Kwa siku ya pili mfululizo, Wabunge wa Uganda wamerushiana makonde Bungeni wakati wa kujadiliwa muswada wa sheria inayotaka kuondoa kikomo cha umri wa kugombea urais nchini humo.
Kadhalika Spika wa Bunge Rebecca Kadaga ameagiza kutolewa kwa nguvu nje ya majengo ya Bunge Waziri mmoja na Wabunge 25 wanaodaiwa kuzusha vurumai hapo jana, aghalabu yao wakiwa wa upinzani.
Hapo jana wabunge wa chama tawala NRM na wale wa upinzani waliligeuza Bunge kuwa uwanja wa masumbwi na kutwangana makonde huku wengine wakirushiana viti.
Haya yanaarifiwa huku Kamisheni ya Mawasiliano ya nchi hiyo (UCC) ikisimamisha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge.
Godfrey Mutabazi, Mkurugenzi Mkuu wa UCC amesema idhaa au runginga yoyote itayopeperusha matangazo ya Bunge mubashara itajiweka katika hatari ya kupokonywa leseni, chini ya ibara ya 41 ya Sheria ya Kamisheni hiyo ya mwaka 2013.
Museveni mwenye umri wa miaka 73, ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miongo mitatu, kisheria hafai kuwania tena urais katika uchaguzi mkuu wa 2021 kwa sababu katiba ya Uganda imeainisha miaka 75 kuwa kikomo cha umri wa mtu anayetaka kugombea urais.
No comments:
Post a Comment