Monday, December 25, 2017

25 December 2017, Mahasimu Sudan Kusini warushiana tuhuma

Wakuu wa serikali ya Sudan Kusini na kundi kubwa zaidi la waasi wamerushiana lawama kuhusu kukiuka mapatano ya usitishwaji mapigano yaliyaonza kutekelezwa jana.

Mapatano hayo ya amani yaliyofikiwa Alkhamisi mjini Addis Ababa Ethiopia kupitia upatinishi wa jumuiya ya maendeleo ya serikali ya nchi za Mashariki mwa Afrika IGAD.

Mapatano hayo ni sehemu ya jitihada za kieneo za kujaribu kusitisha mapigano ya nchi hiyo yaliyoanza mwezi Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu makamu wake, Riek Machar kuwa alipanga njama ya kumpindua.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumapili, kundi la waasi linaloongozwa na Machar lijulikanalo kwa jina la SPLA-IO limewatuhumu askari wa serikali kuwa wamefanya mashambulizi katika ngome za kundi hilo mjini Bieh Payam kaskazini mwa nchi hiyo na pia katika kaunti ya Yei iliyoko kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Lakini msemaji wa Jeshi la Sudan Kusini, Lul Ruai Koang amekanusha tuhuma hizo na badala yake amewalaumu waasi kuwa wamekiuka mapatano ya usitishwaji vita.

Amesema waasi wamefanya shambulizi la kuvizia dhidi ya msafara wa serikali uliokuwa unapelekea chakula na mishahara katika jimbo la Amadi kusini mwa nchi hiyo.

Wakati huo huo mahasimu wa Sudan Kusini, yaani serikali na makundi ya waasi yaliyosaini makubaliano ya amani wametakiwa kuyatekeleza kikamilifu makubaliano hayo ili kumaliza migogoro katika taifa hilo changa zaidi barani Afrika.

Jumuiya za kimataifa zikiwemo Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU) pamoja na jumuiya nyingine za kikanda na serikali zimeyapokea vizuri makubaliano hayo na kutaka wahusika wote kuyatekeleza.

No comments: