Thursday, September 21, 2017

21 September 2017,Tume ya uchaguzi nchini Kenya yaamuru uchaguzi mpya kufanyika tarehe 26 Oktoba

Tume ya uchaguzi nchini IEBC imetangaza tarehe 26 mwezi Otoba 2017 kama tarehe mpya ya uchaguzi wa marudio Kenya ikiwa ni siku tano tu kabla ya kukamilika kwa siku 60 zilizowekwa kikatiba kufanyika kwa uchaguzi huo.

Katika taarifa fupi ,mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini humo IEBC Wafula Chebukati ametangaza kuwa hatua hiyo imechukuliwa ili kuhakikisha kuwa tume hiyo imejiandaa vilivyo kuambatana na uamuzi wa mahakama ya juu uliotolewa siku ya Jumatano.

''Hakuna tashwishi yoyote kwamba uamuzi wa mahakama ya juu utaathiri maandalizi ya uchaguzi hususan katika idara ya teknolojia'', alisema Chebukati.

''Ili kuhakikisha kuwa tume imejiandaa vilivyo kusimamia uchaguzi unaoafikia viwango vilivyowekwa na mahakama ya juu, tungependa kuwaelezea raia na washikadau kwamba uchaguzi mpya wa urais sasa utafanyika siku ya Alhamisi mwezi Oktoba 2017 ', amesema Mwenyekiti, akiongezea kwamba IEBC itatoa maelezo zaidi siku ya Ijumaa kuhusu hali ya maandalizi.

Kulingana na Chebukati ,IEBC inaendelea kuangazia uamuzi uliotolewa na mahakama ya juu kwa lengo la kutaka kuelewa madhara yake kuhusu uchaguzi huo mpya.

Katika uamuzi huo, majaji wanne wa mahakama ya juu akiwemo jaji mkuu David Maraga, naibu jaji mkuu Philomena Mwilu, Jaji Smokin Wanjala na Isaac Lenaola waliamuru kwamba uchaguzi huo uliofanyika mnamo tarehe 8 mwezi Agosti haukufanyika kulingana na katiba na hivyobasi kuyafutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais.

Pia majaji hao walisema kuwa kulikuwa na makosa ya kutofuata sheria katika uchaguzi huo wa urais ambayo yaliathiri uadilifu wa uchaguzi huo na matokeo yake.

No comments: