Thursday, September 28, 2017

28 September 2017,SIMBA:Tutaichakaza Yanga bila kujali uwanja tutaochezea

MABOSI wa Simba wamecheka sana baada ya kuusikia mpango ya Yanga wa kutaka kulihamishia pambano lao la watani litakalopigwa Oktoba 28, kuja kuchezwa jijini Mwanza, kisha wakaamua kuwajibu kuwa si CCM Kirumba tu, hata kama wanataka kwenda nje ya nchi wao freshi tu.

Mabosi hao wa Wekundu wa Msimbazi, wamesema wapo tayari kucheza na Yanga popote wanapotaka, lakini wajue wazi kuwa kipigo chao katika mchezo huo kipo palepale.

Simba na Yanga zinatarajiwa kucheza mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu Oktoba 28 ambapo Yanga watakuwa wenyeji na juzi kati walifichua kuwa wana mpango wa kuhamishia pambano hilo Kirumba, Mwanza.

Hii ni kutokana na Uwanja wa Taifa kuwa katika matengenezo na Uwanja wa Uhuru uliokuwa umepangwa awali utumike kwa mechi hiyo, kutowaridhisha na hasa suala zima la kukusanya mapato.

Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten, alisema wako katika mchakato wa kuiomba Bodi ya Ligi kuhamisha mchezo huo akidai Uhuru ni mdogo kulinganisha na mechi yenyewe ilivyo kubwa.

Lakini mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Said Tulliy, amesema wao kama Simba wako tayari mchezo huo kufanyika uwanja wowote hapa nchini kwa sababu wanaamini Yanga haiwezi kutoka salama mbele yao.

“Si Kirumba tu, hata kama Yanga watataka tukacheze nao nje ya nchi ni freshi tu kwa sababu sisi hatuna wasiwasi nao kwa kikosi tulichonacho na namna msimu huu tulivyojiandaa kuwatia adabu,” alisema Tulliy.

Tulliy alisema Simba ina mashabiki kila kona ya Tanzania hivyo hawana wasiwasi wowote.

“Tuko tayari kucheza uwanja wowote ule hivyo Yanga wakitaka tucheze Kirumba sawa kwani Simba tuna mashabiki wengi sana kila mkoa, tunao hata nje ya nchi, hivyo watani zetu wasitapetape, tutawafuata popote,” alisema Tulliy.

Tulliy aliyasema hayo kwenye mkutano na wanahabari uliofanyika jana Jumatano jijini hapa ambao ulizungumza pia ishu nzima ya Kocha Joseph Omog, Simba wakisisitiza kuwa bado yupo sana Msimbazi tofauti na habari zinazovumishwa kuwa yupo mbioni kutimuliwa kazi.

Katika kuonyesha kuwa mechi hiyo ya watani haitapigwa jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amenukuliwa akisisitiza kuwa mchezo huo hautaweza kuchezwa Uwanja wa Taifa kwa vile uwanja huo unaendelea kukarabatiwa na utakamilika baada ya miezi mitatu.

Waipigia hesabu Stand

Katika hatua nyingine Simba imeanza kuzipigia hesabu pointi tatu za Stand United watakaocheza nao Jumapili hii kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Mratibu wa Simba, Abbas Ally, alisema wachezaji wote wapo fiti kuelekea mchezo huo, huku Shiza Kichuya akirejea kikosini baada ya kuumia katika mchezo uliopita dhidi ya Mbao FC.

Naye Msemaji wa Simba, Haji Manara, alisema timu hiyo inatarajiwa kuondoka kesho (Ijumaa) kuelekea Shinyanga kwa ajili ya mpambano huo.

“Tunakwenda Shinyanga kwa lengo la kupata pointi tatu muhimu tunajua tuko ugenini lakini tutapambana kuhakikisha tunapata ushindi,” alisema Manara.

No comments: