Monday, January 29, 2018

29 January 2018,UVCCM Wilaya ya Kinondoni Yaliomba Jeshi la polisi kuchunguza juu ya kukamatwa kwa gari la Meya wa Jiji la Dar es salaam

UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), wilaya ya Kinondoni umeliomba Jeshi la Polisi kuchunguza na kutoa majibu ya haraka baada ya kulikamata gari la Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Issaya Mwita (Chadema) likiwa na dereva wake ofi si za CCM wilaya hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa UVCCM wilaya hiyo, Lilian Rwebangira alisema matukio kama hayo hayapaswi kufumbiwa macho na kuchukuliwa kwa wepesi kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kinondoni.

“Nataka kuwafahamisha wana Kinondoni matukio yanayofanywa na wenzetu upande wa pili ambao ni wapinzani wetu hasa Chadema katika kipindi hiki cha kampeni, Chadema wameshajiona wanaenda kushindwa katika uchaguzi utakaofanyika Februari 17,” alisema.

Alisema baada ya kuona wanashindwa wameamua kutumia mbinu mbadala za kuhujumu kampeni ili kutia hofu wananchi waanze kuogopa ili wasijitokeze kupiga kura kama ilivyofanyika katika Kata ya Bweni kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani.

Alisema juzi walimkamata mwanamke mmoja wa Chadema akiwa amevaa nguo za kiraia ofisi hizo za CCM akijifanya mwendawazimu lakini baada ya kumhoji vizuri na kumfuatilia hadi katika familia yake walibaini ni wa Chadema.

Pia alisema juzi limetokea tukio katika ofisi hizo za CCM ambapo saa 2:30 usiku walikamata gari la Meya wa jiji wa Dar es Salaam likiwa na vijana wawili waliovalia kofia za CCM na wametokea wilaya ya Kigamboni.

“Baada ya tukio hilo tulibahatika kumbana dereva na kutoa taarifa Polisi na walifika wakamkamata dereva na gari na kulipeleka kituo cha polisi Magomeni... natoa rai kwa vyombo vya dola hili jambo wasilichukulie kimasihara ni jambo nyeti, wasifumbie macho jambo hili na wachukue hatua haraka,” alisema.

“Tumeshapata taarifa nyingi kutoka Chadema wanapanga kufanya fujo na kutishia wananchi wasipige kura lakini sisi kama UVCCM tukiwa walinzi wa chama tunatoa angalizo kwa vijana wa Chadema wanaojipanga kufanya vurugu, hatutavumilia vitendo hivyo,” alisema Lilian.

Alisema walipombana dereva aliwaambia alikuja kupaki gari katika eneo hilo kwa kuwa ni eneo salama lakini baadaye akadai alikuja na Meya akampeleka kikao mtaa wa Hananasif.

“Dereva huyu baadaye alisema alikuja na vijana wawili ambao aliwataja kwa jina moja, Alex na God ambao walimwambia awapeleke ofisi za CCM na kwa maelezo yake alipowashusha hakujua wameelekea wapi,” alisema Lilian.

“Wale vijana baada ya kushuka kwenye gari waliomba kuingia maliwatoni na kwa kuwa walitambuliwa walielekezwa vyoo vya ndani na wakashtuka wakajua wametambuliwa wakatoka nje wakakimbia na dereva naye alitoka lakini alirudi,” Lilian aliwaambia waandishi wa habari.

Pia alisema walitahadharishwa kuhusu vijana hao kwamba ni watu wa fujo ambao wamekuwa wakifanya vurugu wilaya ya Temeke hasa kwenye misiba ya wanachama wa CCM, mikutano ya chama na sherehe za chama.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa kipolisi Kinondoni, Jumanne Muliro alithibitisha kushikiliwa kwa gari hilo la Meya kwa madai linachunguzwa lakini hakutoa ufafanuzi zaidi. Meya wa Dar es Salaam, Mwita alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo simu yake iliita bila majibu.



Admit Habarileo

No comments: