya Waislamu.

Wakati huo huo, hatua za kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) huko barani Ulaya na kadhalika ongezeko la propaganda za vyombo vya habari vya Magharibi na baadhi ya viongozi wa mataifa hayo katika kuuhusisha Uislamu na ugaidi, yote hayo yamepalilia ongezeko la chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu na wafuasi wa dini hiyo.

Kama alivyosema, Piruz Izadi, mtaalamu wa masuala ya kisiasa, ugaidi umesababisha kukithiri chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya na matokeo yake ni kushtadi mashinikizo dhidi ya Waislamu wa nchi hizo.

23 September 2017,Waislamu wa Bahrain wazuiwa kuswali Swala ya Ijumaa kwa wiki ya 62

Askari usalama wa Bahrain jana Ijumaa wamezuia kufanyika Swala ya Ijumaa katika eneo la al Deraz katika mji mkuu wa nchi hiyo, Manama kwa wiki ya 62 mtawalia.

Duru za habari za Bahrain zimeripoti kuwa, wananchi wa Bahrain waliokuwa wamejiandaa kwa ajili ya Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Imam Sadiq (A.S) katika eneo la al Deraz wiki hii pia wameshindwa kutekeleza ibada hiyo na kulazimika kusali furada baada ya kuzuiwa na askari wa utawala wa Aal Khalifa.

Msikiti wa Imam Sadiq (A.S) uliopo katika eneo la al Deraz leo asubuhi ulizingirwa na wanajeshi wa utawala wa Aal Khalifa.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, utawala wa Bahrain umemfutia uraia Sheikh Issa Qassim mwanazuoni mashuhuri wa nchi hiyo tangu mwezi Juni mwaka jana na kisha ukalizingira eneo la al Deraz ambako kuna makazi ya msomi huyo mtajika.

Wananchi wa Bahrain wamekuwa wakiandamana kwa amani dhidi ya utawala wa Aal Khalifa tangu Februari 14 mwaka 2011 wakipigania uhuru, kukomeshwa ubaguzi na kurejeshwa uadilifu. Aidha wanataka serikali ichaguliwe kwa njia ya kidemokrasia.

Hata hivyo utawala wa kifalme wa Aal Khalifa umekuwa ukiwakandamiza kwa kushirikiana na wanajeshi wa Saudia na maajenti wa usalama wa Imarati.

22 September 2017, Andre Ward astaafu ndondi

Bingwa wa ndondi uzito wa kati duniani Andre Ward amestaafu mchezo huo ikiwa ni mapema tofauti na ilivyotarajiwa.

Ward mwenye miaka 33 ameshinda mataji matatu tofauti ya uzani wa kati ikiwa ni pamoja na WBA, IBF na WBO.

Katika taarifa yake amesema mwili wake haupo tiyari kupata magonjwa ya kutetemeka.

''Kama siwezi kuipa familia yangu,timu yangu na mashabiki yangu kile wanachokitaka, basi sipaswi kuendelea kupigana,''alisema.

Mapema wiki hii Ward alituma picha kwenye mitandao ya kijamii akionyesha baadhi ya mikanda yake aliyoinyakua siku za nyuma.

Mara ya mwisho alipigana mwezi June na kumtangwa Sergey Kovalev mjini Las Vegas.

22 September 2017,Agizo la Rais Magufuli la kujenga uzio kuzunguka machimbo ya madini ya tanzanite umeanza kutekelezwa

Siku moja baada ya agizo la Rais Dkt. JOHN MAGUFULI kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania - JWTZ kujenga uzio kuzunguka machimbo ya madini ya tanzanite eneo la Mererani, kikosi cha wataalamu wa Jeshi hilo kimeanza kukagua mipaka ya eneo hilo ili kuanza ujenzi.

Akizungumza mara baada ya kutembelea eneo hilo Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT Meja Jenerali Michael Isamuyo amewaomba wananchi katika maeneo yatakayopitiwa na ujenzi huo pamoja na wamiliki wa migodi kutoa ushirikiano.

Ukaguzi huo umefanyika angani na ardhini kuzunguka machimbo ya tanzanite yaliyopo Mererani mkoani Manyara.

Mara bada ya kutembelea eneo hilo, Meja Jenerali ISAMUYO amesema wataanza kazi hiyo mara moja kama walivyoagizwa na Amri Jeshi Mkuu Rais John Magufuli.

Zoezi hili limeungwa mkono na wachimbaji wa madini katika eneo hili wakielezea kuleta manufaa kwao na taifa.

22 September 2017,Mwanamke tajiri kuliko wanawake wote duniani afariki

Mwanamke tajiri kuliko wote duniani Liliane Bettencourt amefariki dunia akiwa na umri wa 94 .

Liliane Bettencour aliyekuwa mmiliki wa shirika la vipodozi la L'Oreal amefariki akiwa amelala nyumbani kwake.

Taarifa za kifo chake zimetolewa na mtoto wake wa kike Francoise Bettencourt.

Kwa mujibu wa habari,baba yake marehemu Eugène Schueller alianzisha kampuni hiyo mwaka 1990 ambayo baadae ilibadilishwa jina kuwa  L'Oreal na kuonyesha mafanikio makubwa.

Liliane Bettencourt alikuwa tajiri wa 14 duniani.

22 September 2017, Yafahamu mambo kumi aliyoyafafanua Zitto kuhusu kamati ya haki, maadili na Madaraka ya Bunge

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe jana amesisitiza msimamo wake kwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwa Bunge limekosa meno na limeingiliwa na mhimili wa Serikali, huku pia akiihusisha Serikali na shambulio la risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Hata hivyo, Msemaji wa Serikali Hassan Abbas amekanusha madai ya Zitto akimtaka kufuata kanuni za Bunge na kuheshimu sheria za nchi.

Zitto aliyekamatwa juzi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akitokea Kigoma, alikiri kutoa maoni kwenye mitandao ya kijamii akimkosoa Spika wa Bunge, Job Ndugai na Serikali na kusisitiza kuwa anatumia uhuru wake wa kikatiba kutoa maoni.

Awali, Zitto alimkosoa Spika baada ya ripoti ya kamati aliyoiunda kuchunguza biashara ya madini ya almasi na Tanzanite kwenda kusomewa Ikulu, Septemba 7, jambo lililosababisha aitwe kwenye kamati hiyo.

Hata hivyo, kabla hajaenda kwenye kamati hiyo, Zitto aliandika tena kwenye mtandao wa Twitter akimshutumu Spika Ndugai. Katika maelezo yake kwa kamati hiyo ya Bunge ambayo gazeti hili limeyaona, Zitto alikiri kuandika maoni yake katika mtandao wa Twitter yenye kichwa cha habari ‘Bunge siku hizi ni Idara ya Tawi la Utawala’ akisema Bunge la 11 limekuwa likifanya kazi kwa kuingiliwa na Serikali chini ya Rais John Magufuli.

“Maneno na vitendo vya Rais yanaashiria kuwa Bunge halina uhuru wake na mimi kama mbunge nina wajibu wa kuonyesha kutopendezwa kwangu,” alisema.

Mbunge huyo alitaja mambo 10 ambayo alisema yanathibitisha maelezo yake kuwa ni pamoja na kuzuiwa kuonyeshwa kwa vipindi vya Bunge moja kwa moja kupitia televisheni akisema ilikuwa ni kwa kisingizio cha kupunguza gharama za uendeshaji wa mhimili wa Bunge.

“Ni dalili ya wazi ya kufifisha sauti ya Bunge na kupandisha sauti ya Serikali. Hata vituo binafsi ambavyo vilipanga kurusha Bunge Live bila malipo vilizuiwa, lakini vinarusha live mikutano ya Rais,” alisema.

Pia, aliseka kitendo cha uongozi wa Bunge kurudisha serikalini Sh6 bilioni bila ridhaa ya wabunge kwa kisingizio kwamba zimebaki kutokana na kubana matumizi ni dalili ya “kujipendekeza” kwa Serikali na kuongeza kuwa; “Wakati Uongozi wa Bunge ukirejesha kiwango hicho cha fedha, kuna taarifa kwamba kamati nyingi za Bunge zinashindwa kutekeleza wajibu wake kwa sababu ya ukata.”.

Alitaja sababu ya tatu kuwa ni maelekezo ya Serikali kwa Bunge kupitia maagizo ya Rais Magufuli kwa Spika Ndugai aliyoitoa wakati akipokea Ripoti ya Profesa Osoro kuhusu mikataba ya madini Juni 12, 2017 aliposema awashughulikie wabunge aliowaita waropokaji.

Alisema kauli hiyo inaonyesha picha dhahiri kuwa Bunge linapokea maelekezo kutoka serikalini ya kuwadhibiti wabunge hasa wanaoiwajibisha Serikali.

Pia, alisema kitendo cha Bunge kuhariri hotuba za kambi ya upinzani kwa kushinikiza kuondolewa kwa vipengele vinavyoikosoa Serikali ni sababu mojawapo ya Bunge kukosa nguvu, huku akitoa mfano wa hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Godbless Lema iliyoamriwa kuondolewa maneno yanayohusu kashfa ya mkataba wa Lugumi, kumhusisha Rais na kuuzwa kwa nyumba za Serikali, mauaji ya wanasiasa pamoja na Bunge kulinda wahalifu.

“Kauli ya Rais Magufuli ya Novemba 4, 2016 akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuwa mzizi wa mhimili wa Serikali ni mrefu zaidi kuliko mihimili mingine, baada ya kuulizwa juu ya matumizi ya Serikali nje ya bajeti inaonyesha dhahiri fikra ya Rais na Serikali yake juu ya ukuu wa mhimili wa Serikali dhidi ya Bunge,” alisema Zitto.

Alitaja pia kitendo cha ripoti ya kamati za Tanzanite na Almasi kusomwa nje ya Bunge na kuwasilishwa kwa Waziri Mkuu na Rais bila kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni ili kuwekewa azimio la Bunge akisema kinazifanya kamati hizo kuonekana kuwa za Serikali badala ya Bunge.

“Kauli ya Rais kuwa Spika alimpigia simu kumuuliza juu wajumbe wa kuwaweka kwenye kamati ya Bunge ya Tanzanite na Almasi inaonyesha dhahiri kuwa Spika anafanya kazi kwa maelekezo ya Rais. Bunge na Spika hawajawahi kuikana kauli hii ya Rais,” alisisitiza.

Vilevile alikitaja kitendo cha Serikali kutowasilisha taarifa za utendaji wa robo mwaka kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya mwaka 2014 ni dharau kwa mhimili wa Bunge.

“Ni dharau zaidi kwamba Serikali ilileta muswada wa sheria kuondoa kifungu kinacholazimisha Waziri wa Fedha kutoa taarifa hizo na Bunge kupitisha kuwa Sheria, hivyo kuondoa kabisa uwajibikaji wa kibajeti wa Serikali ndani ya Bunge,” alisema.

Alisema licha ya Katiba kuonyesha mihimili mitatu ya dola ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama kufanya kazi bila kuingiliana kikatiba, mbali na wajibu wake wa kutunga sheria, Bunge ni kama kiranja wa Serikali.

“Haijapata kutokea katika historia ya Bunge letu, wabunge kukamatwa hovyo mbele ya mageti ya Bunge na kusafirishwa usiku usiku bila hata Spika kujulishwa kama taratibu za mabunge ya Jumuiya ya Madola zinavyotaka. Tukio linalolenga kuliziba mdomo Bunge,” aliongeza.

Shambulio la Lissu

Akiendelea kufafanua mambo hayo 10, Zitto aligusia suala Lissu kushambuliwa kwa risasi wakati mkutano wa Bunge ukiendelea Septemba 7 akisema ni mara ya kwanza kwa historia ya nchi.

“Kitendo cha ‘watu wasiojulikana’ kummiminia risasi zaidi ya 30 Mbunge wa Singida Mashariki, Ndugu Tundu Lissu akitokea bungeni tena kwenye makazi yake ambayo kwa mujibu wa sheria ni sehemu ya Bunge ni dharau ya hali ya juu kwa mhimili huu,” alisema.

Katika makala yake aliyoiandika kwa ajili ya kuwasilisha kwenye kamati hiyo ya Bunge yenye kichwa cha habari ‘Asiyehusisha jaribio la mauaji ya Lissu hana moyo; asiyeamini kwamba vyombo vya dola vinahusika hana kichwa’, Zitto amejenga dhana ya shambulio hilo akilihusisha na Serikali

Msemaji wa Serikali

Akizungumza kwa njia ya simu, Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas alikanusha madai ya mhimili wa Serikali kuingilia Bunge akimtaka Zitto kuchukua hatua kama sheria zimevunjwa.

“Serikali ina majukumu yake, inatoa bajeti kwa Bunge, huko ndiyo kuingilia Bunge? Bunge linatunga sheria ndiyo tuseme linaingilia mahakama? Mahakama inapotafsiri sheria inaingilia Bunge? Hii mihimili haiwezi kufanya kazi in isolation (kwa kutengana).”

Kuhusu Serikali kuhusika na shambulio la Lissu, Dk Abbas alimtaka Zitto kusubiri uchunguzi wa Serikali badala ya kujadili hisia.

22 September 2017,JAJI MKUU:Tunahitaji sheria ya makosa ya mtandaoni

Jaji Mkuu mpya wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma jana September 21, 2017 alikutana na Waandishi wa Habari kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa na kuapishwa kwake kuchukua nafasi hiyo aliyokua anaikaimu baada ya aliyekuwa Jaji Mkuu kustaafu.

Jaji Mkuu pamoja na mambo mengi aliyozungumza katika mkutano wake wa kwanza na Wanahabari, alizungumzia suala la Sheria ya makosa ya mtandao ambao wengi wamekuwa wakiipinga na kusema Tanzania haihitaji, lakini Jaji Mkuu amekuwa na mtazamo tofauti na hakubaliani nao

22 Sptember 2017,Jaji Mkuu nchini Kenya aapa kulinda na kutetea sheria ya nchi hio

Jaji Mkuu nchini Kenya ,David Maraga ameapa kuilinda na kuitetea sheria ya nchi hiyo hasa baada ya vitisho kutoka kwa wanasiasa.

Bwana Maranga ameyasema hayo katika mkutano mjini Nairobi na kuongezea kuwa yeye na majaji wengine hawatalazimika kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta wala upinzani wake.

Kwa mujibu wa habari,bwana Maranga ametoa tamko hilo baada ya ombi la kumuondoa jaji mkuu kupelekwa katika mahakama ya juu ya Kenya.

Jaji Mkuu huyo pia amesema kuwa upande wao upo tayari kukabiliana na chochote kuhakikisha wanailinda katiba ya nchi hiyo.

Nje ya mahakama kuu,wafuasi wa rais Kenyatta walikuwa wakiandamana wakitaka majaji wakuu wawili wa juu waondolewe katika wadhifa wao.

Polisi walilazimika kupiga mabomu ya machozi.

Thursday, September 21, 2017

21 September 2017,Tume ya uchaguzi nchini Kenya yaamuru uchaguzi mpya kufanyika tarehe 26 Oktoba

Tume ya uchaguzi nchini IEBC imetangaza tarehe 26 mwezi Otoba 2017 kama tarehe mpya ya uchaguzi wa marudio Kenya ikiwa ni siku tano tu kabla ya kukamilika kwa siku 60 zilizowekwa kikatiba kufanyika kwa uchaguzi huo.

Katika taarifa fupi ,mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini humo IEBC Wafula Chebukati ametangaza kuwa hatua hiyo imechukuliwa ili kuhakikisha kuwa tume hiyo imejiandaa vilivyo kuambatana na uamuzi wa mahakama ya juu uliotolewa siku ya Jumatano.

''Hakuna tashwishi yoyote kwamba uamuzi wa mahakama ya juu utaathiri maandalizi ya uchaguzi hususan katika idara ya teknolojia'', alisema Chebukati.

''Ili kuhakikisha kuwa tume imejiandaa vilivyo kusimamia uchaguzi unaoafikia viwango vilivyowekwa na mahakama ya juu, tungependa kuwaelezea raia na washikadau kwamba uchaguzi mpya wa urais sasa utafanyika siku ya Alhamisi mwezi Oktoba 2017 ', amesema Mwenyekiti, akiongezea kwamba IEBC itatoa maelezo zaidi siku ya Ijumaa kuhusu hali ya maandalizi.

Kulingana na Chebukati ,IEBC inaendelea kuangazia uamuzi uliotolewa na mahakama ya juu kwa lengo la kutaka kuelewa madhara yake kuhusu uchaguzi huo mpya.

Katika uamuzi huo, majaji wanne wa mahakama ya juu akiwemo jaji mkuu David Maraga, naibu jaji mkuu Philomena Mwilu, Jaji Smokin Wanjala na Isaac Lenaola waliamuru kwamba uchaguzi huo uliofanyika mnamo tarehe 8 mwezi Agosti haukufanyika kulingana na katiba na hivyobasi kuyafutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais.

Pia majaji hao walisema kuwa kulikuwa na makosa ya kutofuata sheria katika uchaguzi huo wa urais ambayo yaliathiri uadilifu wa uchaguzi huo na matokeo yake.

21 September 2017,Raia nane wa Ethiopia wakamatwa wakiwa hawana vibari wakielekea mkoani Mtwara

Idara ya uhamiaji nchini imewakamata wahamiaji wasio na vibali nane raia wa Ethiopia waliokuwa wakisafiri kwenye lori kwenda mkoani Mtwara.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Kamishna wa Utawala na Fedha wa Idara ya uhamiaji Edward Chogero amesema wahamiaji hao wamekamatwa jana usiku katika eneo la Kongowe.

Kamishna Chogero amesema wahamiaji hao wamekamatwa kutokana na taarifa zilizopatikana kutoka kwa raia wema.

Amesema maafisa uhamiaji pia wamewakamata watanzania wanne na gari dogo aina ya Toyotà Passo ambayo inadaiwa kutumiwa na watuhumiwa hao wanaohusishwa na mtandao wa usafirishaji wa wahamiaji wasio na vibali.

Kamishna Chogero amesema mali za watu watakaobainika kujihusisha na mtandao huo zitataifishwa.

Wahamiaji wasio na vibali wapatao 5,700 wamekatwa tangu mwezi Januari hadi Juni mwaka huu.