Saturday, December 23, 2017

23 December 2017,Raia wa Uganda kizimbani kwa tuhuma ya kuingiza dola milioni moja kinyume na sheria nchini

Raia wa Uganda, Winfred Businge amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu akidaiwa kuingiza nchini dola milioni moja za Marekani bila kutoa taarifa kwa mamlaka ya forodha.

Businge (33) anadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 11 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Katika kesi hiyo namba 417 ya mwaka 2017, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Awamu Mbagwa alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha kanuni zinazotaka taarifa ya fedha kutolewa kwa mtu anayeziingiza nchini.

Baada ya kusomewa shtaka mshtakiwa alikana huku upande wa mashtaka ukidai kuwa upelelezi umekamilika.

Wakili Emmanuel Safari anayemwakilisha mshtakiwa huyo alimwomba Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kumpatia mteja wake dhamana akisema kosa linalomkabili lina dhamana.

Hakimu Shaidi alitoa masharti ya dhamana kwamba awe na mdhamini mmoja anayetambulika. Alisema fedha zilizokamatwa zitabaki mahakamani kama dhamana.

Mshtakiwa alitimiza masharti na kuachiwa kwa dhamana na kesi itatajwa Januari 18 mwakani.
Wakili Safari aliieleza Mahakama kwamba kwa kuwa upelelezi umekamilika, anaomba ipangiwe siku ya kuanza kusikilizwa.

Hakimu Shahidi alisema kwa kuwa anakwenda likizo, kesi hiyo haitaweza kuanza kusikilizwa badala yake itatajwa siku hiyo.

Rais John Magufuli alizungumza kuhusu fedha hizo Desemba 13 alipohutubia wakati akifungua tawi la Benki ya CRDB mjini Dodoma.

No comments: