Wasomi na wanasiasa nchini wameunga mkono agizo lililotolewa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli, lililowataka viongozi wa Serikali kuwajibika mbele ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyotolewa juzi wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho, mjini Dodoma.
Wakizungumza na gazeti hili, wasomi hao akiwemo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana, alisema agizo hilo siyo jipya isipokuwalimekuwa halitekelezwi kutokana na kutukuwepo kwa msisitizo uliowekwa tangu nyuma katika masuala hayo ya uongozi.
Alisema kutokana na uwepo wa Ilani na sera zinazosimamiwa na kila chama, hakuna ubishi kwa serikali iliyowekwa madarakani na chama chochote cha siasa, kutekeleza kile kilichopo ndani ya sera kulingana na utaratibu huo uliowekwa, na kwamba agizo hilo la Rais Magufuli limelenga kuwakumbusha viongozi hao wa serikali.
“Ni kauli ya Rais, yeye pia ndiye Mwenyekiti wa Taifa wa chama na msimamizi namba moja wa Ilani na sera za chama, alichokisema hakina ubishi kuwa ndicho kinachopaswa kutekelezwa na viongozi wa serikali kwa kuwa ndiyo wenye Ilani inayotekelezwa na serikali kwa sasa,” alisema Dk Banna.
Alisema utendaji huongozwa na kusimamiwa na mambo mawili ambayo ni Katiba pamoja na Ilani ya chama, na kwamba ni suala lisilopingika pia kuona sera ikibeba mambo yote yaliyopangwa kutekelezwa katika Ilani kwa utaratibu ule ule uliowekwa na chama kilichopo madarakani
Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Bashiru Ally alisema ni suala lililo wazi kuwa siasa na utendaji ni vitu visivyoweza kutenganishwa, hivyo suala la msingi ni kwa watendaji wa serikali kufuata utaratibu kwa lengo la kuepuka misuguano.
Akitolea mfano wa namna Bunge linavyoisimamia serikali, Dk Bashiru alisema kama ilivyo kwa utendaji huo, vivyo hivyo watendaji wa serikali wanapaswa kujua kuwa anayewaonesha njia ya utendaji wao ni mwanasiasa huku wote wakiwajibika kwa bosi wao ambaye ni mwananchi.
“Hakuna ubishi kuwa wanasiasa ndiyo wanaoonesha njia huku watendaji wakibaki kuwa wawajibikaji kwa kupenyeza utaalamu wao, hauwezi kuwatenganisha, jambo la msingi ni wote kufanya kazi kwa kuheshimiana ili kuepusha msuguano wa namna yoyote unaoweza kujitokeza,” alisema Dk Bashiru.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Mhadhiri wa vyuo mbalimbali nchini, Profesa Mwesiga Baregu alisema licha ya kauli hiyo ya Rais kupokewa vyema na wajumbe wa mkutano huo na baadhi ya wananchi, bado kunahitajika ufafanuzi kwa kiasi fulani ili kuondoa misuguano baina ya wanasiasa na watumishi wa umma.
Alisema anachoona hapo ni kuwa Ilani ya chama haiwezi ikazitangulia sheria za serikali, ikiwemo taratibu wa utekelezaji wa sheria za utumishi wa umma, ila kutokana na kuzoeleka kwa hali hiyo ni vyema likajengewa utaratibu wa wazi utakaosaidia kuondoa migogoro baina ya pande hizo mbili katika jamii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustino Mrema alisema kauli hiyo ya Rais Magufuli inatekelezeka kwa kuwa hakuna ubishi kuwa CCM ndicho chama kilichounda na kuisimamia serikali iliyopo madarakani kwa sasa.
Alisema hata kama ingekuwa hivyo kwa chama kingine chochote, ni jambo la kawaida kwa serikali kufuata na kutekeleza yale yote yaliyowekwa ndani ya Ilani ya chama hicho na mengine ni kulingana na matakwa ya chama husika ili mradi kama hayavunji utaratibu uliopo katika katiba ya nchi.
Aidha Mrema alimpongeza Rais Magufuli kwa kudai kuwa uongozi wake ‘umetukuka’ ndani ya CCM na Tanzania kwa ujumla ndani ya muda mfupi tangu aingie madarakani, kutokana na hatua yake ya kushughulikia masuala mbalimbali yakiwemo ya ufisadi na mengineyo ndani na nje ya chama chake.
Alisema CCM ya sasa kama ingekuwa ni mtu basi angesema ‘ameokoka’ kwa namna ambavyo kila kitu ndani yake kimebadilika kuanzia utendaji hadi uwajibikaji hivyo kutokana na hilo si jambo la kushangaza ‘upepo’ huo ukaelekezwa pia kwa watumishi wa umma kuiga kilichopo CCM kwa sasa.
No comments:
Post a Comment