Ndege ya usafirishaji inayomilikiwa na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeanguka leo karibu na mji mkuu Kinshasa na kuuwa makumi ya watu. Hayo yameelezwa na duru za kijeshi nchini humo.
Ndege hiyo ya usafirishaji aina ya Antonov ilipata ajali mara baada ya kuruka na ilikuwa imebeba makumi ya watu. Ndege hiyo imeanguka katika eneo la Nsele umbali wa kilomita 100 mashariki mwa Kinshasa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Afisa mmoja wa eneo hilo amesema kuwa hakuna mtu aliyenusurika katika ajali hiyo. Jeshi la Congo limetangaza kuwa ndege hiyo iliyokuwa na rubani raia wa Russia, ilikuwa imebeba magari mawili, silaha na wanajeshi. Limesema ndege hiyo ilikuwa na watu kati ya 20 na 30 wakati ilipoondoka katika uwanja wa ndege wa Ndolo mjini Kinshasa.
Mtu mmoja aliyeshuhudia ndege hiyo ikipata ajali amesema ilikuwa majira ya asubuhi kwa wakati wa Kongo alipoiona ndege ikianguka lakini hakukuwa na moshi kutoka kwenye ndege hiyo.
Wakala wa Shirika la Usafiri wa Anga la Kongo amesema kuwa ndege hiyo ilishindwa kuruka inavyotakikana katika uwanja wa ndege wa Ndolo na imeanguka katika eneo jirani la Nsele.
No comments:
Post a Comment