Friday, September 22, 2017

23 September 2017,Waislamu wa Bahrain wazuiwa kuswali Swala ya Ijumaa kwa wiki ya 62

Askari usalama wa Bahrain jana Ijumaa wamezuia kufanyika Swala ya Ijumaa katika eneo la al Deraz katika mji mkuu wa nchi hiyo, Manama kwa wiki ya 62 mtawalia.

Duru za habari za Bahrain zimeripoti kuwa, wananchi wa Bahrain waliokuwa wamejiandaa kwa ajili ya Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Imam Sadiq (A.S) katika eneo la al Deraz wiki hii pia wameshindwa kutekeleza ibada hiyo na kulazimika kusali furada baada ya kuzuiwa na askari wa utawala wa Aal Khalifa.

Msikiti wa Imam Sadiq (A.S) uliopo katika eneo la al Deraz leo asubuhi ulizingirwa na wanajeshi wa utawala wa Aal Khalifa.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, utawala wa Bahrain umemfutia uraia Sheikh Issa Qassim mwanazuoni mashuhuri wa nchi hiyo tangu mwezi Juni mwaka jana na kisha ukalizingira eneo la al Deraz ambako kuna makazi ya msomi huyo mtajika.

Wananchi wa Bahrain wamekuwa wakiandamana kwa amani dhidi ya utawala wa Aal Khalifa tangu Februari 14 mwaka 2011 wakipigania uhuru, kukomeshwa ubaguzi na kurejeshwa uadilifu. Aidha wanataka serikali ichaguliwe kwa njia ya kidemokrasia.

Hata hivyo utawala wa kifalme wa Aal Khalifa umekuwa ukiwakandamiza kwa kushirikiana na wanajeshi wa Saudia na maajenti wa usalama wa Imarati.

No comments: