Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewakemea watumishi wa umma na madiwani ambao wameunda makundi ndani ya Manispaa ya Songea kwa kuweka mbele masilahi binafsi.
Onyo hilo amelitoa jana Jumamosi, Desemba 23,2017 alipozungumza na watumishi wa manispaa na madiwani kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea mkoani Ruvuma.
“Watumishi wa umma ni lazima muelewe katika halmashauri zenu mnafanya kazi na waheshimiwa madiwani sababu mnatekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi, na mnapotekeleza majukumu yenu mzingatie masilahi ya umma. Mnalo jukumu la kuhakikisha halmashauri yenu inaongozwa kitaalamu,” amesema.
Amesema, “Nanyi waheshimiwa madiwani, mtambue kuwa mnaongoza wataalamu wa fani tofauti lakini hapa Songea, madiwani mmeigawa halmashauri, mnaiendesha vibaya. Miradi haiendi vizuri kwa sababu mmejiingiza kwenye kujali masilahi yenu binafsi,” amesema.
“Mmebishana sana katika miradi ya maji, ujenzi wa kituo cha mabasi kwa sababu kila mmoja anataka mtu wake aingie. Wakati mwingine pesa zinatumwa, ninyi mnaanza kubishana tu, sasa ni mwisho.
Mkitaka kutuangusha Serikali, ama tutawafukuza uanachama au tutavunja halmashauri. Tunao uwezo wa kulivunja Baraza la Madiwani,” ameonya.
No comments:
Post a Comment