Licha ya vitisho vilivyotolewa na Marekani dhidi ya wanachama wa Umoja wa Mataifa, lakini Baraza Kuu la umoja huo limepasisha kwa kauli moja azimio linaloitaka Marekani kufuta kauli yake ya kuitambua Quds kuwa eti ni mji mkuu wa Israel.
Baraza hilo lenye wanachama 193 jana Alkhamisi lilipasisha kwa kura mutlaki mwito huo kwa kura 128 za ndio na 9 za hapana huku nchi 35 zikijizuia kupiga kura.
Mara baada ya kura hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif ametumia ukurasa wake wa Twitter kupongeza hatua hiyo ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kusema kuwa kura hiyo inaonesha ni majibu ya hapana kwa tishio la rais wa Marekani, Donald Trump aliyetishia kulipiza kisasi kwa taifa lolote litakalopiga kura ya kuunga mkono mwito wa kumtaka afute kauli yake ya kuitambua Baytul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala pandikizi wa Kizayuni.
Itakumbukwa kuwa, kabla ya kupigwa kura hiyo, mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa alizitishia nchi wanachama wa umoja huo kuwa atazishitaki kwa Donald Trump.
Katika hatua nadra kushuhudiwa katika historia ya Umoja wa Mataifa, balozi huyo wa Marekani alitishia kuwa mustakbali wa uhusiano kati ya nchi hiyo na wanachama wa Umoja wa Mataifa utaangaliwa upya kwa mujibu wa kura zijazo zitakazopigwa na nchi hizo.
Nikki Haley aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: Majina ya nchi ambazo zitapiga kura katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupinga uamuzi wa Rais wa Marekani wa kuitambua Quds kama mji mkuu wa Israel atakabidhiwa Donald Trump kwa ajili ya kuangaliwa upya uhusiano wa nchi hizo na Marekani.
Naye msemaji wa Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amelipongeza Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kusema kuwa huo ndi ushindi mwingine kwa taifa la Palestina. Nabil Abu Rudaina aidha amesema, Palestina itaendelea na jitihada zake ndani ya Umoja wa Mataifa na katika taasisi zote za kimataifa hadi itakapohakikisha nchi huru ya Palestina inaundwa, mji mkuu wake ukiwa ni Baytul Muqaddas.
No comments:
Post a Comment