Friday, September 22, 2017

23 September 2017, Waislamu wa Ulaya walalamika juu ya ubaguzi na miamala mibaya

Matokeo mapya ya uchunguzi wa Shirika la European Union Agency for Fundamental Rights (FRA) unaonyesha kwamba, idadi ya Waislamu ambao wanabaguliwa na kufanyiwa miamala mibaya katika jamii ya Ulaya, imeongezeka sana.

Hadi sasa Waislamu wa Ulaya wanahisi kubaguliwa na kutengwa kutokana na imani yao ya kidini.

Uchunguzi huo uliofanyika mwaka jana wa 2016 katika nchi 15 wanachama wa Umoja wa Ulaya kwa kuwahoji Waislamu 10500 waliohajiri kuingia nchi hizo, unaonyesha kwamba idadi ya Waislamu wanaoubaguliwa katika jamii hiyo ya EU imeongezeka sana.

Kizazi cha pili cha wahajiri barani Ulaya kinatajwa kuwa waathirika wakubwa zaidi kuliko kizazi cha kwanza.

Matokeo ya uchunguzi huo yanaonyesha kwamba, mbali na ubaguzi huo, karibu asilimia 27 ya Waislamu barani Ulaya wamekiri kufanyiwa ukatili na kuudhiwa.

Kuhusiana na suala hilo wanawake Waislamu hususan wanaovaa hijabu barani humo wanaonekana kulengwa moja kwa moja na mashambulizi ya kimwili na kuudhiwa pia.

Kwa mujibu wa Ismail Haghi Yaouwzjan, ambaye ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Tübingen nchini Ujerumani: "Makundi yenye misimamo mikali ya kufurutu ada katika nchi za Magharibi yanaamini kuwa, ongezeko la uhajiri wa Waislamu wanaokwenda barani Ulaya, linaweza kubadili muundo wa kale wa kijamii barani humo.

Ni kwa ajili hiyo ndio maana yanawaona wahajiri hao kuwa ni tishio la usalama na hivyo kuamua kukabiliana nao." Mwisho wa kunukuu. Ukweli ni kwamba kama yalivyoonyesha matokeo ya uchunguzi huo, chuki dhidi ya Uislamu na ubaguzi kuwalenga Waislamu, limebadilika na kuwa suala nyeti kwa Waislamu wanaoishi barani humo.

Licha ya kutolewa na baadhi ya viongozi wa Ulaya matamshi ya kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu na madai yao ya kuwalinda Waislamu wanaoishi nchi hizo, lakini kivitendo kumeendelea kushuhudiwa mashinikizo na ubaguzi mkubwa dhidi ya wafuasi wa dini hiyo katika nchi za Ulaya hususan Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.

Kuendelea mwenendo wa vitendo vya chuki na ubaguzi dhidi ya Waislamu, kumesababisha ongezeko la ukosoaji wa asasi za haki za binaadamu ikiwemo kamisheni ya kupambana na ubaguzi ya Umoja wa Mataifa ndani ya nchi hizo.

Aidha chuki dhidi ya Uislamu katika nchi kubwa za Ulaya sambamba na vitendo kama vile vya kuwabambikizia kesi, kuyavunjia heshima matukufu yao, kueneza propaganda chafu dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla na kadhalika kuwafanyia vitendo mbalimbali vya ubaguzi wa kijamii, kiuchumi na hata kuwafukuza katika maeneo ya kazi, ni miongoni mwa hujuma za kidini zinazowakabili Waislamu wa barani Ulaya.

Kadhalika kuzuiliwa kupewa ajira au kuwekewa masharti magumu, kukiwemo kuzuiliwa kujistiri kwa hijabu wanawake wa Kiislamu wanapokuwa kazini, ni sehemu nyingine ya vikwazo vinavyowakabili Waislamu hao. Katika hali hiyo, wimbi la wahajiri na hujuma ya maelfu ya wakimbizi kwenda barani Ulaya ambapo akthari yao ni Waislamu, limeenda sambamba na wimbi la chuki dhidi ya wahajiri, wageni na hatimaye chuki dhidi ya Uislamu, ambapo mbali na upinzani juu ya suala la uwepo wa Waislamu barani humo, kumeshuhudiwa ongezeko kubwa la mashinikizo dhidi ya Waislamu wanaoishi nchi hizo.

Propaganda za makundi ya mrengo wa kulia na yenye misimamo mikali ya chuki kama vile PEGIDA la nchini Ujerumani, chama cha Kitaifa cha nchini Ufaransa na chama cha Uhuru cha nchini Uingereza zimekuwa na taathira kubwa katika kupigilia msumari wa chuki na ubaguzi kuwalenga Waislamu.

Hivi sasa hakuna matumaini yoyote ya kupatikana mabadiliko juu ya hali hiyo, bali kujiri mashambulizi ya kigaidi katika baadhi ya nchi za Ulaya kumezidisha mashinikizo dhidi ya Waislamu.

Wakati huo huo, hatua za kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) huko barani Ulaya na kadhalika ongezeko la propaganda za vyombo vya habari vya Magharibi na baadhi ya viongozi wa mataifa hayo katika kuuhusisha Uislamu na ugaidi, yote hayo yamepalilia ongezeko la chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu na wafuasi wa dini hiyo.

Kama alivyosema, Piruz Izadi, mtaalamu wa masuala ya kisiasa, ugaidi umesababisha kukithiri chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya na matokeo yake ni kushtadi mashinikizo dhidi ya Waislamu wa nchi hizo.

No comments: