Sunday, December 31, 2017

31 December 2017, Amuua mkewe kwa kumchoma kisu sababu ya wivu wa mapenzi mkoani Tabora

Mkazi wa barabara ya Sikonge mkoani Tabora, Kapezi Fundikira (28) ameuawa kwa kuchomwa kisu na mume wake kutokana na wivu wa mapenzi.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Tabora, Wilbroad Mutafungwa alisema tukio hilo ni la Desemba 26, mwaka huu asubuhi katika eneo la barabara ya Sikonge.

Kwamba chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi.

Alimtaja mume wa Kapezi kuwa ni Issa Hamisi na kwamba baada ya kutenda mauaji hayo, alikimbia na juhudi za jeshi la polisi za kumtafuta zinaendelea.

Alisema polisi inaendelea kufanya doria usiku na mchana katika maeneo yote katika manispaa ya Tabora ili kuuweka mji vizuri na kudhibiti matukio ya mauaji na wizi usiku.

Mutafungwa alisema polisi mkoani Tabora inawaomba wananchi kutoa ushirikiano ili mtuhumiwa akamatwe na afikishwe mahakamani.

Wakati huo huo kijana mmoja, Michael Peter (20), mkazi wa Kata ya Chem Chem amegundulika amekufa akiwa ndani ya kilabu cha pombe za kienyeji.

Kamanda Mutafungwa alisema tukio hilo ni la Desemba 26, mwaka huu, majira ya saa 11 jioni maeneo ya mtaa wa Masempele Kata ya Ngambo, Manispaa ya Tabora.

Alisema Peter alikunywa pombe za kienyeji kupita kiasi na kusababisha kifo chake. Kwamba mwili wake baada ya uchunguzi, ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi

31 December 2017,Nape aiponda hama hama ya wanasiasa

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amehoji sababu za vyama vya siasa kuhangaika kupokea wanachama wa vyama vingine, badala ya kushughulika na Watanzania wasio na vyama.

Akizungumza leo Jumapili Desemba 31,2017 katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Azam, Nape amesema siku zote amekuwa na msimamo tofauti na wanachama wanaovihama vyama vyao kwa maelezo kuwa unawajenga wanaohama, si vyama.

"Kama tunataka kujenga vyama viwe vya kitaasisi ni lazima kuhamahama lisiwe suala la kawaida. Yaani mtu mpaka anahama watu waseme kweli huyu alistahili kuhama," amesema Nape.

Amesema, "Watanzania wapo zaidi ya 50 milioni, wenye uwezo wa kujiunga na vyama kikatiba wanaweza kuwa zaidi ya 30 milioni, waliopo kwenye vyama wanaweza wasifike 10 milioni. Kwa nini tunakwenda kuhangaika na wanachama wa vyama vingine badala ya kushughulika na Watanzania wasio na vyama.

Tushughulike kuwashawishi hawa."
Katika kipindi hicho, mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro na mwanahabari mkongwe, Dk Gideon Shoo waliungana na Nape kukosoa vitendo vya wanachama kuvihama vyama vyao.

Kwa mtazamo wao, hamahama ya wanasiasa ni miongoni mwa kasoro zilizojitokeza mwaka 2017.

31 December 2017,Askari polisi anyongwa kwa kipande cha chandarua hadi kufariki Jijini Mwanza

Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Kituo cha Nansio wilayani Ukerewe, John Kalongola amejinyonga kwa kipande cha chandarua nyumbani kwake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amesema mwili wa askari huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe.

Amesema baada ya uchunguzi na utaratibu kukamilika mwili utasafirishwa kwa mazishi mkoani Iringa.

Kamanda Msangi amesema mwili huo ulibainika baada ya harufu kutoka ndani ya nyumba yake na mlango ulipovunjwa ulikutwa ukining’inia.

Mwili wa askari huyo uligunduliwa jana Ijumaa Desemba 29,2017. Amesema kipande cha chandarua kilifungwa juu ya dari.

Saturday, December 30, 2017

30 December 2017,Rais ahukumiwa miaka mitatu jela baada ya kujivunjia heshima

Rais aliyeuzuliwa madarakani wa Misri, Muhammad Mursi amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa tuhuma za kuvivunjia heshima vyombo vya mahakama vya nchi hiyo.

Hukumu hiyo imetolewa leo dhidi ya Mursi ambaye hadi sasa anaendelea kuzuiliwa katika jela za nchi hiyo huku akiwa tayari amekwisha hukumiwa mara kadhaa kikiwemo kifungo cha maisha.

Mbali na Muhammad Mursi, mahakama ya Misri pia imewahukumu watu 18 wengine kwa tuhuma hiyohiyo ya kuvivunjia heshima vyombo vya mahakama. Adha mahakama ya Misri imemtaka Mursi kulipa faini ya Pauni milioni moja za Misri kwa jaji Muhammad al-Nemr.

Hivi karibuni mahakama ya Misri ilitoa pendekezo kwa asasi za juu za kisheria la kutaka kufutwa uraia wa Mursi, waziri mkuu na waziri wa mambo ya ndani wa rais huyo wa zamani wa Misri.

Tangu alipoondolewa madarakani rais huyo mwaka 2013, hadi sasa mamia ya wafuasi wake wamehukumiwa vifungo vya maisha au kunyongwa.

Aidha tangu alipoondolewa madarakani rais huyo, Misri imekuwa ikikumbwa na wimbi la mashambulizi ya makundi ya kigaidi.

30 December 2017,TCRA yashusha gharama za upigaji simu

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), yashusha gharama za kupiga simu kutoka shilingi 26.96 kwa dakika moja hadi shilingi 15.60 kuanzia 2018.

Mkurugenzi wa TCRA James Kaliba amesema kuwa gharama hizo zitaendelea kupungua kadiri miaka inavyozidi kwenda kama ambavyo imeanishwa hapa.

Gharama za mwingiliano zitakazotozwa kwa dakika na mwaka kwenye mabano ni Sh15.60 (Januari Mosi, 2018), Sh10.40 (2019), Sh5.20 (2020), Sh2.60 (2021) na Sh2.00 (2022).

Viwango hivyo vimepungua kulinganisha na miaka mitano iliyopita ambayo gharama zake za mwingiliano zilizokuwa zikitozwa kwa dakika na mwaka wake kwenye mabano ilikuwa Sh34.92 (2013), Sh32.40 (2014), 30.58 (2015), Sh28.57 (2016) na Sh26.96 (2017).

Hata hivyo amesema kuwa kampuni za simu zimekuwa na kigugumizi kukubaliana na viwango hivyo na kuingia mikataba ya mwingiliano kwa sababu ya masilahi ya kibiashara hivyo TCRA ililazimika kuingilia kati na kuvipangia kwa kufuata utaratibu kama ilivyoainishwa katika sheria namba 12 ya kuanzishwa kwake mwaka 2003.

“Kupungua kwa gharama hizi kutawezesha na kuongeza ufanisi katika shughuli za sekta zingine kiuchumi na kijamii, pia kutaongeza mapato ya watoa huduma na Serikali kutokana na ongezeko la matumizi ya huduma za mawasiliano,” alisema.

Alisema kwa sasa simu za mezani ni 127,976 na watumiaji wa simu za kiganjani imeongezeka kutoka laini 2,963,737 mwaka 2005 hadi kufikia laini 40,002,364, Septemba na mpaka kufikia Septemba, mwaka huu watumiaji wa huduma wamefikia 21,611,855

30 December 2017,Jeshi la polisi nchini latoa takwimu ya watoto Waliopotea 2017

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema matukio ya watoto kupotea yameongezeka kutoka watoto 17 mwaka jana, hadi watoto 22 mwaka huu, ambayo ni sawa na asilimia 29.4.

Amesema takwimu hizo ni kuanzia Januari hadi Desemba, huku akibainisha watoto hao huibiwa na wanawake ambao hawajabahatika kupata watoto.

Mambosasa alitoa kauli hiyo jana katika mkutano na waandishi wa habari wakati akieleza matukio ya uhalifu, watoto kutupwa, jinai na dawa za kulevya yaliyotokea mwaka huu akilinganisha na mwaka jana.
Akifafanua kuhusu watoto kupotea, alisema huibiwa hospitali, majumbani na katika shule wanazosoma.

Pia, alisema watoto waliotupwa wameongezeka na kufikia 21 sawa na asilimia 31.25 katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka huu, ikilinganishwa na mwaka 2016 ambako walikuwa 16.

“Matukio ya kikatili dhidi ya watoto yameongezeka ikiwamo baadhi ya wazazi kuwatupa katika majalala na vyoo,” alisema Mambosasa.
Kuhusu matukio ya uhalifu alisema yalikuwa 126,200 ukilinganisha na kipindi cha mwaka 2016 yalikuwa 129,602 takwimu alizosema kuwa zimepungua kwa asilimia 2.6.

Alisema matukio ya jinai yalikuwa 9,736 ikilinganisha na mwaka 2016 yalikuwa 12,550, ikiwa ni pungufu kwa matukio 2,814 sawa na asilimia 22.4.

“Jeshi linaimarisha doria na misako, wahalifu 18,194 walikamatwa kwa tuhuma mbalimbali kuanzia Januari hadi Desemba 2017.

“Bangi zenye uzito wa zaidi ya kilogramu 2,455 zilikamatwa na watuhumiwa walikuwa 5,205; hatua za kisheria zimechukuliwa,” alisema.
Alisema kilogramu 1.444 za dawa za kulevya aina ya cocaine zilikamatwa, heroine kilogramu 2.234 huku jumla ya watuhumiwa 352 wakikamatwa, “kesi zilizofunguliwa zilikuwa 201.

Mirungi ilikamatwa kilogramu 96.702, jumla ya watuhumiwa waliokamatwa wakijihusisha na mirungi hiyo ni 184, na kesi 57 zilifunguliwa.”

Alisema Polisi imejipanga kupunguza uhalifu mwaka 2018, ikiwa ni pamoja na kuelimisha wafanyabiashara wakubwa kuweka kamera za CCTV katika maeneo ya biashara zao ili kusaidia ulinzi.



Admit Mwananchi

Friday, December 29, 2017

29 December 2017,Askari sita wa Jeshi la Misri wauawa kwa kushambuliwa na bomu kaskazini mwa nchi hio, (SINAI)

Wanajeshi sita wa Misri wameuawa katika shambulizi la bomu lililotokea jana Alkhamisi katika eneo linalokumbwa na misukosuko la Rasi ya Sinai, kaskazini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, bomu la kutegwa ardhini liliripuka baada ya kukanywagwa na gari la jeshi lililokuwa likilinda doria katika mji wa Bir al-Abd, kaskazini mwa eneo la Sinai.

Msemaji wa Jeshi la Misri katika eneo hilo, Kanali Tamer el-Rifaai amethibitisha kutokea tukio hilo na kusisitiza kuwa, afisa mmoja wa ngazi za juu na wanajeshi watano ndio waliouawa katika hujuma hiyo, baada ya kuenea habari kuwa ni makamanda wawili wameuawa.

Haya yanajiri siku chache baada ya vyombo vya sheria nchini humo kuwanyonga watu 15 waliopatikana na hatia ya kufanya mashambulizi ya kigaidi yaliyoua askari usalama huko kaskazini mwa Peninsula ya Sinai.

Wapiganaji wa makundi ya kigaidi na kiwahabi wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika eneo la Sinai nchini Misri dhidi ya askari usalama, polisi na vituo vya ibada kama misikiti na makanisa.

Shambulizi la hivi karibuni zaidi la matakfiri hao ni lile lililofanyika mwezi uliopita katika Msikiti wa al-Rawdhah ulioko katika mji wa Bir al-Abd, yapata kilomita 40 kutoka mji wa Arish, makao makuu ya mkoa wa Sinai Kaskazini.

Zaidi ya Waislamu 300 waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala waliuawa katika shambulizi hilo.

29 December 2017,Lissu aja na hili lakusisimua

Zikiwa zimepita Siku kadha tangu Lissu asimame  Tundu Lissu ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema),  ametoa waraka akilaani ukiukwaji wa haki za binadamu na kuminywa kwa uhuru wa kutoa mawazo.

Waraka huo alioutoa jana Alhamisi Desemba 28,2017 akiwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya anakopatiwa matibabu tangu Septemba 7,2017 aliposhambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi kwenye makazi yake Area D mjini Dodoma.

Lissu pia amezungumzia tukio la kutoweka mwandishi wa habari wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Azory Gwanda ambaye leo ni siku ya 39 tangu alipotoweka akiwa wilayani Kibiti mkoani Pwani anakofanyia kazi zake.

“Watanzania ambao wamekuwa wakitumia uhuru wao wa maoni kutoa mawazo wamekuwa wakikamatwa na kushtakiwa mahakamani... mwanachama wa Chadema, Ben Saanane na mwandishi wa Mwananchi (Azory Gwanda) wametoweka na hawajulikani walipo. Hakuna uchunguzi au taarifa za kutoweka kwao,” amesema.

Lissu ambaye pia ni mwanasheria wa Chadema amesema vyombo vya habari vimekuwa katika wakati mgumu baada ya kukutana na mkono wa sheria, ikiwamo kufungiwa pale vinapoandika habari zinazotafsiriwa kuwa ni za kichochezi au uongo.

Kupitia waraka huo alioupa jina ‘Barua kutoka kitanda cha Hospitali ya Nairobi’ amezungumzia pia mambo yaliyojitokeza na yanayoendelea katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Waraka huo ameutoa siku tatu baada ya kusimama kwa mara ya kwanza tangu Septemba 7,2017 aliposhambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi.

29 December 2017,Rais Magufuli awapa onyo hili watumishi wa Umma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli tayari amewasilisha fomu yake ya tamko kuhusu rasilimali na madeni katika ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliyopo Mtaa wa Ohio, Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam.

Magufuli ametoa tamko hilo na kuwataka viongozi wa umma kuhakiki rasilimali na madeni yao kwa mujibu wa kifungu cha 9 na cha 11 cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995.

Ambapo Jaji Nsekela amewaambia viongozi kuwa kufanya hivyo sio ombi bali ni kufuata katiba na sheria inazoziongoza nchi.

“Viongozi hawaombwi kujaza fomu hizi, kuna baadhi wanadhani labda kutuletea hilo tamko ni fadhila, hapana, sheria ya nchi inahitaji hivyo na kuna sababu zake za msingi” amesema Mhe. Jaji Mstaafu Nsekela.

Magufuli amemtaka Jaji Nsekela mwisho wa kupokea fomu hizo ni tarehe 31 Disemba, 2017 kutopokea fomu ya kiongozi yeyote ambaye atakuwa hajawasilisha mpaka tarehe hiyo.

“Mhe. Jaji Nsekela ikifika tarehe 31 Desemba, ambayo ni siku ya mwisho kwa Mujibu wa Sheria, weka mstari na usipokee fomu zingine, halafu tuone sheria itafanyaje, nakutakia kazi njema” amesisistiza Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Jaji Mstaafu Nsekela amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kuwasilisha taarifa ya akaunti yake ya benki sambamba na tamko hilo, na amekiri kuwa ameonesha mfano wa kuigwa na viongozi wengine

Thursday, December 28, 2017

28 December 2017,Yatajwa siku Lissu atayorejea nchini

Siku moja baada ya mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kusimama kwa mara ya kwanza tangu Septemba 7, amesema huenda akakaa hospitalini kwa miezi sita zaidi.

Juzi, Lissu anayepata matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alisimama kwa msaada wa madaktari.

Akijibu swali ni lini atarejea nchini na kama atasafiri nje ya Afrika kwa matibabu zaidi aliloulizwa jana na mwandishi wetu, Lissu alisema, “Ndio kwanza nimesimama jana (juzi), kuna miezi sita ya ‘rehabilitation’ (kumrudisha katika hali ya kawaida).

Madaktari waliniambia kuna miezi sita au tisa.”

“Kwanza nimesimama kwa mara ya kwanza uamuzi wa je, nitamalizia hapa au nitakwenda bado, itategemea ushauri wa madaktari na kisha majadiliano na familia kwa sasa bado sijajua.”

Tangu mwanasheria huyo mkuu wa Chadema aliposhambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi akiwa katika makazi yake Area D mjini Dodoma Septemba 7, hakuwahi kusimama na wakati wote alikuwa akionekana amelala au amekaa hadi juzi.

Katika picha iliyomwonyesha Lissu akiwa amesimama, madaktari wawili walimshika huku mmoja akiurekebisha mguu wake wa kulia.

Lissu alituma ujumbe kwa wapigakura wa Singida Kaskazini akisema; “Wajiandae kwa mapambano makubwa ya kisiasa… kila mmoja atimize wajibu wake na kuacha visingizio.”

Akizungumzia hatua ya Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) kusimama, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema, “Ni jambo la kumshukuru Mungu, tulikuwa tunapigania mwenzetu asimame, tunamshukuru Mungu kwa hatua hii.

“Itachukua muda kidogo ili aweze kurejea katika hali yake, lakini tumshukuru sana Mungu kwa kutupa Lissu, lakini tuwashukuru sana madaktari waliomuuguza na hili ni funzo kwetu,” alisema.

Alipoulizwa iwapo wanamkumbuka Lissu katika harakati zake, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alisema, “Kila kiongozi ana wajibu wake wa kiharakati, uongozi si shule unakwenda kujifunza, kila mmoja ana vipawa vyake, wengine ni wazuri katika kuhoji, wengine katika mikutano ya hadhara, wengine mikakati na kila mmoja ana wajibu wake.

“Lissu ni moja ya wanasiasa makini na mahiri hasa linapokuja suala la kuhoji, amekuwa msaada mkubwa katika kambi ya upinzani bungeni na zaidi katika masuala ya sheria na Mahakama, kila mmoja anajua hivyo, kwa hiyo ni kweli tunaposema ‘tumemmisi’ ni kweli tumemmisi sana,” alisema.

Mbowe alisema, “Tunawashukuru Watanzania walio wengi walioshiriki kumuuguza Lissu, kumwombea, kutoa michango na salamu zao hadi amefikia hatua ile ambayo wengi hawakutegemea.

Tunawashukuru viongozi wa dini na watu waliomwombea kamanda wetu aweze kupona.”

Admit.  Mwananchi

28 December 2017,Askari anayetuhumiwa kumuua mkewe kwa risasi ajisalimisha

Makambako mji mdogo uliopo mkoani Njombe, asubuhi ya leo Askari polisi ajulikanae kwa jina la Zakayo Dotto Kileka amempiga risasi na kumsababishia kifo mpenzi wake ambae ni mwanajeshi anayejulikana kwa jina la Neema.

Mdogo wa marehemu ambaye alikua akiishi nae ameeleza kuwa Zakayo alimfumania dada yake Neema akiwa amelala na mwanaume mwingine na ugomvi mkubwa ulitokea baada ya kuona kazidiwa, Zakayo aliamua kutumia silaha.

‘’Jamaa alikimbia kwa hasira akaamua kumtwanga risasi mchumba wake’’ amesema mdogo wa Marehemu.

Hata hivyo katika harakati za kumsaka mtuhumiwa huyo, Pc Zakayo amejisalimisha kituo cha polisi Makambako asubuhi leo majira ya saa moja na nusu.

Alionekana katika vazi lake la uniform likiwa limelowa damu, lakini pia koromeo lake lameonekana kama mtu alietaka kujizuru.

Neema alikua akifanya kazi JWTZ Camp ya Makambako na Zakayo akiwa ni Polisi Makambako katika ofisi za banki ya NMB.

Mwili wa marehemu Neema umehifadhiwa katika hospitali teule ya Ilembula baada ya kufanyiwa Pm katika hospitali ya mji Makambako. Neema ataagwa leo tayari kwa kuurejesha mwili makwao kwa maziko..

28 December 2017,Mbao yazidi kuinyima Yanga usingizi

Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara klabu ya Yanga, kupitia kwa msemaji wake Dismas Ten imekiri kuwa kupata matokeo dhidi ya Mbao FC imekuwa ni jambo mgumu lakini wamejipanga vyema kwa mchezo wa Jumapili.

Ten amekiri ugumu huo wakati akiongelea maandalizi ya Yanga kuelekea mchezo huo ambao utapigwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

“Hatujawahi kupata matokeo dhidi ya Mbao FC, imekuwa ni mechi ngumu kila tunapokutana nao lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata hizo alama tatu kabla ya kwenda kwenye Kombe la Mapinduzi”, amesema Ten.

Yanga imekuwa ikipata wakati mgumu inapokutana na Mbao FC tangu ilipopanda daraja misimu miwili iliyopita ambapo katika mechi nne za ligi Yanga haijashinda hata mechi moja.

Yanga kwasasa inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 22 nyuma ya Simba SC na Azam FC zenye alama 23 kila mmoja. Ligi kuu itaendelea wikiendi hii kwa mechi za raundi ya 12 kupigwa. 
 

Wednesday, December 27, 2017

27 December 2017,Wazayuni waendelea kuwashambulia waandishi wa habari nchini Israel

Wanajeshi makatili wa Kizayuni ambao wanaikalia kwa mabavu Quds Tukufu yenye Kibla cha Kwanza cha Waislamu wamewashambulia na kuwajeruhiwa waandishi wa habari zaidi ya mia moja tangu lilipozuka wimbi la kulalamikia uamuzi wa rais wa Marekani wa kuitangaza Baytul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala pandikizi wa Israel.

Shirika la habari la Mehr limetangaza habari hiyo leo na kuyanukuu mashirika ya haki za binadamu yakisema kwamba, Wazayuni wamekuwa wakiwashambulia kwa makusudi waandishi wa habari tangu lilipozuka wimbi la kupinga kitendo cha rais wa Marekani Donald Trump cha kuitangaza Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni na kwamba kati ya waandishi hao walioshambuliwa na Wazayuni, 20 ni wanawake.

Wanajeshi makatili wa Israel wanatumia kisingizio cha kukabiliana na maandamano ya Wapalestina kuwashambulia kwa makusudi waandishi wa habari kwa risasi hai na za plastiki pamoja na mabomu ya kutoa machozi, kuwamwagaia pilipili na kuwapiga kwa marungu.

53 kati ya waandishi hao wamejeruhiwa wakati walipokuwa wanaripoti maandamano ya Wapalestina ya kumlaani Donald Trump huko Baytul Muqaddas pekee.

Hii ni katika hali ambayo idadi kubwa ya waandishi wa habari wamekamatwa na wanajeshi wa Israel wakati waandishi hao wakiwa katika kuripoti matukio mbalimbali huko Palestina katika kipindi hicho.

Kamati ya kulinda usalama wa waandishi wa habari ya Palestina imesema kuwa, lengo la utawala wa Kizayuni ni kuzuia waandishi hao wasiwafichulie walimwengu jinai kubwa zinazofanywa na Israel dhidi ya wananchi wa Palestina.

27 December 2017,Watu watatu wafariki ,mmoja Kati yao kwa kunyongwa kwa sababu ya wivu wa mapenzi Mkoani Mara

Watu watatu wamefariki dunia katika siku ya mkesha wa Krismasi wilayani Tarime mkoani Mara, wakiwemo Robhi Magaigwa (36) aliyeuawa kwa kunyongwa kwa sababu za wivu wa kimapenzi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Tarime Rorya, Henry Mwaibambe alitaja matukio mengine mawili ya vifo kuwa ni pamoja na Nyamboge Kegokora (93) aliyekufa baada ya kukanyagwa na lori la mchanga na dereva wa bodaboda Nankongo Makanda (32) aliyepata ajali ya pikipiki na kufa papo hapo.

Alisema katika tukio la kwanza mkazi wa Ronsoti, Magaigwa aliuawa kwa kunyongwa shingo na mtu anayedaiwa kuwa mpenzi wake Chacha Mangiti ama kwa jina lingine Peter Irondo.

Alieleza kuwa katika taarifa za awali, sababu za kifo hicho zinadaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi na tayari mtuhumiwa amekamatwa, kuhojiwa na anasubiriwa kupandishwa kizimbani.

Akizungumzia kifo cha Kegokora, Kamanda Mwaibambe alisema Desemba 25, gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T 766 DJN lililokuwa likiendeshwa na mmliki wa gari hilo, Chacha Borega lilimkanyaga mzee huyo aliyekuwa amekaa kando ya barabara.

Alisema pamoja na tukio hilo pia siku hiyo ya Desemba 25, mwendesha bodaboda mkazi wa Kijiji cha Pemba tarafa ya Inchugu, Makanga alipata ajali wakati akiendesha pikipiki yake kwa mwendokasi na kupatwa na mauti.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni kikoi alichokuwa amevaa kunasa kwenye rimu ya tairi ya pikipiki yake na kusababisha pikipiki hiyo ipinduke ambapo mwendesha bodaboda huyo, alikufa kutokana na majeraha makubwa aliyopata kichwani.

Admit habarileo

27 December 2017,Rais Magufuli atunukiwa tozo hii

Rais John Magufuli ametunukiwa tuzo ya amani ya Mandela (Mandela Peace Prize) kwa kuendeleza shughuli ya kulinda amani na kupigania usawa wa kijamii.

Kamati ya tuzo za Mandela kwa mwaka 2017 ilipokea maombi ya wawania tuzo 4,956.
Wengine waliotunukiwa ni Rais Uhuru Kenyatta aliyeshinda tuzo ya Mandela ya Demokrasia kutokana na kuendeleza demokrasia nchini Kenya.

Pia, Mahakama ya Juu nchini Kenya na Jeshi la Zimbabwe zimetunukiwa tuzo ya ujasiri (Mandela Boldness) kwa kufanya uamuzi kwa kijasiri kwa masilahi ya mataifa yao.

Rais wa Taasisi ya Mandela, Dk Paul Kananura amesema Rais Kenyatta ametunukiwa kwa kudhihirisha demokrasia kwa kukubali uamuzi wa Mahakama ya Juu hivyo kuheshimu kanuni za utengano wa mamlaka.

Mahakama ya Juu ya Kenya ilibatilisha matokeo ya urais katika uchaguzi wa Agosti 8,2017 yaliyompa ushindi Kenyatta na kuamuru uchaguzi kurudiwa ambao alishiriki na kuibuka mshindi.


"Hii inaonyesha kuwa Rais Kenyatta amechangia katika uimarishaji wa demokrasia Kenya,” amesema Dk Kananura.

Rais wa Chad, Idriss Itno amepata tuzo ya Mandela ya Ulinzi (Mandela Security) kutokana na sera ya kupambana na ugaidi katika maeneo ya Sahel na Ziwa Chad.

Mwingine ni Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza aliyetuzwa tuzo ya ujasiri (Mandela Courage).

Tuesday, December 26, 2017

26 December 2017,Lissu asimama kwa mara ya kwanza

Mwanasheria mkuu wa  CHADEMA na Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu ambae yuko katika mataibabu Nairobi ameweza kusimama kwa mara ya kwanza baada ya kushambuliwa.

Tundu Lissu amekuwa akipokea matibabu Nairobi tangu alipopigwa risasi na watu wasiojulikana jijini Dodoma mwezi September, 2017.

Katika picha iliowekwa katika ukurasa wa Facebook wa CHADEMA, Mbunge huyo anaonekena akisimama akisaidiwa na wahudumu wawili wa hospitali.Ujumbe ulioambatana na picha umesema“Wiki iliyopita niliwataarifu kwamba madaktari wangu wamesema ‘nitasimama, nitatembea na nitarudi Tanzania.

Leo Boxing Day (Tarehe 26 Disemba) nimeweza kusimama kwa mguu mmoja.

Hatua inayofuata ni magongo kesho na nitawajulisheni hatua nyingine katika matibabu yangu

.”“TUWAULIZE TSH MILIONI 360 WALIMPA NANI?” – MOLEL,

26 December 2017,Haya ndo matukio matatu yaliyovuta hisia za wengi mwaka huu

Wakati tukielekea mwisho wa mwaka 2017, Jeshi la Polisi limeeleza matukio matatu kuwa ndiyo yaliyovuta hisia za jamii mwaka huu mkoani Tabora

Matukio hayo ni kuuawa kwa aliyekuwa Diwani wa Muungano, wilayani Urambo, Francis Kasanga, kuuawa kwa wanawake watano wa Kijiji cha Undomo (Nzega) na kunusurika kuuawa kwa wanawake wanne, Kijiji cha Mwamabondo (Uyui).

Kamanda wa polisi mkoa wa Tabora, Wilbrod Mutafungwa alisema matukio hayo matatu ndiyo yalivuta hisia kubwa za watu na jeshi lake kufanya kazi kwa weledi mkubwa.
Katika tukio la kuuawa kwa Kasanga, Kamanda Mutafungwa alisema diwani huyo alidungwa sindano ya sumu na kisha kufungwa kamba shingoni na kutundikwa ili ionekane amejinyonga.

Alieleza kuwa tukio hilo lililotokea Julai 7 mwaka huu, limehusishwa na mambo ya kisiasa na watuhumiwa wamekamatwa na kufikishwa mahakamani.

Katika tukio la Undomo, Kamanda Mutafungwa alisema Julai 25 kwenye kitongoji cha Mwisulu, kata ya Uchama wilayani Nzega kulifanyika mkutano wa wananchi wa eneo hilo lengo likiwa ni kuwataja na kuwabaini watu wanaojihusisha na vitendo vya kishirikina.

Alieleza kuwa mkutano huo uliongozwa na Mtemi wa Sungusungu, watu watano ambao ni wanawake walipelekwa katika mkutano huo huku wakishambuliwa kwa kupigwa fimbo sehemu mbalimbali za miili yao.

Alieleza kuwa wanawake hao baadaye walipelekwa porini kisha kuuawa na miili yao kuchomwa moto huku watuhumiwa 38 wakifikishwa mahakamani.

Katika tukio la Mwamabondo la Septemba 17 mwaka huu kata ya Loya wilayani Uyui, wanawake wanne, Manugwa Lutema, Elizabeth Kashindye, Rahel Mukowangwa na Maria Sahani walikamatwa na wananchi waliojichukulia sheria mkononi kwa tuhuma kuwa wanajihusisha na vitendo vya kishirikina.

Wanawake hao walishambuliwa kwa kupigwa maeneo mbalimbali ya miili yao kwa kutumia fimbo, kufungwa vitambaa usoni na baadaye kuwarundikia nyasi na kuni kwa lengo la kuwateketeza kwa moto.

Kabla hawajachomwa moto taarifa zilifika polisi waliochukua hatua na kufanikiwa kuwaokoa wakiwa wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao.

Watuhumiwa 55 walifikishwa mahakamani.

Katika kipindi cha mwaka huu, watuhumiwa 201 wa mauaji, walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za unyang’anyi wa kutumia silaha.

Katika hatua nyingine, mkoa wa Tabora umekuwa na ongezeko la makosa ya jinai kutoka makosa 16,872 mwaka uliopita hadi makosa 17,882 mwaka huu (Januari hadi Novemba) likiwa ni ongezeko la makosa 1,010 sawa na asilimia 5.98.

Alitaja makosa yaliyoshika kasi kuripotiwa kuwa ni ya kimaadili ambayo ni 602 ukilinganisha na mwaka jana yaliyokuwa 373 ikiwa ni ongezeko la makosa 229 sawa na asilimia 61.39.

Kwa upande wa makosa ya kuwania mali yaliyoripotiwa mwaka huu ni 1,215 ukilinganisha na 1,417 mwaka jana, hivyo kuwa na upungufu wa makosa 202 sawa na asilimia 14.25.

Makosa dhidi ya binadamu yaliyoripotiwa mwaka huu ni 404 ukilinganisha na mwaka jana yaliyokuwa 431 mwaka jana ambayo ni pungufu ya makosa 27 sawa na asilimia 6.26.

“Ongezeko la makosa hayo linatokana na juhudu za askari kufanya operesheni, misako na doria katika maeneo mbalimbali mkoani Tabora,” alisema Mutafungwa.
Pamoja na hayo, polisi mkoani Tabora pia imeongeza makusanyo kutokana na adhabu za barabarani kwa zaidi ya Sh600 milioni katika kipindi cha mwaka mmoja.

Kiasi hicho kimetokana na makosa ya usalama barabarani yapatayo 55,081 hadi Novemba mwaka huu ukilinganisha na makosa 34,540 ya mwaka jana, hivyo kuwa na ongezeko la makosa 20,541 sawa na asilimia

Admit Mwananchi

26 December 2017,Yanga waanza kutekeleza mkakati huu juu ya uwanja wao wa Kaunda uliopo Jangwani

Mabingwa watetezi  wa Ligi Kuu ya soka ya Tanzania Bara, Yanga SC wameanza matengenezo ya uwanja wao  wa kaunda  uliopo eneo la Jangwani Jijini Dar es Salaam.

Mabigwa hao watetezi wa kupitia ukurasa wao wa  Instagram wameweka video ikionyesha ukarabati ukiendelea katika uwanja huo.

Video hiyo inaonyesha ikisawazisha vifusi vilivyokuwa vimemwagwa uwajani hapo kwa siku kadhaa zilizopita.

Yanga imepanga kuukarabati uwanja huo wa kaunda  na kuujenga uwanja huo pamoja na kujenga hosteli za kisasa za wachezaji.

Uwanja huo Kaunda maarufu (Jangwani) umekuwa ukiathiriwa mara kwa mara na mvua zinazonyeesha na kuusababishia kujaa maji.

Monday, December 25, 2017

25 December 2017,Watu wasiopungua 12 wafariki 30 wajeruhiwa Katika maandamano mjini Jerusalem

Watu 12 wamekwishafariki na wengine zaidi ya 30 kukamatwa na jeshi la Israel katika maandamano yaliofanyika Jerusalem na maeneo mengine Palestina baada ya rais wa Marekani kutangaza kuwa mji wa Jeusalem ni mji mkuu wa Israel

Taarifa zizlitolewa na wizara ya afya ya Palestina zimefahamisha kuwa kijana mmoja mwenye umri wa miaka 19 aliepigwa na jeshi la Israel alifariki.

Kifo cha kijana huyo kimeongeza idadi ya watu waliofariki katika maandamano hayo tangu Disemba 6.

Rais wa Marekani alitangaza kuwa ubalozi wa Marekani uliopo mjini Tel Aviv utahamishiwa mjini Jerusalem katika siku za hivi karibuni.

25 December 2017,Dkt.Shein mimi sio mpole

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein, amewaonya wale waonadhani kuwa yeye ni mpole na kwamba hawezi kuwachukulia hatua viongozi wa serikali na chama wanaovunja nidhamu na kukiuka taratibu za utendaji.

Dkt. Shein ambaye pia ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ametoa kauli hiyo katika sherehe za kumpongeza baada ya kuchaguliwa tena kushika wadhifa wa Makamu Mwenyekiti wa CCM katika Mkutano Mkuu wa tisa wa CCM uliofanyika mjini Dodoma hivi karibuni.

Amesema, kiongozi wa nchi anapaswa kutumia taratibu za uongozi na si kukurupuka kwa kuwaadhibu watu bila ya utaratibu.

Amesema yupo madhubuti na imara kwa kuwashughulikia wanaovunja nidhamu ya chama hicho na hatomuonea wala kumuadhibu mtu bila kufuata utaratibu wa maadili ya CCM.

25 December 2017, Mahasimu Sudan Kusini warushiana tuhuma

Wakuu wa serikali ya Sudan Kusini na kundi kubwa zaidi la waasi wamerushiana lawama kuhusu kukiuka mapatano ya usitishwaji mapigano yaliyaonza kutekelezwa jana.

Mapatano hayo ya amani yaliyofikiwa Alkhamisi mjini Addis Ababa Ethiopia kupitia upatinishi wa jumuiya ya maendeleo ya serikali ya nchi za Mashariki mwa Afrika IGAD.

Mapatano hayo ni sehemu ya jitihada za kieneo za kujaribu kusitisha mapigano ya nchi hiyo yaliyoanza mwezi Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu makamu wake, Riek Machar kuwa alipanga njama ya kumpindua.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumapili, kundi la waasi linaloongozwa na Machar lijulikanalo kwa jina la SPLA-IO limewatuhumu askari wa serikali kuwa wamefanya mashambulizi katika ngome za kundi hilo mjini Bieh Payam kaskazini mwa nchi hiyo na pia katika kaunti ya Yei iliyoko kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Lakini msemaji wa Jeshi la Sudan Kusini, Lul Ruai Koang amekanusha tuhuma hizo na badala yake amewalaumu waasi kuwa wamekiuka mapatano ya usitishwaji vita.

Amesema waasi wamefanya shambulizi la kuvizia dhidi ya msafara wa serikali uliokuwa unapelekea chakula na mishahara katika jimbo la Amadi kusini mwa nchi hiyo.

Wakati huo huo mahasimu wa Sudan Kusini, yaani serikali na makundi ya waasi yaliyosaini makubaliano ya amani wametakiwa kuyatekeleza kikamilifu makubaliano hayo ili kumaliza migogoro katika taifa hilo changa zaidi barani Afrika.

Jumuiya za kimataifa zikiwemo Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU) pamoja na jumuiya nyingine za kikanda na serikali zimeyapokea vizuri makubaliano hayo na kutaka wahusika wote kuyatekeleza.

Sunday, December 24, 2017

24 December 2017,Waziri Mkuu abainisha haya juu ya watumishi wa umma wasioweka mbele masilahi ya umma

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewakemea watumishi wa umma na madiwani ambao wameunda makundi ndani ya Manispaa ya Songea kwa kuweka mbele masilahi binafsi.

Onyo hilo amelitoa jana Jumamosi, Desemba 23,2017 alipozungumza na watumishi wa manispaa na madiwani kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea mkoani Ruvuma.

“Watumishi wa umma ni lazima muelewe katika halmashauri zenu mnafanya kazi na waheshimiwa madiwani sababu mnatekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi, na mnapotekeleza majukumu yenu mzingatie masilahi ya umma. Mnalo jukumu la kuhakikisha halmashauri yenu inaongozwa kitaalamu,” amesema.

Amesema, “Nanyi waheshimiwa madiwani, mtambue kuwa mnaongoza wataalamu wa fani tofauti lakini hapa Songea, madiwani mmeigawa halmashauri, mnaiendesha vibaya. Miradi haiendi vizuri kwa sababu mmejiingiza kwenye kujali masilahi yenu binafsi,” amesema.

“Mmebishana sana katika miradi ya maji, ujenzi wa kituo cha mabasi kwa sababu kila mmoja anataka mtu wake aingie. Wakati mwingine pesa zinatumwa, ninyi mnaanza kubishana tu, sasa ni mwisho.

Mkitaka kutuangusha Serikali, ama tutawafukuza uanachama au tutavunja halmashauri. Tunao uwezo wa kulivunja Baraza la Madiwani,” ameonya.

24 December 2017,Korea kaskazini yaja na hii

Baraza la ulinzi la Umoja wa Mataifa lilitangaza vikwazo vipya siku ya Ijumaa kufuatia majaribio ya makombora ya masafa marefu ya Korea Kaskazini.

Korea Kaskazini imetaja vikwazo vya hivi majuzi vya Umoja wa Mataifa dhidi yake kuwo kitendo cha vita.

Wizara ya mashauri ya nchi za kigeni ilisema kuwa hatua hizo zilikuwa ni kubwa na ngumu kwa uchumi kwa mujibu wa shirika la KNCA la Korea Kaskazini.

Iliongeza kuwa kuwa kuongeza msimamo mkali zaidi wa Korea Kaskazini ndilo jibu kwa Marekani. Baraza la ulinzi la Umoja wa Mataifa lilitangaza vikwazo vipya siku ya Ijumaa kufuatia majaribio ya makombora ya masafa marefu ya Korea Kaskazini.

Marekani ilipendekeza vikwazo hivyo na kuungwa mkono na wanacha wote 15 wa baraza la usalama la Umoja Mataifa vikiwemo vya kukata mauzo ya mafuta kwa asilimia 90 kwa Korea Kaskazini.

Korea Kaskazini tayari iko chini ya vikwani kutoka Marekani, Umoja wa Mataifa na EU.

24 December 2017,Mbaroni kwa tuhuma za kumuua mumewe

Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara linamsaka mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Zuhura Ismail (29) kwa tuhuma za kumuua mume wake baada ya kumfungia ndani na kisha kuichoma nyumba kwa petroli.

Taarifa hizo zimetolewa na Kamanda wa Polisi mkoani humo Lucas Mkondya, ambapo amesema kwamba chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi, baada ya mwanamke huyo kugundua kuwa aliyekuwa mume wake anaishi na mke mwingine, na kuamua kumvizia nyumbani kwake kisha kuichoma moto na kusababisha kifo chake.

"Ni kweli Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara linamsaka mwanamke mmoja ayefahamika kwa jina la Zuhura Ismail kwa tuhuma za kuichoma nyumba aliyokuwa anaishi mume wake na mwanamke mwingine, kutokana na wivu wa kimapenzi baada ya Zuhura kugundua kuwa mumewe anaishi na mke mwingine, na kuamua kwenda kuchoma nyumba hiyo moto na kuwasababishia majeraha makubwa, ambapo mumewe alipelekwa hospitali lakini kutokana na majereha hayo makubwa alifariki dunia, lakini mwanamke aliyekuwa nae anaendelea vizuri", amesema Kamanda Mkondya.

Aidha Kamanda Mkondya amesema mara baada ya tukio hilo mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Zuhura Ismail alitoroka na kwenda kusikojulikana, na Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka na pindi atakapopatikana watatoa taarifa.

Saturday, December 23, 2017

23 December 2017,Marekani yazidi kupingwa na nchi za jumuiya mbalimbali za kiafrika

Nchi na jumuiya mbalimbali za Kiafrika zimeendelea kuunga mkono azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopinga hatua ya Marekani ya kuitambua Quds tukufu kuwa eti ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel.

Hatua hiyo ya nchi za Afrika imechukuliwa kufuatia hatua ya Alkhamisi iliyopita ambapo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha muswada uliopendekezwa na Misri unaolaani na kupinga uamuzi wa Marekani wa kutambua rasmi Quds kuwa ni mji mkuu wa Israel.

Nchi za Afrika zimechukua msimamo huo licha ya Rais Donald Trump wa Marekani kutishia kwamba, atakata misaada ya kifedha kwa nchi yoyote itakayounga mkono azimio hilo.
Togo ilikuwa nchi peke ya Afrika iliyopinga azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Wizara ya Mambo ya Nje ya Botswana imejibu vitisho vya Marekani kwa kutoa taarifa iliyosisitiza kuwa, Gaborone haitatishwa na vitisho hivyo na itatoa kura yake kwa kufuata haki ya kujitawala na misingi ya siasa zake za kigeni.

Serikali ya Uganda pia imetoa taarifa ikiitaja Marekani kuwa ni nchi ya kijuba na kibabe.

Jamii ya Waislamu wa Zambia pia imeunga mkono azimio la UN na kupinga matakwa na viatisho vya Marekani.

23 December 2017,Waziri wa ulinzi atia maguu Kongo kuwaona wanajeshi wa JWTZ

Ikiwa zimepita siku 16 tangu kuuawa kwa askari 14 wa Jeshi laWananchi Tanzania (JWTZ) waliokuwa kwenye  oparesheni ya ulinzi wa amani katika Jamhuriya Kidemokrasia ya Congo, Waziriwa Ulinzi wa Tanzania Husssein Mwinyi  amewatembelea wanajeshi wa Tanzaenia waliopo nchini humo.

Mwinyi alifika nchini humo December 22, 2017 ambapo  alipowatembelea Wanajeshi wa Tanzania wanaoshiriki katika kikosi cha kimataifa cha kulinda amani mashariki ya Congo, na kuwatembelea wanajeshi waliojeruhiwa wakati wa shambulizi la December  7, 2017.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Beni, Mwinyiametoa wito wa kudumisha ushirikiano kati ya pande zote zinazoshiriki katika kuleta amani Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Wanajeshi 14 wa Tanzania wa kikosi maalum cha nchi za Kusinimwa Afrika SADC waliuawa na wengine 44 kujeruhiwa wakati wamajibizano ya risasi na waasi wasiojulikana katika kambi yao huko Semulik, karibu na mji wa Beni.

23 December 2017,Raia wa Uganda kizimbani kwa tuhuma ya kuingiza dola milioni moja kinyume na sheria nchini

Raia wa Uganda, Winfred Businge amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu akidaiwa kuingiza nchini dola milioni moja za Marekani bila kutoa taarifa kwa mamlaka ya forodha.

Businge (33) anadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 11 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Katika kesi hiyo namba 417 ya mwaka 2017, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Awamu Mbagwa alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha kanuni zinazotaka taarifa ya fedha kutolewa kwa mtu anayeziingiza nchini.

Baada ya kusomewa shtaka mshtakiwa alikana huku upande wa mashtaka ukidai kuwa upelelezi umekamilika.

Wakili Emmanuel Safari anayemwakilisha mshtakiwa huyo alimwomba Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kumpatia mteja wake dhamana akisema kosa linalomkabili lina dhamana.

Hakimu Shaidi alitoa masharti ya dhamana kwamba awe na mdhamini mmoja anayetambulika. Alisema fedha zilizokamatwa zitabaki mahakamani kama dhamana.

Mshtakiwa alitimiza masharti na kuachiwa kwa dhamana na kesi itatajwa Januari 18 mwakani.
Wakili Safari aliieleza Mahakama kwamba kwa kuwa upelelezi umekamilika, anaomba ipangiwe siku ya kuanza kusikilizwa.

Hakimu Shahidi alisema kwa kuwa anakwenda likizo, kesi hiyo haitaweza kuanza kusikilizwa badala yake itatajwa siku hiyo.

Rais John Magufuli alizungumza kuhusu fedha hizo Desemba 13 alipohutubia wakati akifungua tawi la Benki ya CRDB mjini Dodoma.

Friday, December 22, 2017

22 December 2017,UN yaonyesha msimamo huu juu nya maamuzi ya Marekani kuhusu Jerusalem

Licha ya vitisho vilivyotolewa na Marekani dhidi ya wanachama wa Umoja wa Mataifa, lakini Baraza Kuu la umoja huo limepasisha kwa kauli moja azimio linaloitaka Marekani kufuta kauli yake ya kuitambua Quds kuwa eti ni mji mkuu wa Israel.
Baraza hilo lenye wanachama 193 jana Alkhamisi lilipasisha kwa kura mutlaki mwito huo kwa kura 128 za ndio na 9 za hapana huku nchi 35 zikijizuia kupiga kura.

Mara baada ya kura hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif ametumia ukurasa wake wa Twitter kupongeza hatua hiyo ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kusema kuwa kura hiyo inaonesha ni majibu ya hapana kwa tishio la rais wa Marekani, Donald Trump aliyetishia kulipiza kisasi kwa taifa lolote litakalopiga kura ya kuunga mkono mwito wa kumtaka afute kauli yake ya kuitambua Baytul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala pandikizi wa Kizayuni. 
Itakumbukwa kuwa, kabla ya kupigwa kura hiyo, mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa alizitishia nchi wanachama wa umoja huo kuwa atazishitaki kwa Donald Trump.
Katika hatua nadra kushuhudiwa katika historia ya Umoja wa Mataifa, balozi huyo wa Marekani alitishia kuwa mustakbali wa uhusiano kati ya nchi hiyo na wanachama wa Umoja wa Mataifa utaangaliwa upya kwa mujibu wa kura zijazo zitakazopigwa na nchi hizo. 
Nikki Haley aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: Majina ya nchi ambazo zitapiga kura katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupinga uamuzi wa Rais wa Marekani wa kuitambua Quds kama mji mkuu wa Israel atakabidhiwa Donald Trump kwa ajili ya kuangaliwa upya uhusiano wa nchi hizo na Marekani.

Naye msemaji wa Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amelipongeza Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kusema kuwa huo ndi ushindi mwingine kwa taifa la Palestina. Nabil Abu Rudaina aidha amesema, Palestina itaendelea na jitihada zake ndani ya Umoja wa Mataifa na katika taasisi zote za kimataifa hadi itakapohakikisha nchi huru ya Palestina inaundwa, mji mkuu wake ukiwa ni Baytul Muqaddas.



22 December 2017,Bilioni mbili zamfikisha mahakamani

Siku chache baada ya Rais John Magufuli kubainisha kukamatwa kwa kiasi kikubwa cha fedha katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA) aliyekamatwa na fedha hizo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mshtakiwa huyo ni Raia wa Uganda, ambaye ni Kalani wa Kampuni ya Ulinzi ya SGA, Winfred  Businge  (33).Busige amefikishwa mahakamaniakikabiliwa na kosa la kushindwa kuelezea kwa mamlaka ya forodha fedha alizokamatwa nazo Airpot ambazo ni USD Milioni moja(takribani Sh.Bil 2).

Wakili wa serikali Mwandamizi, Awamu Mbagwa amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kosa moja.

Amedai kuwa kosa hilo amelitenda kinyume na kanuni zasheria za utakatishaji fedha, ambayo haimnyimi mshtakiwa dhamana.Wakili Mbagwa amedai kuwa Businge ametenda kosa hilo December 11, 2017 katika Uwanjawa Ndege wa Kimataifa wa JuliusNyerere (JNIA).

Inadaiwa akiwa ndani ya jiji la Dares Salaam alikutwa ameingia nchini akiwa na USD Milioni 1 (zaidi ya Sh.Bil 2) ambazo alishindwa kuzitolea maelezo kwa wakala wa forodha.

Baada ya kusomewa kosa hilo, mshtakiwa alikana kosa, ambapo wakili Mbagwa alieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na anaomba tarehe kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.

Hata hivyo, wakili wa utetezi Emmanuel Safari alimuombea dhamana mteja wake.

Hakimu Shaidi alimuachia mshtakiwa huyo kwa masharti yadhamana ya mdhamini mmoja bila kusaini bondi.

Hakimu Shaidi amesema amemuachia kwa dhamana bila bondi kwa sababu fedha zilizokamatwa zitakuwa kama dhamana yake.

Kesi imeahirishwa hadi January 18,2018.

22 December 2017,Bunge la Afrika mashariki lapewa lawama kwa hili

Katika hali inayozidi kuleta mkanganyiko kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (Eala), wabunge wawili wamechaguliwa wajumbe wa Tume ya bunge bila ya ridhaa yao.

Wabunge hao ni Fancy Nkuhi na Mariam Ussi Yahya ambao Jumatano Desemba 20,2017 walichaguliwa wajumbe wa tume licha ya umoja wa wabunge wa Tanzania katika Eala kutaka majina yao yaondolewe.

Kila mmoja alipata kura 35 katika uchaguzi uliosusiwa na wabunge wote kutoka Burundi.

Habari kutoka ndani ya Bunge zilizothibitishwa na msemaji wa Eala, Bobi Odiko zimesema wabunge wa Tanzania sasa ni wajumbe halali wa Tume licha ya Taifa hili kususia vikao tangu Jumatatu wiki hii.

Taarifa kutoka Eala zinasema wabunge hao walichaguliwa kwa kishindo kuwa wajumbe katika kikao kilichofanyika Jumatano ambacho kilihudhuriwa na wabunge watatu tu kutoka Tanzania.
Odiko alisema ni kweli umoja wa wabunge wa Tanzania ulishamwandikia barua Katibu wa Bunge la Eala mapema wiki hii kuwa majina ya Nkuhi na Yahya yaondolewe katika orodha ya wagombea ujumbe wa Tume ya Eala.

Hata hivyo, alisema ilipofika siku ya uchaguzi wagombea hao walikuwa hawajaondoa majina yao kutokana na utaratibu na ndipo walipochaguliwa kuwa wajumbe wa Tume ambayo kazi yake kubwa ni kuratibu shughuli za Bunge.

"Licha ya Tanzania kususia vikao vya Eala tangu Jumatatu baada ya kukapishwa, kulikuwa na wabunge wasiopungua watatu wakati wa uchaguzi wa wajumbe wa Tume," amesema Odiko.

Wabunge wa Eala kutoka Tanzania na Burundi wamekuwa wakisusia vikao vya Bunge kutokana na utata juu ya uchaguzi wa Spika.

Martin Ngoga alichaguliwa kuwa Spika baada ya vuta nikuvute.

Wabunge kutoka Tanzania na Burundi walisusia uchaguzi huo kwa madai kuwa haikuwa zamu ya Rwanda kuteua mgombea.

Thursday, December 21, 2017

21 December 2017,Zitto ,Mbowe wala saani moja

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe amekutana na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe kwa ajili ya kujadili masuala ya uchaguzi wa haki nchini baada yavyama hivyo kutangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio.

Zitto amekutana na Mbowe ikiwa ni siku chache baada ya kutoa taarifa kwamba watavizungukia vyama vyote vya siasa ili kujadili masuala ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa Afisa Habari wa chama hicho, Abdallah Hamis kikao cha chama hicho kilichoketi hivi karibuni na kuamua kugomea kushiriki uchaguzi wa marudio katika Kata na Majimbo mbalimbali nchini unaotarajiwa kufanyika mapema mwakani.

“Kamati Kuu ya ACT iliuagiza Uongozi wa Taifa wa Chama kuwafikia wadau wote wa Demokrasia nchini na kuweka mikakati ya pamoja ya hatua za ziada za kuchukua ili kuboresha mazingira ya chaguzi za haki nchini kwetu, kwa kuanzisha mazungumzo na vyama vyote vya Upinzani,”

Abdallah“Lengo ni kuona njia bora zaidi yamapambano ya pamoja ya kukabiliana na vitendo vya chama tawala za kuvuruga chaguzi huru na za haki nchini,”

Abdallah Zitto ameanza mazungumzo hayo na Mbowe, wakati Katibu Mkuu wa chama hicho, Dorothy Semu, akiwa anaendelea na utaratibu rasmi wa kulitekeleza suala hilo.

“Nilipewa wajibu wa kuanzisha mazungumzo ya Viongozi wa Juuwa vyama, jana nimezungumza na Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR Mageuzi, ndugu James Mbatia aliyeko hospitalini KCMC baada ya hapo nimekutana na Mbowe na kujadili kuhusu mazingira ya chaguzi za haki nchini,”–

Aidha Zitto amesema mazungumzo na viongozi hao yameenda vizuri.

21 December 2017,NEC - Mgombea ubunge Jimbo singida kaskazini kupitia tiketi ya CHADEMA hajakidhi vigezo

Mkurugenzi  wa tume ya Taifa ya Uchaguzi Ramadhan Kailima ameeleza kuwa mgombea ubunge wa CHADEMA kwenye jimbo la Singida Kaskazini wanayedai kuwa sio wa kwao kwa sababu hakupitishwa na Kamati kuu ya CHADEMA, alikidhivigezo vyote vya kupitishwa na tume kuwa mgombea.

Ameeleza kuwa kwa mujibu wa Katiba, hakuna mgombea atakayeteuliwa kwa nafasi yoyoteya ubunge isipokuwa amedhaminiwa na chama cha siasa na mgombea huyo David Djumbe amewasilisha barua iliyosainiwa na Katibu wa CHADEMA wa Wilaya

21 December 2017,Waomba wafungwa wanaoachiwa kupatiwa fedha za kuanzia maisha

Msamaha wa Rais unaotolewa kwa wafungwa ikiwamo wale wa kifungo cha maisha na kunyongwa umewaibua wadau waliopendekeza uendane na kuwaandaa kisaikolojia wanufaika ikiwamo kuwapatia fedha za kuanzia maisha.

Wamesema mfungwa aliyehukumiwa maisha au kunyongwa anakuwa kapoteza matumaini ya kurudi uraiani, hivyo anapoachiwa huru kwa msamaha wa Rais pasipo kumwandaa au kumpa mtaji hali hiyo inaweza kumfanya kurejea kosa lilelile.

Kauli hiyo waliitoa jana kwa nyakati tofauti walipozungumza na Mwananchi baada ya mmoja wa wafungwa hao, Gerald Deus (30) mkazi wa Ushirombo wilayani Bukombe mkoani Geita aliyetoka gerezani Desemba 9 kwa msamaha wa Rais John Magufuli kujikuta akirudi jela kwa miaka 15.

Mfungwa huyo alihukumiwa kifungo hicho na Mahakama ya Mwanzo Bukombe baada ya kukiri kosa la unyang’anyi wa kutumia nguvu.

Deus alihukumiwa na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Damas Gakwaya baada ya kukiri kosa la kupora Sh300,000 kutoka kwa Dina Mwende, mfanyabiashara wa soda za jumla wilayani Bukombe.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Bisimba alisema kuwaachia huru ni jambo jema, lakini kinachopaswa kufanywa na Serikali ni kuwasaidia jinsi ya kuishi katika jamii.

“Mtu anatoka gerezani hana nini wala nini na wakati mwingine hawajaandaliwa kuja kuishi kwenye jamii, mfano kuna mfungwa alifungwa akiwa na miaka 12 ametoka na miaka zaidi ya 50, sasa huyu anakujaje kuishi kwenye jamii,” alihoji Dk Bisimba.

Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), James Seka alisema:

“Hadi mtu anaachiwa anakuwa kakidhi vigezo, lakini kuna umuhimu wa jamii ikaandaliwa ili kuja kuishi nao kwani baadhi wanarudi huku mtazamo wao kwa jamii haujabadilika.”

Mwenyekiti wa Parole, Agustine Mrema alisema Rais Magufuli hakurupuki kumwachia mtu, bali anakuwa amepata taarifa kutoka kwa wakuu wa magereza na vyombo vingine hasa kwa mfungwa kuwa amekiri kosa lake na kuahidi kutorudia.

“Wakati mwingine ni tabia, mtu anajutia kosa na kuahidi kutorudia ila sisi binadamu baadhi ni vigeugeu kwenda kinyume na ndicho kinachotokea kwa baadhi yao,” alisema Mrema ambaye pia ni mwenyekiti wa TLP.

Msemaji wa Magereza nchini, Lucas Mboje alisema wamekuwa wakitoa ushauri mbalimbali kwa wafugwa ili kuachana na tabia zinazoweza kuwaweka matatani kwa kuwa hiyo ni sehemu ya wajibu wao.

Wednesday, December 20, 2017

20 December 2017,Wasomi waichambua hivi CCM

Wasomi na wanasiasa nchini wameunga mkono agizo lililotolewa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli, lililowataka viongozi wa Serikali kuwajibika mbele ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyotolewa juzi wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho, mjini Dodoma.

Wakizungumza na gazeti hili, wasomi hao akiwemo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana, alisema agizo hilo siyo jipya isipokuwalimekuwa halitekelezwi kutokana na kutukuwepo kwa msisitizo uliowekwa tangu nyuma katika masuala hayo ya uongozi.

Alisema kutokana na uwepo wa Ilani na sera zinazosimamiwa na kila chama, hakuna ubishi kwa serikali iliyowekwa madarakani na chama chochote cha siasa, kutekeleza kile kilichopo ndani ya sera kulingana na utaratibu huo uliowekwa, na kwamba agizo hilo la Rais Magufuli limelenga kuwakumbusha viongozi hao wa serikali.

“Ni kauli ya Rais, yeye pia ndiye Mwenyekiti wa Taifa wa chama na msimamizi namba moja wa Ilani na sera za chama, alichokisema hakina ubishi kuwa ndicho kinachopaswa kutekelezwa na viongozi wa serikali kwa kuwa ndiyo wenye Ilani inayotekelezwa na serikali kwa sasa,” alisema Dk Banna.

Alisema utendaji huongozwa na kusimamiwa na mambo mawili ambayo ni Katiba pamoja na Ilani ya chama, na kwamba ni suala lisilopingika pia kuona sera ikibeba mambo yote yaliyopangwa kutekelezwa katika Ilani kwa utaratibu ule ule uliowekwa na chama kilichopo madarakani

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Bashiru Ally alisema ni suala lililo wazi kuwa siasa na utendaji ni vitu visivyoweza kutenganishwa, hivyo suala la msingi ni kwa watendaji wa serikali kufuata utaratibu kwa lengo la kuepuka misuguano.

Akitolea mfano wa namna Bunge linavyoisimamia serikali, Dk Bashiru alisema kama ilivyo kwa utendaji huo, vivyo hivyo watendaji wa serikali wanapaswa kujua kuwa anayewaonesha njia ya utendaji wao ni mwanasiasa huku wote wakiwajibika kwa bosi wao ambaye ni mwananchi.

“Hakuna ubishi kuwa wanasiasa ndiyo wanaoonesha njia huku watendaji wakibaki kuwa wawajibikaji kwa kupenyeza utaalamu wao, hauwezi kuwatenganisha, jambo la msingi ni wote kufanya kazi kwa kuheshimiana ili kuepusha msuguano wa namna yoyote unaoweza kujitokeza,” alisema Dk Bashiru.

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Mhadhiri wa vyuo mbalimbali nchini, Profesa Mwesiga Baregu alisema licha ya kauli hiyo ya Rais kupokewa vyema na wajumbe wa mkutano huo na baadhi ya wananchi, bado kunahitajika ufafanuzi kwa kiasi fulani ili kuondoa misuguano baina ya wanasiasa na watumishi wa umma.

Alisema anachoona hapo ni kuwa Ilani ya chama haiwezi ikazitangulia sheria za serikali, ikiwemo taratibu wa utekelezaji wa sheria za utumishi wa umma, ila kutokana na kuzoeleka kwa hali hiyo ni vyema likajengewa utaratibu wa wazi utakaosaidia kuondoa migogoro baina ya pande hizo mbili katika jamii.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustino Mrema alisema kauli hiyo ya Rais Magufuli inatekelezeka kwa kuwa hakuna ubishi kuwa CCM ndicho chama kilichounda na kuisimamia serikali iliyopo madarakani kwa sasa.

Alisema hata kama ingekuwa hivyo kwa chama kingine chochote, ni jambo la kawaida kwa serikali kufuata na kutekeleza yale yote yaliyowekwa ndani ya Ilani ya chama hicho na mengine ni kulingana na matakwa ya chama husika ili mradi kama hayavunji utaratibu uliopo katika katiba ya nchi.

Aidha Mrema alimpongeza Rais Magufuli kwa kudai kuwa uongozi wake ‘umetukuka’ ndani ya CCM na Tanzania kwa ujumla ndani ya muda mfupi tangu aingie madarakani, kutokana na hatua yake ya kushughulikia masuala mbalimbali yakiwemo ya ufisadi na mengineyo ndani na nje ya chama chake.

Alisema CCM ya sasa kama ingekuwa ni mtu basi angesema ‘ameokoka’ kwa namna ambavyo kila kitu ndani yake kimebadilika kuanzia utendaji hadi uwajibikaji hivyo kutokana na hilo si jambo la kushangaza ‘upepo’ huo ukaelekezwa pia kwa watumishi wa umma kuiga kilichopo CCM kwa sasa.

20 December 2017, UN yakemea kitendo cha Israel kumpiga risasi na kumuua Mpalestina mlemavu

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa amesema amestaajabishwa sana na kitendo cha jeshi la Israel kumuua kwa kumpiga risasi mtu mwenye ulemavu aliyekuwa anaelekea msikitini siku ya Ijumaa

Zeid Ra'ad Al Hussein Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa ametoa kauli hiyo kufuatia ripoti kwamba mtu huyo Ibrahim Abu Thurayeh aliuawa shahidi akiwa kwenye kitimwendo chake.

Ibrahim alikuwa miongoni mwa mamia ya Wapalestina walioandamana Ijumaa karibu na uzio kati ya Ukanda wa Gaza na Israel, wakipinga hatua ya Marekani kutambua mji wa Quds (Jerusalem) kuwa eti ni mji mkuu wa utawala bandia wa Israel.

Zeid amesema taarifa zinadhihirisha kuwa jeshi la Israel lilitumia nguvu nyingi kupita kiasi kitendo ambacho ni kinyume na sheria za kimataifa za kibinadamu.

Hili ni janga la pili kumkuta Ibrahim ambapo mwaka 2008 makombora yaliyorushwa na Israel yalimkataa miguu yake miwili.

Afisa huyo wa Umoja wa Maaifa ametaka hatua za kisheria zichuliwe dhidi ya waliotekeza jinai hiyo.

Tuesday, December 19, 2017

19 December 2017,Msongamano wa watu wasababisha watu kumi kufariki ,50 wakijeruhiwa nchini Bangladesh

Msongamano wa watu umesababisha watu 10 kupoteza maisha huku wengine 50 wakiwa wamejeruhiwa nchini Bangladesh.
Kwa mujibu wa habari,msongamano na kukanyagana huko kwa watu kumetokea wakati chakula kikitolewa katika msiba wa aliyekuwa meya wa Chittagong ,Mohiuddin Chowdhury.
Famlia hiyo ilikuwa imendaa chakula kwa ajili ya watu 80,000 katika miji 12 tofauti.
Meya Mohiuddin Chowdhury73,alifariki siku ya Ijumaa.

19 December 2017,Takukuru yawapandisha mahakamani viongozi hawa watatu wa Halmashauri ya Hai mkoani Klimanjaro

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imewafikisha kortini vigogo watatu wa zamani wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Waliofikishwa mahakamani leo Jumanne Desemba 19,2017 mbele ya Hakimu Mkazi, Arnold Kirekiano ni aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Melkzedeck Humbe ambaye sasa yuko Halmashauri ya Bariadi na wenzake wawili.

Wengine waliofikishwa mahakamani ni aliyekuwa mweka hazina wa Halmashauri ya Hai, Thadeus Meela na ofisa mwandamizi, Valentina Mollel.

Mwendesha mashtaka wa Takukuru, Susan Kimaro amedai Julai 8,2014 washtakiwa walighushi nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri na kufanya malipo ya Sh27 milioni.

Washtakiwa wamekana mashitaka na wameachiwa kwa dhamana.

Wamedhaminiwa kwa bondi ya Sh5 milioni kila mmoja na kesi imepangwa kutajwa Februari 15,2018.

19 December 2017,Mahakama yaamuru hiki juu ya aliyekuwa mwenyekiti wa UVCCM mkoani Dodoma

Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma imetoa dhamana kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM na Mbunge wa Donge, Zanzibar Sadifa Juma Khamis anayetuhumiwa kwa kesi ya rushwa.

Sadifa Juma Khamis alikamatwa nyumbani kwake Dodoma December 9, 2017 kwa tuhuma za Rushwa akidaiwa kuwapa wajumbe kutoka Kagera vinywaji na pia kuahidi kuwalipia nauli ili wamchague Mwenyekiti mpya aliyekuwa akimpigia kampeni.

Monday, December 18, 2017

18 December 2017,Baraza la usalama la umoja wa mataifa kujadili juu ya Jerusalem

Baraza la Umoja wa Mataifa kukutana leo hii kujaidili suala la Jerusalem na hatma yake baada ya rais wa Marekani kutangaza kuwa mji huo ni mji mkuu wa Israel.

Suala litakalo jadiliwa katika mkutano huo wa Baraza la Usalama ni hatma ya jiji la Jerusalem na kutolea wito mataifa kutohamisha balozi zao mjini Jerusalem.

Makubaliano kuhusu maazimio yaliochukuliwa kuhusu jiji la Jerusalem yanatakiwa kuheshimishwa.

Wizara ya mambo ya nje ya Uturuki ilifahamisha Jumapili kuwa Jumatatu kutafanyika mkutano wa kuhusu Jerusalem na ukiukwaji wa makubaliano ya Umoja wa Mataifa.

Uamuzi wa Marekani kutangaza kuutangaza mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel hauna maana yeyote.

Mkutano huo wa Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa umetolewa wito na Misri baada ya Palestina kutama waraka wake.

Ikumbukwe kuwa Marekani ina kura ya turufu katika Baraza la Usalama jambo ambalo linaonekana kuwa suala la Jerusalem litafikishwa katika Umoja wa Mataifa na kutatuliwa na wanachama wote.

18 December 2017,Serikali yaokoa bilioni 156 ambazo zingetumika kwenye uchaguzi mdogo wa marudio

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) George Masaju amesema ofisi yake imeokoa Sh156 bilioni ambazo zingetumika kwa ajili ya uchaguzi wa marudio kama serikali ingeshindwa na kurudia kufanya uchaguzi katika majimbo 52.

Masaju amesema hayo wakati wa mkutano wa baraza la wafanyakazi wa ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali.

Masaju amesema kiasi hicho kiliokolewa baada ya serikali kushinda kesi 52 kati ya 53 zilizofunguliwa kupinga ushindi wa wabunge na kutaka uchaguzi urudiwe.

Kwa tafsiri hiyo gharama za uchaguzi kwa mujibu wa AG kwa jimbo moja itakuwa ni Sh3 bilioni kiasi kinachoelezwa kuwa ni kikubwa kwa uchumi wa nchi.

Masaju ambaye ni mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi wa ofisi ya mwanasheria, amesema kiasi hicho kiliokolewa baada ya ofisi yake kusimamia weledi na taaluma na haki ikapatikana kwa serikali.

18 December 2017, SHEIKH PONDA AIBWAGA JAMUHURI KATIKA RUFAA DHIDI YAKE

Mbele ya Mhe Jaji Edson Mkasimongwa sheikh Ponda Issa Ponda ameibwaga Jamhuri katika rufaa dhidi yake iliyokatwa na Mkurugenzi wa mashitaka akipinga hukumu iliyomwachia huru huko mkoani Morogoro mwaka 2015 katika mashitaka matatu ikiwemo kuchochea watu kutenda kosa la mkusanyiko usio halali na kukiuka amri ya mahakama.

Mhe Jaji alikubaliana na hoja za mawakili wa sheikh Ponda Juma Nassoro, Abubakar Salim na Hamidu Ubaid kuwa upande wa mashitaka haukuthibitisha mashitaka yao wakati wa usikilizwaji wa kesi kule Morogoro na pia hata hati ya mashitaka ilikuwa na mapungufu hasa shitaka la kwanza.

Mhe Jaji alisema haikuwa sahihi kumshitaki Sheikh Ponda kwa madai ya kukiuka amri ya mahakama ya kisutu katika mahakama ya Morogoro badala yake Sheikh ilitakiwa  apelekwe pale Mahakama ya Kisutu ajieleze tu lakini kwasababu ambazo hazijawekwa wazi DPP aliamua kufungua kesi mpya kitu ambacho hakipo kwenye sheria.

Mhe Jaji alisema maneno yanayodaiwa kuwa ya uchochezi hakuna mtu mwenye akili timamu anaweza kuchochewa nayo lakini pia ukiyasoma hayo maelezo hayatengenezi kosa lolote la jinai.

Sunday, December 17, 2017

17 December 2017,Watu watano wamefariki dunia kwa ajali ya gari ,13 Kujeruhiwa mkoani Mwanza

Watu watano wamefariki dunia na 13 wajeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea katika barabara ya Mwanza kwenda Shinyanga eneo la mtaa wa Buhongwa Nyamagana mkoa wa Mwanza baada ya gari yenye namba za usajili T.107 BKK Toyota coaster kugongana na Lori

Gari hiyo aina ya Coaster ilikuwa ikiiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina la Badru Habibu (33) mkazi wa Nyegezi na chanzo cha ajali hiyo kimefahamika kuwa ni mwendokasi wa dereva wa Coaster aliyekuwa akijaribu kuyapita magari ya mbele bila tahadhari na kusababisha vifo vya watu watano na majeruhi 13. 

Marehemu waliofariki katika ajali hiyo hadi sasa ametambulika jina moja tu ambaye ni 1. Abdul Mustafa, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 42 hadi 45, huku marehemu wengine wa nne majina yao bado hayajafahamika.

Aidha majeruhi wote kumi na tatu wapo hospitali ya rufaa ya Bugando wakipatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri, miili ya marehemu pia imehifadhiwa hospitali ya rufaa ya Bugando kwa ajili ya uchunguzi na utambuzi

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Naibu Kamishina wa polisi, Ahmed Msangi anatoa wito kwa waendeshaji wa vyombo vya moto hususani madereva wa magari ya abiria akiwataka kuwa makini pindi wawapo barabarani huku wakijua wamebeba roho za watu, hivyo wazingatie sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani ili kuepusha vifo na majeruhi ya aina kama hii yanavyoweza kuepukika. 

17 December 2017,Bunge la Afrika Mashariki kuanza shughuri zake Kesho

Bunge la Afrika Mashariki EALA linatazamiwa kurejelea shughuli zake kuanzia kesho Jumatatu baada ya Kenya kuwateua wawakilishi wake katika chombo hicho cha kieneo.

Msemaji wa EALA, Bobi Odiko amesema miongoni mwa ajenda za kwanza kwenye kikao hicho ni kuapishwa kwa wabunge wa bunge hilo lenye makao yake Arusha, Tanzania.

Aidha Spika wa bunge hilo atateuliwa pamoja na wanachama wa kamisheni na tume mbali mbali za bunge hilo la Afrika Mashariki.
Kadhalika bunge hilo la kieneo linasubiriwa na kibarua cha kujadili na kupasisha kuwa sheria, miswada 13.

Itakumbukwa kuwa, Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki walitazamiwa kuapishwa Juni 6 mwaka huu na kuanza vikao vyao mara moja, lakini hilo halikufanyika kwa kuwa Kenya ilichelewa kuwateua wanachama wake 9 wa kuiwakilisha katika taasisi hiyo ya kikanda.

Kenya iliwaidhinisha wanachama wake wa EALA Alkhamisi iliyopita, na hivyo kutamatisha mkwamo huo wa karibu nusu mwaka.

17 December 2017,Aliyetoka kwa msamaha wa Rais ahukumiwa tena jela miaka 15

Gerald Deus (30), mkazi wa Ushirombo wilayani Bukombe mkoani Geita aliyetoka jela kwa msamaha wa Rais, amehukumiwa tena kifungo cha miaka 15 jela.

Deus aliyehukumiwa kifungo hicho juzi na Mahakama ya Mwanzo Bukombe baada ya kukiri kosa la unyang’anyi wa kutumia nguvu, ni miongoni mwa wafungwa 8,157 waliopewa msamaha Desemba 9 na Rais John Magufuli.

Msamaha huo wa Rais ulitolewa wakati wa maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara).

Deus alihukumiwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Bukombe, Damas Gakwaya baada ya kukiri kosa la kupora Sh300,000 kutoka kwa Dina Mwende, mfanyabiashara wa soda za jumla wilayani Bukombe.

Tukio hilo kwa mujibu wa mwendesha mashtaka wa Polisi, Mohamed Simai lilitokea katika Mtaa wa Malendeja, Kata ya Katente wilayani Bukombe saa sita mchana Desemba 14, ikiwa ni siku nne tu tangu mshtakiwa huyo atoke gerezani.

Simai aliiambia Mahakama kuwa kabla ya kupora kiasi hicho cha fedha, mshtakiwa alifika dukani akijifanya anataka kununua soda za jumla kwa ajili ya vibarua aliodai walikuwa wakilima shambani kwake.

“Wakati muuza soda akiendelea kupanga kreti dukani, ghafla mshtakiwa alimvamia na kumpora Sh300,000 na kuanza kutimua mbio kabla ya kukamatwa na raia wema waliojitokeza kutoa msaada baada ya kelele za aliyeporwa fedha,” Simai aliieleza Mahakama.

Mwendesha mashtaka alisema baada ya kumkamata, wananchi walianza kumshambulia lakini aliokolewa na polisi waliofika eneo la tukio.

Baada ya kusomewa mashtaka, mshtakiwa Deus alikiri kutenda kosa hilo na kuiomba Mahakama imhurumie kwa kumpa adhabu ndogo kwa sababu ana siku tano tu tangu alipotoka gerezani kwa msamaha wa Rais Magufuli.

Akitoa hoja baada ya mshtakiwa kukiri kosa, mwendesha mashtaka aliiomba Mahakama kumpa Deus adhabu kali kwa sababu anaonekana ni mhalifu mzoefu na hajajifunza kwa kipindi cha miezi sita aliyokaa gerezani akitumikia kifungo cha mwaka mmoja alichohukumiwa kwa kosa la wizi.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama, Juni Mosi, mwaka huu, Deus alihukumiwa kifungo cha miezi 12 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la wizi wa nguo mali ya Naomi Musa, mkazi wa Mtaa wa Kapela, Kata ya Igulwa katika mji mdogo wa Ushirombo wilayani Bukombe.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mujuni Mchunguzi wa Mahakama ya Mwanzo Bukombe katika shauri la jinai namba 188/2017.

Kabla ya kutoka kwa msamaha wa Rais Desemba 9, mshtakiwa alikuwa akitumikia adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela katika Gereza la Kahama ambako ndiko alikorejeshwa juzi.

“Kwa sababu mshtakiwa amekiri kosa; na kwa kuzingatia ametenda kosa hilo siku chache tu baada ya kutoka Magereza kwa msamaha wa Rais; naiomba Mahakama kumpa adhabu kali ili iwe fundisho kwake na watu wengine wenye nia ya kutenda kosa kama hilo,” aliomba Simai.

Akitoa hukumu, Hakimu Gakwaya aliyeonyesha mshangao kwa mshtakiwa kushindwa kutumia vizuri msamaha wa Rais Magufuli, alisema Mahakama inamhukumu kifungo cha miaka 15 jela badala ya miaka 30 aliyostahili kwa mujibu wa sheria kwa sababu hakuisumbua Mahakama kwa kukiri kosa.

“Kwa sababu hujaisumbua Mahakama kwa kukiri kosa; nakupa adhabu ya onyo ya miaka 15 na kazi ngumu gerezani ili iwe fundisho kwako na kwa wengine,” alisema hakimu Gakwaya.

Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa kifungu cha 285 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 16 na marekebisho yake ya mwaka 2002.

Admit Mwananchi