Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema matukio ya watoto kupotea yameongezeka kutoka watoto 17 mwaka jana, hadi watoto 22 mwaka huu, ambayo ni sawa na asilimia 29.4.
Amesema takwimu hizo ni kuanzia Januari hadi Desemba, huku akibainisha watoto hao huibiwa na wanawake ambao hawajabahatika kupata watoto.
Mambosasa alitoa kauli hiyo jana katika mkutano na waandishi wa habari wakati akieleza matukio ya uhalifu, watoto kutupwa, jinai na dawa za kulevya yaliyotokea mwaka huu akilinganisha na mwaka jana.
Akifafanua kuhusu watoto kupotea, alisema huibiwa hospitali, majumbani na katika shule wanazosoma.
Pia, alisema watoto waliotupwa wameongezeka na kufikia 21 sawa na asilimia 31.25 katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka huu, ikilinganishwa na mwaka 2016 ambako walikuwa 16.
“Matukio ya kikatili dhidi ya watoto yameongezeka ikiwamo baadhi ya wazazi kuwatupa katika majalala na vyoo,” alisema Mambosasa.
Kuhusu matukio ya uhalifu alisema yalikuwa 126,200 ukilinganisha na kipindi cha mwaka 2016 yalikuwa 129,602 takwimu alizosema kuwa zimepungua kwa asilimia 2.6.
Alisema matukio ya jinai yalikuwa 9,736 ikilinganisha na mwaka 2016 yalikuwa 12,550, ikiwa ni pungufu kwa matukio 2,814 sawa na asilimia 22.4.
“Jeshi linaimarisha doria na misako, wahalifu 18,194 walikamatwa kwa tuhuma mbalimbali kuanzia Januari hadi Desemba 2017.
“Bangi zenye uzito wa zaidi ya kilogramu 2,455 zilikamatwa na watuhumiwa walikuwa 5,205; hatua za kisheria zimechukuliwa,” alisema.
Alisema kilogramu 1.444 za dawa za kulevya aina ya cocaine zilikamatwa, heroine kilogramu 2.234 huku jumla ya watuhumiwa 352 wakikamatwa, “kesi zilizofunguliwa zilikuwa 201.
Mirungi ilikamatwa kilogramu 96.702, jumla ya watuhumiwa waliokamatwa wakijihusisha na mirungi hiyo ni 184, na kesi 57 zilifunguliwa.”
Alisema Polisi imejipanga kupunguza uhalifu mwaka 2018, ikiwa ni pamoja na kuelimisha wafanyabiashara wakubwa kuweka kamera za CCTV katika maeneo ya biashara zao ili kusaidia ulinzi.
Admit Mwananchi
No comments:
Post a Comment