Thursday, September 28, 2017

28 September 2017, Wakimbizi laki moja wa Nigeria watimuliwa Cameroon

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limekosoa vikali hatua ya Cameroon kuwafukuza nchini wakimbizi zaidi ya laki moja raia wa Nigeria.

Gerry Simpson, Mkurugenzi Mkuu wa masuala ya wakimbizi wa shirika hilo amesema mbali na jeshi la Cameroon kuwatimua wakimbizi na raia wanaotafuta hifadhi wa Nigeria kutoka nchini humo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, pia limewatesa na kuwakandamiza wengine wengi miongoni mwao.

Amesema kitendo hicho cha kuwarejesha wakimbizi hao nyumbani ambako walikimbia mauaji na mateso ya kundi la kigaidi la Boko Haram huenda kikasababisha moja ya migogoro mikubwa kabisa ya kibinadamu duniani.

Waziri wa Mawasiliano wa Cameroon amekataa kuongea na waandishi wa habari kuhusu kadhia hiyo ya kutimuliwa wakimbizi wa Nigeria.

Haya yanajiri katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa hivi karibuni ulionya kwamba karibu watu milioni 8.5 katika maeneo yaliyoathiriwa na mashambulizi ya Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa Nigeria wanahitaji misaada ya kibinadamu.

Shirika la Kushughulikia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema nalo limewahi kurekodi visa vya kutimuliwa na kukandamizwa wakimbizi wa Nigeria walioko katika nchi jirani ya Cameroon.

No comments: