Tuesday, September 12, 2017

12 September 2017 , Mashambulizi ya tarehe 11 Septemba 2001 na matukio ya miaka16 baadaye...

Miaka 16 iliyopita katika siku kama hii ya leo yaani Septemba 11 mwaka 2001 Marekani ilikabiliwa na mashambulizi mawili ya kigaidi yaliyosababisha uharibifu mkubwa.

Ndege tatu za abiria zilizokuwa zimetekwa nyara ziligonga majengo mawili pacha ya Kituo cha Biashara ya Dunia mjini New York na jengo la Wizara ya Ulinzi, Pentagon, katika mji wa Washington. Mashambulizi hayo yaliua karibu watu elfu tatu.

Serikali ya wakati huo ya Marekani ililituhumu kundi la al Qaida kuwa ndilo lililotekeleza mashambulizi hayo na ikaamua kuishambulia Afghanistan ili kulipiza kisasi.

Miaka miwili baadaye, mashambulizi na uvamizi wa Afghanistan uliofanyika chini ya mwavuli wa kile kilichopewa jina la "mapambano dhidi ya ugaidi" yalipanuliwa zaidi na kuilenga nchini nyingine ya Waislamu yaani Iraq.

Sasa imepita miaka 16 tangu baada ya mashambulizi ya Septemba 11 yaliyoitikisa Marekani.

Ilipangwa kuwa, mashambulizi ya Marekani katika nchi mbalimbali baada ya Septemba 11 mwaka 2001 yangeng'oa mizizi ya ugaidi nchini humo na katika maeneo mengine ya dunia.

Hata hivyo tunapotupia jicho haraka mwenendo wa matukio ya kisiasa na kiusalama katika kipindi cha miaka 16 iliyopita inatubainikia kwamba, serikali ya Marekani imefeli na kushindwa kufikia malengo yake makuu katika kile kilichodaiwa ni mapambano dhidi ya ugaidi wa kimataifa.

Mica Zinco ambaye ni mtaalamu wa Baraza la Uhusiano wa Kigeni wa Marekani amehoji katika makala iliyochapishwa na gazeti la New York kwamba: Kwa nini kwa mujibu wa tangazo la Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani, idadi ya makundi ya kigaidi ya nje imeongeza kutoka 28 mwaka 2002 na kufikia 61 kwa sasa?

Katika kipindi cha miaka 16 iliyopita nchi kadhaa zimevamiwa na Marekani au zimeshambuliwa kwa ndege zisizo na rubani za Marekani. Inasemekana kuwa, vita na mashambulizi ya Marekani dhidi ya nchi za Iraq na Afghanistan vimewagharimu walipa kodi wa Marekani zaidi ya dola trilioni 6.

Katika vita na mashambulizi hayo zaidi ya watu milioni moja katika nchi za Afghanistan, Iraq, Yemen, Syria, Libya, Pakistan na Somalia wameuawa kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.

Askari zaidi ya 4500 wa Marekani pia waliuawa katika vita vya Iraq pekee, idadi ambayo imevunja rekodi ya askari wa nchi hiyo waliouawa katika vita vya Vietnam.

Sambamba na hayo serikali ya Marekani imevuka mipaka yote ya haki za kiraia kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kuanzisha operesheni kubwa zaidi ya ujasusi katika historia ya mwanadamu.

Hata hivyo takwimu rasmi zinaonesha kuwa, idadi ya wahanga wa mashambulizi ya kigaidi ya baada ya Septemba 11 mwaka 2001 imeongeza mara kadhaa kuliko ile ya kabla yake.

Mashambulizi ya kigaidi ambayo kabla ya Septemba 11 mwaka 2001 yalikuwa yakifanyika tu katika maeneo machache sana ya dunia hususan magharibi na kusini mwa Asia, sasa yamekuwa tatizo la dunia nzima na yanalenga nchi zote zikiwemo za Ulaya na kwengineno.

Inatupasa kusema kuwa, siasa za kindumakuwili za nchi za Magharibi hususan Marekani kuhusu suala la ugaidi na makundi ya kigaidi kama Daesh na al Qaida zimeeneza zaidi ugaidi duniani katika miaka ya baada ya tukio la Septemba 11 na sasa dunia imegeuka na kuwa eneo hatari zaidi kwa maisha ya wanadamu.

No comments: