Thursday, November 30, 2017

30 November 2017,Serikali yanasa zaidi ya kilo Sita za madini ya dhahabu

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya DSM kitengo cha makosa ya rushwa na uhujumu uchumi kimetaifisha kilo zaidi ya sita za madini ya dhahabu yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 507 iliyokuwa imepangwa kusafirisha kwa njia za magendo kutoka Dar es salaam kwenda Zanzibar.

Hatua hiyo inafuatia hatua ya serikali kushinda kesi dhidi ya wafanyabiashara wawili wa jijini waliokuwa wakishirikiana na mchimba madini kutoka Geita Kalangalala Mashaka Lucas.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,Huruma Said watuhumiwa wamekiri kosa chini ya sheria ya makosa ya uhujumu uchumi namba 67 ya mwaka 2017.

Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Biswalo Mganga amethibitisha kutaifishwa kwa miche mitano ya dhahabu na kuwataja wafanyabiashara wakazi wa Dar es salaam waliokuwa wakishirikiana na mfanyabiashara kutoka Geita kuwa ni Jaffar Hussein na Latiff Mohamed.

30 November 2017,Wabunge waliotimuliwa CUF Kulisikilizia Bunge kwa jirani

Katibu wa Bunge, Steven Kagaigai amesema nafasi za ubunge zilizoachwa wazi baada wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF) kufukuzwa uanachama, zilijazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa Sheria, na Wabunge waliopatikana kujaza nafasi hizo wanaendelea kutekeleza majukumu yao ya kibunge.

Amesema kumekuwapo na tafsiri isiyo sahihi ya uamuzi wa Mahakama inayotolewa na baadhi ya watu na vyombo vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii kusambaza taarifa potofu kwamba wabunge waliofukuzwa na CUF wamerejeshwa bungeni kwa uamuzi wa Mahakama baada ya kurejeshewa uanachama.

Katika taarifa yake aliyoitoa leo Novemba 30, Kagaigai amesema waliokuwa wabunge pia wameiandikia Ofisi ya Bunge wakiomba kufahamishwa utaratibu utakaotumika kuwarejesha bungeni.

“Ni vema ifahamike kuwa, hakuna sehemu yeyote katika uamuzi huo wa Mahakama inapoelezwa kuwa Wabunge hao wanatakiwa kurudishiwa ubunge wao.

“Uamuzi huo wa mahakama ni wa awali uliotolewa kwenye mapingamizi ya awali na uliwalenga walalamikiwa ambao ni Baraza la Wadhamini wa CUF pamoja na uongozi wake ambao uliamuru kuwa walalamikiwa wasitishe utekelezaji wa uamuzi wa kuwafukuza uanachama na kutojadili suala lolote kuhusu uanachama wa Walalamikaji hao hadi Mahakama itakapokamilisha kusikiliza shauri la msingi,” imesema taarifa hiyo.

Novemba 10, mwaka huu Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitoa uamuzi wa awali katika shauri lililofunguliwa na waliokuwa wabunge wanane wa Viti Maalumu CUF, lililofunguliwa kupinga uamuzi wa chama hicho kuwafukuza uanachama.

30 November 2017,Zaidi ya viongozi 80 kutoka Afrika na Ulaya waketi kuzungumzia uchumi na Uhamiaji nchini Ivory Coast

Zaidi ya viongozi 80 kutoka Afrika na Ulaya wamekutana nchini Ivory Coast siku ya Jumatano ya jana

Kwa mujibu wa habari,viongozi hao wamekutana katika mji mkuu wa Abidjan kwa muda wa siku mbili kuzungumzia masuala ya uchumi pamoja na uhamiaji.

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Macky Sall wa Senegal,Emmanuel Macron wa Ufaransa,Muhamadu Buhari wa Nigeria.

Kabla ya rais Macron kuhudhuria mkutano huo alipitia Burkina Faso kuzungumzia suala la kupambana na ugaidi.

Macron anaonekana kutengeneza uhusiano mzuri na viongozi mbalimbali barani Afrika.

30 November 2017,Mbunge wa CUF aliamsha dude Mahakamani

Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh ameruka kihunzi cha Serikali mahakamani, baada ya kushinda pingamizi la awali lililowekwa na Serikali katika kesi ya kuhoji uhalali wa wajumbe wapya wa bodi ya wadhamini wa chama hicho.

Saleh ambaye pia ni mwanasheria amefungua kesi Mahakama Kuu akihoji uhalali wa wajumbe wapya wa bodi waliosajiliwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).

CUF imegawanyika pande mbili; inayomuunga mkono Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na inayomuunga Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ambaye ndiye aliunda bodi inayopingwa.

Wadaiwa katika kesi hiyo ni Ofisa Mtendaji wa Rita, anayewakilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kupitia jopo la mawakili wa Serikali linaloongozwa na Gabriel Malata.

Wengine ni bodi ya wadhamini (mpya) ya CUF, mwenyekiti wa bodi hiyo, Peter Malebo, wanaowakilishwa na wakili Majura Magafu na wajumbe wapya wa bodi hiyo wanaowakilishwa na wakili Mashaka Ngole.

Wadaiwa wengine ni wajumbe wa bodi waliomaliza muda wao na ambao wengine walipendekezwa tena na upande wa Maalim Seif ambao hata hivyo hawakuidhinishwa na Rita, wanaowakilishwa na mawakili Juma Nassoro, Daimu Halfan na Hashim Mziray.

Serikali kwa niaba ya mdaiwa wa kwanza (Mtendaji wa Rita), iliweka pingamizi la awali ikiiomba Mahakama iitupilie mbali kesi, ikitoa hoja kuwa imefunguliwa kabla ya wakati bila kufuata utaratibu wa kuishtaki Serikali na kwamba mdai amemshtaki mtu asiyestahili.

Saleh anayewakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Fatma Karume, ameshinda pingamizi hilo katika uamuzi uliotolewa na Jaji Wilfred Dyansobera alioutoa jana Jumatano, Novemba 29,2017.

Jaji Dyansobera ametupilia mbali pingamizi hilo la Serikali baada ya kuridhika kuwa hoja za pingamizi hilo hazikuwa na mashiko.

Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo, wakili Malata alidai mdai amemshtaki mtu asiye sahihi; akidai Rita ni wakala ndani ya ofisi ya Kabidhi Wasihi Mkuu ambaye ndiye aliyestahili kushtakiwa na si mtendaji wa Rita.

Pia, alidai kesi ilifunguliwa kabla ya wakati kwa kuwa ilifunguliwa kabla ya kutoa taarifa ya kusudio kwa Serikali ya siku 90, kama inavyoelekezwa katika sheria ya mashauri dhidi ya Serikali.

Wakili Mpoki alipinga hoja hizo akidai mtu waliyemshtaki ni sahihi na kwamba, kwa aina ya kesi hiyo hapakuwa na haja ya kutoa taarifa ya siku 90 kwa Serikali kwa kuwa hawaishtaki Serikali.

Jaji Dyansobera katika uamuzi wake amekubali hoja za upande wa mdai, kuwa suala la nani ashtakiwe na nani asishtakiwe ni jukumu la mdai kwa kuwa ndiye anaona kuwa nafuu anazoziomba atazipata kwa nani.

Amesema kesi hiyo haikuhitaji kutoa taarifa ya siku 90 kwa Serikali kwa kuwa si Serikali inayoshtakiwa bali kesi hiyo inahusu mgogoro wa ndani ya chama cha siasa, ambako Serikali haipaswi kujiingiza wala kuwa na upande.

Jaji Dyansobera amepanga kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo Desemba 8,2017 kwa kusikiliza hoja za msingi za mbunge Saleh na majibu ya wadaiwa na kisha atapanga tarehe ya kutoa uamuzi.

Wednesday, November 29, 2017

29 November 2017,Makamu wa Rais amfariji Lissu hospitalini mjini Nairobi

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amemtembelea Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu anayepatiwa matibabu katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya baada ya kujeruhiwa kwa risasi na watu wasiofahamika mkoani Dodoma. 
Makamu wa Rais amemtembelea Lissu baada ya kushiriki kuapishwa kwa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta. 
Akizungumza na Makamu wa Rais Tundu Lissu amemwomba Makamu wa Rais afikishe salamu zake kwa Rais Dkt. John Magufuli

29 November 2017,Waziri mkuu abaini jumla ya malori 44 yaliyokuwa yanatolewa kimagendo bandarini

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Novemba 29, 2017  amefanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Dar es salaam na kubaini malori 44  yaliyokuwa yakitaka kutolewa bandarini hapo bila ya kufuata utaratibu.
Akiwa bandarini Waziri Mkuu Majaliwa amewataka mawakala kuwa makini na watu wanaowarubuni wawasaidie kupitisha mizigo kwa kutaja majina ya viongozi wakuu wa serikali.

29,November 2017, watu 40 wameuawa ,19 kujeruhiwa na wezi wa zaidi ya mifugo 1,000 Sudan kusini


 watu 40 wameuawa  na   19 kujeruhiwa na wezi walioiba zaidi ya mifugo  1000    siku moja kabla  ya leo  Sudan kusini   
Kwa mujibu wa taarifda zilizotolewa na serikali watu 40 wameuawa na wengine 19 wamejeruhiwa na wezi wa mifugo baada ya kuvamiwa Jumanne katika mkoa wa Jongleri.
Taarifa zinafahamisha kuwa ghasia zinazidi kuongezeka katika eneo hilo.
Waziri wa habari wa Sudani Kusini Jacob Akech Dengdit ameafahamisha kuwa wezi hao wamesababisha vifo vya watu 40 na kuwateka wengine kadhaa.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa ni kwamba watu hao waliokuwa na silaha walitokea katika eneo la Boma.
Wahalifu hao wanaonekana kuwa na lengo la kufifiza zoezi la serikali ya Sudani Kusini ya kurejesha amani ya kudumu.
Mara kwa mara wahalifu kutoka Murle Boma wamekuwa wakivamia raia na kuwapora mali na mifugo yao.
Zaidi ya mifugo  1 000 imeibiwa huku watoto na wanawake wakitekwa na wahailifu hao.

Tuesday, November 28, 2017

28 November 2017,Jiji la Mwanza kuwa kinara kwa ukusanyaji pato nchini

Jiji la  Mwanza kuwa kinara  kwa  ukusanyaji pato nchini baada  uzinduzi  wa mwongozo wa uwekezaji ukiweka mikakati ya kuupiku Dar es Salaam katika uchangiaji wa pato la Taifa.

Mwongozo huo umeandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (ESRF), kwa ufadhili wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema jana Jumatatu Novemba 27,2017 kuwa fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya kilimo, uvuvi, madini, viwanda na biashara ndizo zitatumika kuipiku Dar es Salaam.

“Tumejipanga kuongeza mchango wa Mkoa wa Mwanza katika pato la Taifa kutoka Sh7.4 trilioni za sasa hadi zaidi ya Sh10 trilioni kwa mwaka ifikapo 2025 kulingana na dira ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo muda huo,” amesema Mongella.

Mtaalamu kutoka ESRF, Dk Bohela Lunogelo amesema pato la mwananchi wa Mkoa wa Mwanza ni zaidi ya Sh2 milioni kwa mwaka.

Mongella amesema mkoa utaunda timu maalumu ya wataalam kutoka mamlaka, taasisi na idara za Serikali zinazohusika na utoaji wa vibali na leseni ili kuwapunguzia wawekezaji urasimu wa kimfumo, hasa vibali na leseni za kuanzisha biashara.

“Hatulengi kuvunja kanuni na utaratibu; lakini hatuna budi kuchukua uamuzi pale urasimu wa kimfumo unapokuwa kikwazo kufikia malengo yetu ya maendeleo,” amesema Mongella




28 November 2017,Zitto Kabwe mahusiano ya Tanzania na kenya hayapo vizuri

Zitto Kabwe amefunguka  na kusema  mahusiano ya Tanzania na Kenya hayapo vizuri baada  ya kitendo cha Makamu wa Rais Mhe. Samia kupokelewa na Balozi Kenya na kudai Rais Magufuli kutokwenda kwenye sherehe za kuapishwa Kenyatta inaweza kueleweka.

Zitto Kabwe amesema hayo kupitia mtandao wake wa twitter na kusema kitendo cha Rais Magufuli kutohudhuria kwenye sherehe za kuapishwa kwa Rais mteule wa Kenya Uhuru Kenyatta inaweza kueleweka kwani kiongozi huyo hakuweza kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame.

"Makamu wetu wa Rais kupokelewa na Balozi ( sio hata Waziri wa Mashauri ya Kigeni au Waziri mwengine) ni dalili kuwa mahusiano yetu yanalega lega. Rais kutokwenda Kenya inaweza kueleweka maana hata Rwanda hakwenda kwenye uapishaji wa Paul Kagame" aliandika Zitto Kabwe. 

28 November 2017,Ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni punda wanane wawekwa siku nne gerezani nchini India

Ukistajabu ya Mussa utayaona ya ferauni  punda wanane wametupwa gerezani kwa muda wa siku nne nchini India kwa kosa la kuharibu mimea yenye thamani katika bustani .
Kituo cha runinga cha New Delhi kimefahamisha kuwa  uongozi wa jimbo la Uttar Pradesh uliwatupa jela punda hao kwa lengo la kuwaadhibu.
Mlinzi wa gereza la Jalaun  RK Mishra amesema kuwa wanayama hao waliharibu mimea yenye thamani katika bustani hiyo.
Mlinzi huyo aliendelea kusema kuwa mmiliki wa wanyama hao alipewa tahadhari kuhusu wanyama wake.
Wananyama hao waliachwa huru baada ya mwanasiasa mmoja kujitolea kulipa gharama zote zilizosababishwa na wanyama hao.

Monday, November 27, 2017

27 November 2017,Makosa ya usalama barabarani kwa siku 12 yaingiza zaidi ya bilioni mmoja serikalini Jijini Dar es salaam

Makosa ya  usalama barabarani  yaingiza  serikalini Sh bilioni 1.11 kama tozo za makosa mbalimbali ya usalama barabarani kanda maalum ya Dar es salaam  kwa siku 12.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini hapa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Lazaro Mambosasa alisema fedha hizo zimekusanywa kupitia kikosi hicho ikiwa inaendelea na uperesheni ya ukamataji wa makosa ya usalama barabarani.

Alisema jumla ya makosa yaliyokamtwa ni 36,353 huku magari yaliyokamatwa yakiwa 33,444, pikipiki zilizokamatwa ni 795, daladala 12,197, magari mengine binafsi na malori 21,247.

Mambosasa alisema jumla ya waendesha pikipiki 92 walifikishwa mahakamani kwa makosa ya kutovaa kofia ngumu na kupakia abiria zaidi ya mmoja. Aidha Mambosasa amewatangazia wananchi kutumia namba 41.59.7.174/tms kwa simu zao za mikononi zenye uwezo wa intaneti kwa kutumia kitufe cha kuingia kwenye mtandao google Browser kwa maulizo ya faini zilizoandikwa kwa mashine za kielektroniki Traffic Management Systems (TMS).

Vile vile amewaasa madereva kulipa faini ndani ya muda wa siku saba ili kuepukana na usumbufu wa kukamatwa pamoja na ongezeko la tozo za faini.

Katika tukio jingine jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa 140 kwa makosa mbalimbali ya uhalifu pamoja na dawa za kulenya.

Alisema Polisi wamekamata magunia manne ya bangi, kete 147, puli 73, misokoto 55, pamoja na pombe haramu ya gongo ipatayo lita 300 na mitambo sita ya kutengenezea gongo.

27 November 2017,KILIMANJARO:Mmiliki wa shule mbili msingi na sekondari mbaroni kwa shtaka la mauaji ya mwanafunzi

Mmiliki wa Shule ya Msingi na Sekondari ya Scolastica iliyopo mji wa Himo wilayani Moshi, Edward Shayo amefikishwa mahakamani leo Jumatatu kusomewa shitaka la mauaji.

Mmiliki huyo, pamoja na watu wengine wawili wanatarajiwa kusomewa shitaka la mauaji ya mwanafunzi wa shule hiyo, Huphrey Makundi (16) aliyekuwa kidato cha pili.

Shayo ametolewa hospitali ya rufaa ya KCMC alikolazwa na kupelekwa moja kwa moja Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Muda wowote kutoka sasa anatarajiwa kusomewa shtaka hilo pamoja na mlinzi wa shule na mwalimu mmoja ambao tayari nao wapo chumba cha mahabusu cha Mahakama.

Mtoto huyo alitoweka shuleni Novemba 11 na baadaye kubainika ameuawa baada ya maiti yake iliyozikwa kama ya mtu asiyefahamika, kufukuliwa Novemba 17.

Sunday, November 26, 2017

26 November 2017,Wahamiaji haramu 31 wafa maji katika pwani ya Libya baada ya mashua yao kuzama

Wahamiaji haramu 31 wafa maji na wengine 35 waokolewa baada ya mashua yao kuzama katika  pwani ya Libya

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na polisi ya pwani ya Libya ni kwamba wahamiaji haramu 31 wamefariki na wengine 35  wamokolewa baada ya mashua yao kuzama nchini Libya.

Msemaji wa polisi ya kulinda pwani Libya kanali Ayub Qassem amefahamisha Jumamosi kuwa operesheni ya kuwaokowa wahamiaji hao ilifanyika katika eneo la Castelverde Mashariki mwa Tripoli.

Kanali huyo amefahamisha kuwa miongoni mwa watu waliookolewa walikuwemo watoto.

26 November 2017,Rais Magufuli atoa pongezi kwa Jakaya Kikwete juu ya mchango wake wa ujenzi wa hospitali ya Mloganzila

Rais wa Serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa sifa na pongezi kwa rais mstaafu wa awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kufanikisha ujenzi wa hospitali ya Mloganzila.

Rais ametoa pongezi hizo jana wakati akihotubia wananchi waliohudhuria ufunguzi wa Hospitali na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Mloganzila jijini Dar es salaam.

“Wakati ujenzi wa Hospitali hii unaanza mimi nilikuwa naagizwa tu na niliambiwa nikatafute eneo kubwa nikawaza nitalitoa wapi lakini baadae mzee Jakaya akanipigia tena simu akaniambia kuna eneo huko Mloganzila ni la serikali nenda kaangalie na ujenzi uanze haraka, ndio nikaja hapa”, alisema Rais Magufuli.

Rais magufuli aliongeza kuwa “Watu tunapenda sifa lakini hizi sifa sio zangu ni za rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwani mimi nilikuwa naagizwa tu nikiwa waziri wa Ujenzi, ndio maana nimeona niseme wazi kuwa sifa zote zimwendee mzee Kikwete”.

Aidha rais Magufuli aliweka wazi kuwa wakati anakwenda kuona eneo la Mloganzila wala hakukuwa na barabara lakini aliambiwa na rais Kikwete aanze ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara haraka iwezekanvyo na alifanya hivyo sambamba na waziri wa maji amnbaye naye aliagizwa kuanza ujenzi wa miundombinu ya maji.

Rais Magufuli amesisitiza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Mloganzila jijini Dar es salaam ni mpango na jitihada za rais wa awamu ya nne.

26 November 2017,Zamwizi 40 ukweli wa uchaguzi wa Udiwani kata 43 katika halmashauri 19 nchini kujulikana leo

Zamwizi 40 Uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 43 zilizoko kwenye halmashauri 36 za mikoa 19 ya Tanzania Bara unafanyika leo.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), uchaguzi huo unafanyika kutokana na sababu kadhaa, zikiwemo madiwani kufariki dunia, kujiuzulu, kutohudhuria vikao na wengine ushindi wao kutenguliwa na mahakama.

Mkoa wa Arusha unaongoza kwa kuwa na kata nane miongoni mwa hizo ni za madiwani waliojiuzulu kutoka Chadema na kuhamia CCM wakieleza ni kutokana na kumuunga mkono Rais John Magufuli.

Uchaguzi huu ni wa pili tangu kuanza mwaka huu. NEC katika taarifa yake imesema inatakiwa kufanya uchaguzi wa madiwani mara mbili kwa mwaka kwa mujibu wa sheria.

Uchaguzi mdogo mwingine wa ubunge na udiwani ulifanyika Januari 22 mwaka huu.

Ratiba ya mchakato wa uchaguzi huo ilianza Oktoba 26 kwa vyama vya siasa kufanya uteuzi wa wagombea wa udiwani na kampeni zilianza Oktoba 27 na kuhitimishwa jana.

NEC katika taarifa kwa vyombo vya habari jana imevitaka vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi kuhakikisha unafanyika kwa amani na utulivu na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage alisema wapiga kura wapatao 333,309 wanatarajiwa kupiga kura katika vituo 884 ambako walijiandikishia kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2015.

Alisema tofauti na chaguzi zilizopita, NEC kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa kifungu cha 62 imewaruhusu wapiga kura ambao ama kadi zao za kupigia kura zimepotea, kuchakaa au kufutika kutumia vitambulisho mbadala kwenda katika vituo walivyojiandikisha ili waweze kupiga kura katika uchaguzi huu.

Jaji Kaijage alisisitiza ili kuruhusiwa kutumia kitambulisho mbadala, sharti majina ya mpiga kura yafanane kwa herufi na majina yaliyoko katika kitambulisho mbadala ambayo yako katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Vitambulisho mbadala ambavyo NEC imeruhusu vitumiwe na wapiga kura ni leseni ya udereva, kitambulisho cha uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na pasi ya kusafiria.

Pia, aliwataka wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kutoa kipaumbele kwa makundi maalumu wakati wa kupiga kura, ambayo ni ya walemavu, wajawazito, wenye watoto wachanga, wazee na wagonjwa.

Saturday, November 25, 2017

25 November 2017,Serikali ya Rwanda kupokea dola 5000 kwa kila kichwa kuwahifadhi wakimbizi kutoka Israel

Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo asema kuwa serikali inapanga kuwachukuwa wahamiaji 10 000 wanaoomba hifadhi nchini Israel.

Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Louis Mushikiwabo amesema kuwa Rwanda itawachukuwa wahamiaji wapatao 10 000 kutoka katika mataifa tofauti wanaoomba hifadhi nchini Israel.

Wizara ya mambo ya nje ya Rwanda imethibitisha kuwa serikali ya Rwanda na ile ya Israel zipo katika mazungumzo ili kukubaliana masharti kuhusu wahamiaji hao watakaopoklewa nchini Rwanda.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amefahamisha Jumapili kuwa itawafukuza wahamiaji wapatao 40 000 na kufunga kituo kilichokuwa kikiwazuia wahamiaji Kusini mwa Negev.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na jarida la Haaretz la Israel, serikali ya Israel itatoa kiwango cha dola 5000 kwa Rwanda kwa kila muhamiaji mmoja iwapo Rwanda itakubali kuwapokea.

Wengi miongoni mwa wahamiaji walioko nchini Israel ni raia kutoka Sudan na Eritrea.

25 November 2017,Waziri Mkuu TANESCO iwafuate wananchi walioko vijijini

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) liwafuate wananchi walioko katika vijiji vinavyotarajiwa kuunganishiwa umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na ) kuwahudumia.

Majaliwa amesema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa michezo Tunduru, ambapo aliwasisitiza watumishi wa TANESCO kutokaa maofisini na badala yake wakawahudumie wananchi katika vijiji vyao.

25 November 2017,Lipumba aongea haya baada ya uteuzi wa Slaa

Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amezungumzia uteuzi wa Dk Wilbroad Slaa kuwa balozi akisema hakutarajia.

Rais John Magufuli juzi alimteua Dk Slaa aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Chadema kabla ya kukihama chama hicho wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Wakati wa mchakato wa uchaguzi huo, Profesa Lipumba na Dk Slaa ambao vyama vyao vilikuwa katika umoja uliojulikana Ukawa, walijiondoa baada ya Chadema kumpitisha Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa urais.

Akizungumza jana, Profesa Lipumba alisema, “Imekuwa kama surprise, sikutegemea kama Dk Slaa atateuliwa kwa sababu muda mwingi yupo Canada.”

Hata hivyo, Profesa Lipumba alisema hana shaka na uteuzi huo kwa kuwa Dk Slaa ni mzoefu wa siasa na mzalendo ambaye ataitumikia vyema nafasi hiyo mpya.

“Narudia, sikutegemea. Ila popote atakapopangiwa kazi Dk Slaa atafanya kwa sababu najua ni mchapakazi,” alisema.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema Rais Magufuli ana mamlaka kisheria ya kumteua mtu atakayemuona anafaa katika nafasi fulani.

“Huu ni uamuzi wa Rais sisi wengine hatuna comments zaidi ya kuwatakia kila heri katika utendaji wao wa kazi,” alisema Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai mkoa wa Kilimanjaro.

Akizungumza uteuzi huo wa Dk Slaa, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari alisema Rais Magufuli amemuonea huruma Dk Slaa ndiyo maana akaamua kumpa nafasi ya ubalozi.
Profesa Safari alisema hawezi kumsema vibaya Dk Slaa lakini nafasi hiyo ni huruma na zawadi ya Rais Magufuli.

Amedai Dk Slaa alijaribu kuivuruga Chadema wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2015 lakini hakufanikiwa.

“ Hii ni huruma. Siku zilizopita Dk Slaa aliandikwa katika vyombo vya habari kuwa anafanya kazi Super Market. Mimi nimekaa Ulaya najua maisha ya kule na Dk Slaa ni rafiki yangu sana lakini kwa kitendo alichokifanya mwaka juzi, haya ndiyo matokeo yake,” alisema Profesa Safari.

Kwa upande wake, aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Urusi kuanzia mwaka 2002 hadi 2008, Patrick Chokala alimpongeza Rais Magufuli kwa kumteua Dk Slaa kuwa balozi.

“Sina shaka hata kidogo na Dk Slaa ana uwezo wa kufanya kazi nchi yoyote. Hii kazi anaiweza na ni mtu mwenye dhamira ya kweli,” alisema Balozi Chokala.

Alisema anamfahamu Dk Slaa kwa kipindi kirefu tangu akiwa padre na kwamba, amekuwa ni mchapakazi hodari na mwenye hekima kwa watu.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Azam TV, Dk Slaa alimshukuru Rais Magufuli kwa kumteua ili aungane naye kujenga nchi na hivyo atafanya kazi kwa uwezo wake wote.

Dk Slaa ambaye hivi sasa anaishi Canada alisema, “Ni mapenzi ya Mungu, nashukuru kwa uteuzi.

Ninachoweza kusema katika hatua hii, huu ni wajibu mkubwa kwenye kipindi cha kulijenga Taifa letu.”

Admit Mwananchi

Friday, November 24, 2017

24 November 2017,Tetesi za soka Ulaya michezoni leo Ijumaa

Kiungo wa kati wa Arsenal Mesut Ozil anaitaka Barcelona kumlipa dola 370,000 kwa wiki ili kujiunga nao mwezi Januari.Mkufunzi wa Gunners yuko tayari kumwachilia mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 ili asijiunge na Man United wakati mkataba wake utakapokamilika mwishoni mwa msimu ujao. (AS)

Paris St-Germain imeanzisha mazungumzo na kiungo wa kati wa Manchester United Marouane Fellaini. Kandarasi ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 inakamilika mwishowe wa msimu huu. (Le10Sport - in French)

Liverpool imewasiliana na PSG kuhusu uhamisho wa mkopo wa kiungo wa kati wa Ujerumani Julian Draxler, 24. (L'Equipe via Daily Mail)

Mkufunzi wa zamani wa West Ham Slaven Bilic amekataa mwaliko kutoka kwa West Brom kuzungumzia kuhusu wadhfa ulio wazi wa mkufunzi wa klabu hiyo. (Daily Mail)

Stoke, West Ham, Everton na Southampton wana hamu ya kumsajili mshambuliaji wa Watford Odion Ighalo. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 alielekea katika klabu ya ligi ya Superleague nchini China Changchun Yatai mwezi Januari. (Tutto Udinese, via Stoke Sentinel)

Kiungo wa kati wa Uhispania Juan Mata, 29, anataka kuongeza kandarasi yake katika klabu ya Manchester United na amesema kuwa anaweza kucheza hadi kufika miaka 40.. (ESPN)

Mshambuliaji wa Ubelgiji Eden Hazard, 26, amesema kuwa atasalia hadi mwisho wa msimu kutathmini hatma yake katika klabu ya Chelsea (Canal+ via Independent)

Watford wana imani kwamba mkufunzi Marco Silva hataki kujiunga na Everton kwa kuwa anatafuta nyumba katia eneo la Hertfordshire. (Daily Mirror)

Everton inaonekana kuvunjika moyo katika kujaribu kuwashawishi The Horhets kuwaruhusu kujadiliana na Silva. (Hertfordshire Mercury)

Crystal Palace itashindana na West Ham katika kumsajili kiungo wa kati wa Bournemouth Harry Arter, 27, mnamo mwezi Januari. (Daily Mirror)

Beki wa Uingereza wa zamani Sol Campbel amesema kuwa ana hamu ya kuwa mkufunzi wa timu ya Marekani. (ESPN)

Beki wa Ufaransa Eliaquim Mangala, 26, amekiri kwamba huenda akaondoka Manchester City mnamo mwezi Januari.(Sun)

Winga wa Algeria Riyad Mahrez, 26, hajatoa ishara yoyote kwamba anataka kuondoka Leicester kulingana na mkufunzi Claude Puel. (Leicester Mercury)

24 November 2017,NEC:Kuungua vifaa vya Uchaguzi mdogo wa Udiwani hakuzuii kufanyika kama ulivyopangwa November 26

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)  imesema uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Saranga iliyopo Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam utafanyika Novemba 26,kama ilivyopangwa, licha ya kuteketea kwa moto vifaa vingi vya uchaguzi baada ya jengo la Ofisi ya Kata hiyo kuungua usiku wa kuamkia jana.

Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi (NEC) Hamis Mkunga  amesema hayo leo Novemba 24 baada ya kutembelea eneo la tukio na kueleza kuwa tayari ofisi yake imekwishafanya taratibu nyingine ili kuhakikisha kuwa vifaa vyote vya uchaguzi vilivyoteketea kwa moto vinapatikana na kusisitiza kuwa uchaguzi huo utafanyika kama ilivyopangwa.

“Tumefika hapa baada ya kupata taarifa za kuungua kwa jengo la Ofisi ya Kata ya Saranga ambalo pia tulihifadhi vifaa vya uchaguzi mdogo wa udiwani utakaofanyika Jumapili na bahati mbaya vifaa vingi vya uchaguzi vimeteketea vikiwemo fulana na fomu mbalimbali’’ amesema

Ameongeza kwamba ‘’ Hata hivyo tayari tumefanya utaratibu wa kuhakikisha vifaa hivyo vinapatikana na uchaguzi unafanyika kama ilivyopangwa awali ” amesema Mkunga

Aidha ameeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni hujuma kwani mashuhuda walipofika eneo la tukio walikuta dumu la mafuta ya petroli lakini hawajabaini sababu ya kutokea kwa hujuma hiyo na kuwa vyombo vya ulinzi vinaendelea na uchunguzi zaidi.

Kuhusu hali ya usalama wakati wa uchaguzi Mkunga amesema kuwa tayari vyombo vya usalama Wilaya ya Ubungo vimejulishwa na kuwahakikishia wananchi wa eneo hilo kuwa usalama utaimarishwa na kuwataka wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura.

Mkunga amesema bado hawajaweza kubaini kiwango halisi cha hasara kilichopatikana na kutokana na ajali hiyo na kuwa ofisi yake inaendelea kufanya tathmini juu ya hasara hiyo.

Naye Mkuu wa Idara ya Uchaguzi NEC, Irene Kadushi  amesema kuwa, kata ya Saranga ina vituo vya kupigia kura 139 ambapo vifaa vyote vya uchaguzi awamu ya kwanza na ya pili vilikuwa vimekwishafika na kuwa awamu ya mwisho ya usafirishaji wa vifaa vya uchaguzi katika kata hiyo ilikuwa ni jana asubuhi lakini wamelazimika kuzuia upelekaji wa vifaa hivyo kutokana na tatizo hilo.

Aidha amesema kuwa shughuli zote za uchaguzi ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uchaguzi zimehamishiwa katika Ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa usalama zaidi, na kusisitiza kuwa taratibu nyingine zinaendelea na uchaguzi huo utafanyika kama ulivyopangwa.

24 November 2017,Zimbabwe yaandika historia leo hii Ulimwenguni

Zimbabwe yaandika historia    tangu ulimwengu ulivyouumbwa leo hii Rais mpya wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa ameapa mchana huu na hivyo kuhitimisha miaka 37 ya utawala wa Robert Mugabe aliyetangaza kujiuzulu tangu Jumanne iliyopita.

Mamia ya wananchi wa Zimbabwe wamefurika katika uwanja wa Harare kushuhudia sherehe hizo ambazo pia zimehudhuriwa na marais wa mataifa matatu.

Kelele za vivijo na nderemo zimesikika wakati Mnangagwa akikamilisha kiapo chake.

Mitaani kumekuwa na hali ya shamra shamra za tukio hilo lililokuwa likisubiriwa na wengi.

Thursday, November 23, 2017

23 November 2017,Madiwani wa CHADEMA wasusia kikao cha madiwani

Baadhi ya madiwani wa Chadema katika halmashauri ya Manispaa ya Ilala wamesusia Kikao cha Baraza Madiwani kinachoendelea kwenye ukumbi wa mikutano  Ilala jijini Dar es Salaam.

Madiwani hao wamefikia uamuzi huo baada ya Mkurugenzi kushindwa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa katika kikao kilichopita.

Kwa takribani dakika 50 madiwani hao walikuwa kwenye mvutano wengine wakitaka kikao hicho kiahirishwe hadi pale taarifa hiyo itakapowasilishwa.

Wengine walitaka kikao kiendelee kwa kupitia ajenda nyingine na taarifa hiyo ingefanyiwa kazi kikao kijacho.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Msongela Palela ameomba radhi kwa kushindwa kuwasilisha taarifa hiyo na kutaka busara zitumike kwa kuruhusu kikao kiendelee.

Baada ya mvutano wa muda mrefu hatimaye Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni Naibu Meya wa Ilala, Omar Kumbilamoto ameamuru kikao hicho kiendelee ndipo baadhi ya madiwani hao wa Chadema walipoamua kutoka nje.

Hata hivyo Kumbilamoto ameeendeleza kikao hicho kikiwa na wajumbe pungufu.

23 November 2017,Mameneja kampeni Udiwani Kata ya Mhandu jijini Mwanza walipanda tenga

Mgombea udiwani wa Kata ya Mhandu  wilaya ya Nyamagana (Chadema), jijini Mwanza, Godfrey Misana, meneja wake wa kampeni, Charles Chinchibela na wenzao wawili, wamejikuta wakiishia mikononi mwa polisi muda mfupi baada ya kufutiwa kesi ya kujeruhi.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza leo Alhamisi Novemba 23,2017 iliwafutia kesi washtakiwa na baadaye walikamatwa na polisi.

Mbali ya Misana na Chinchibela, wengine katika shauri hilo ni Dominick Izengo na Ibeneza Mathew.

Hata hivyo, Mathew hakuhudhuria mahakamani kutokana na taarifa zilizowasilishwa na mdhamini wake, William Victor kuwa anaumwa.

Mdhamini huyo ameshikiliwa na polisi kwa kushindwa kuhakikisha mshtakiwa anahudhuria mahakamani.

Awali, Hakimu Mkazi, Ainawe Moshi aliwaachia huru washtakiwa katika shauri namba 540/2017 la kumjeruhi meneja kampeni wa CCM katika kata hiyo, Thomas Warioba iliyokuwa ikiwakabili.

Hakimu ametoa uamuzi huo baada ya upande wa Jamhuri kupitia wakili Castus Ndamugoba kuwasilisha ombi la kuondoa shauri hilo mahakamani.

Wakili Ndamugoba amewasilisha ombi hilo akitumia kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na Marejeo yake ya mwaka 2002 inayotoa fursa kwa upande wa Jamhuri kuondoa shauri mahakamani wakati wowote lakini hakizuii washtakiwa kukamatwa tena.

Washtakiwa walikuwa wakidaiwa kumshambulia Warioba katika tukio lililotokea Novemba 14,2017.

Polisi waliowakamata washtakiwa wamekataa kusema lolote kwa maelezo kuwa wao si wasemaji.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Faustine Shilogile  hajapatikana kuzungumzia suala hilo baada ya waandishi wa Mwananchi waliofika ofisini kwake kuelezwa kuwa yuko kwenye kikao.


Admit  Mwananchi

Wednesday, November 22, 2017

22 November 2017,Korea Kaskazini yapiga marufuku mziki na pombe nchini humo

Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amepiga marufuku mashirika ya burudani yakiwemo yale ya pombe na muziki.

Kwa mujibu wa habari,Korea Kaskazini imefanya hivyo kwa nia ya kudhibiti uchumi wa nchi hiyo hasa baada ya vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa mataifa,
Korea Kaskazini imewekewa vikwazo vingi kutokana na kukiuka masharti na kuendelea kutengeneza makombora ya nyuklia.

Wananchi nchini humo wamekuwa wakijaribu kuishi ndani ya matakwa ya serikali.

Mbali na kuwa vigumu kwa wananchi wa Korea Kaskazini kusafiri nje ya nchi,utumiaji wa mitandao ya kijamii bila idhini ya serikali nao umedhibitiwa vilivyo.

Hata hivyo Pyongyang haionyeshi dalili zozote za kaucha kufanya majaribio ya makombora ya nyuklia.

22 November 2017,Wakulima wa zao la Pamba Mwanza,Tabora,shinyanga,Kigoma na Singida wapatiwa zaidi ya tani 25,000 za mbegu

MSIMU mpya wa kilimo cha pamba 2017/18 katika Kanda ya Magharibi inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Geita, Tabora, Mara, Kagera, Singida, Kigoma na Katavi, umezinduliwa rasmi kwa upandaji pamba utakaoendelea hadi mwishoni mwa mwezi ujao.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika katika kijiji cha Mwamashimba wilayani hapa jana, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Marco Mtunga alisema katika msimu wa kilimo wa 2017/18 jumla ya tani 25,000 za mbegu zimetengwa, zikijumuisha tani 11,548 za mbegu mpya ya UKM08 na tani 13,452 za mbegu ya UK91.

Alisema kiasi hicho cha mbegu kinawahakikishia wakulima uwepo wa mbegu za kutosha kwa maeneo yote yatakayozalisha pamba kwa msimu huu wa kilimo na kuongeza kuwa hadi Novemba 12, mwaka huu, jumla ya tani 11,056 ambayo ni sawa na asilimia 70 ya mbegu zote zilikuwa zimesambazwa katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni kati ya tani 15,694 zilizopangwa kusambazwa katika mgao wa awali.

Aliongeza usambazaji wa mbegu ulianza Septemba 15, mwaka huu na ukitarajiwa kukamilika Novemba 30, mwaka huu, ambapo jumla ya ekari 1,300,000 zinatarajiwa kupandwa katika msimu wa kilimo kwa mwaka huu.

Mtunga alisema serikali kwa kushirikiana na wadau imefanikiwa kufufua mfumo wa kuzalisha mbegu bora za kupanda na kwamba azma yake ya kuwapatia wakulima mbegu bora mpya ya UKM08 ifikapo mwaka 2018/2019 itatekelezwa kama ilivyopangwa.

Alisema mfumo wa uzalishaji wa mbegu bora za pamba unaanzia Kituo cha Utafiti cha Ukiriguru ambapo mbegu mama huzalishwa na baada ya kupatikana zinapelekwa kupandwa katika shamba la Nkanziga lililopo wilayani Misungwi mkoani Mwanza kwa lengo la kuzalisha mbegu za awali.

22 November 2017,Mbowe CHADEMA bado ipo fiti

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema chama hicho hakiwezi kutetereka au kufa kwa kiongozi au mwanachama wake kuondoka.

Kauli hiyo ameitoa leo Jumatano Jijini Dar es salaam  baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa vijana wa chama hicho, Patrobas Katambi kutangaza kujiunga na CCM. "Tuko ‘strong enough’ sio mara ya kwanza watu kuondoka hivyo wanachama wetu wasiogope waendelee kujenga chama na kuendelea na kampeni za udiwani,"

Aidha ameongeza kuwa Chadema ilipofika haiwezi kufa kwani imejijenga na hapo walioondoka lakini mpaka sasa kimeendelea kuwapo.

Pia amesema mwitikio wa wananchi katika kampeni za udiwani kwenye kata 43 umeishtua CCM ikiwamo kuhama kwa aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu.


Admit Mwananchi

Tuesday, November 21, 2017

21 November 2017,NEC yakaa mkao wa kula leo Jijini Dar es salaam

Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) imekutana jijini Dar Es Salaam chini ya Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Rais Dkt. John Magufuli.

Katika mkutano huo baadhi ya wanachama waliokuwa katika vyama mbalimbali vya siasa wamezungumza na kuomba ridhaa ya mkutano huo kujiunga na CCM.

Waliotangaza kujiunga na chama hicho kwenye mkutano huo kutoka ACT WAZALENDO ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Maji Profesa Kitila Mkumbo, Albert Msando, Samson Mwigamba na Edna Sunga.

Lawrence Masha aliyejiondoa hivi karibuni kutoka CHADEMA na Patrobus Katambi aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA - BAVICHA.

Halikadhalika aliyekuwa mwanachama wa CCM, Sophia Simba ameandika barua ya kuomba radhi na kukubaliwa kurejeshwa ndani ya chama hicho.

NEC imewakubali wote walioomba kujiunga na chama hicho.

21 November 2017, Trump asema korea kaskazini inafanya mambo yaliopitwa na wakati

Marekani imelitambua rasmi taifa la Korea Kaskazini kama taifa la kigaidi.

Kwa mujibu wa habari,rais Donald Trump anaamini jambo hilo lilipashwa kufanywa miaka mingi iliyopita.

Hatua hiyo itaongeza vikwazo dhidi ya Pyongyang ambayo bado iko kwenye hatua ya kutengeneza makombora ya nyuklia.

Ripoti zinaonyesha kuwa Korea Kaskazini inajiandaa kuwa na kombora litakaloweza kuiangamiza Marekani.

Kim Jong Un anaonekana kutobabaishwa na vikwazo vinavyozidi kuongezwa dhidi ya nchi yake.

21 November 2017, Aliyekuwa mwenyekiti wa BAVICHA afunguka haya mbele ya Rais Magufuli

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi ambaye amehamia CCM amesema kama ataitwa msaliti basi atakuwa kundi la wasaliti wa nchi hii.

Akizungumza leo Jumanne Jijini Dar es salaan mbele ya Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli kwenye Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Katambi amesema, “mambo mengi yalikuwa mrama  na watu tunapenda mabadiliko ila hatutaki kubadilika.”

"Kama nitaitwa msaliti basi nitakuwa msaliti kundi la wasaliti wa nchi hii, ukombozi ulishapatikana, siyo tunachokisema majukwaani ndiyo tunachokiishi,"

"Maisha tunayoyahubiri siyo tunayoishi, ukienda jimboni kwake, vijana kama nguvu kazi ya Taifa, tunajadili ‘personalities’ badala ya ‘issues’ mawazo mbadala," amesema.

"Niwaombe nijiunge na CCM siyo kwa sababu za madaraka ila tuijenge, CCM inatoa nafasi kwa vijana, vijana kwa upinzani ni sawa na karai katika ujenzi.”

Katika kikao hicho Rais Magufuli amesema karibu wanachama 200 wameomba kujiunga na chama hicho.

Amesema kwa sasa hawatatambulishwa hadi mkutano mwingine.

Monday, November 20, 2017

20 November 2017,Waislam kutoka jamii ya Rohingya nchini Myanmar wazidi kukumbwa na madhila

Wabunge nchini Marekani katika mkutano wao na Jeff Merkley wasema kuwa madhila yanayowakumbwa waislamu kutoka jamii ya Rohingya nchini Myanmar ni uhalifu wa kivita.

Taarifa hiyo ilitolewa na msemaji wa waziri mkuu wa Bangladesh Ihsan Karim.

Tume ya wabunhe wa Marekanş imefahamisha Jumapili kuwa Myanmar imetenda uhalifu wa kivita dhidi ya jamii ya Rohingya.

Seneta Jeff Merkley na wiziri mkuu wa Bangladesh  katika mkutano wao mjini Dhaka walitoa taarifa kuwa madhila yanayowakabila Rohingya ni uhalifu wa kivita.

Kabla ya kuonana na waziri mkuu wa Bangladesh , tume ya wabunge hao kutoka Marekani ilitembelea kambi ya wakimbizi wa jamii ya Rohingya Balushali katika mpaka wa Cox Bazar.

20 November 2017,Serikali yawataka viongozi wake kuzingatia mpango wa bajeti

Serikali imewaagiza watendaji wakuu na viongozi wote Serikalini kuzingatia kikamilifu mwongozo wa maandalizi ya mpango wa bajeti ya mwaka 2018/2019 ili uweze kuleta tija na kuendeleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Agizo hilo limetolewa na Waziri Mkuu, mjini Dodoma, ambapo amewataka watendaji hao ambao ndio maafisa katika taasisi zao wahakikishe wanazingatia mambo yote muhimu yaliyoainishwa kwenye mwongozo ili kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa mpango wa bajeti.

Amesema kuwa miongoni mwa mambo ya kuzingatia ni ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo aliwataka maafisa masuuli kuhakikisha makusanyo yote yanawekwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali.

“Maafisa masuuli waendelee kupunguza matumizi ya Serikali kwa kufanya tathmini ya uendeshaji wa taasisi zao ili kuchukua hatua stahiki na kuhakikisha taasisi zinazojiendesha kibiashara zinapata faida na kuacha kutegemea ruzuku kutoka Serikali kuu,” amesema Majaliwa.

Aidha,katika kudhibiti matumizi na kupunguza gharama, amewataka waendelee kufanya uhakiki wa watumishi ili mishahara ilipwe kwa watumishi wanaostahili na wanaopaswa kupandishwa madaraja wahakikiwe na malimbikizo yote ya madeni yabainishwe ili yaweze kulipwa.

Hata hivyo, ameongeza kuwa maafisa masuuli hao wanatakiwa kuhakikisha madai ya watoa huduma wote yanahakikiwa na mkaguzi mkuu wa ndani wa hesabu za Serikali na kuingizwa kwenye hesabu za fungu husika.

20 November 2017, CCM yawateua hawa wenyeviti wa wilaya sita kichama

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimefanya uteuzi wa majina ya wagombea wa uenyekiti wa wilaya sita za kichama.

Wilaya hizo ni Moshi Mjini, Hai, Siha, Makete, Musoma Mjini na Musoma Vijijini.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na CCM leo Jumatatu Novemba 20,2017 imesema Kamati Kuu ya chama hicho kwa niaba ya Halmashauri Kuu imeteua majina ya wagombea katika wilaya ya Hai ambayo ni ya Abdulah Mriri, Magai Maganda na Justice Masawe.

Kwa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro walioteuliwa ni Justice Mkita, Wilfred Mossi na Humfrey Nnko, huku Wilaya ya Moshi Mjini wateule ni Absalom Mwakyoma, Joseph Mtui, Faraji Swai na Alhaji Omar Amin Shamba.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole imesema kwa Wilaya ya Makete wateule ni Aida Chengula, Mwawite Njajilo na Onna Nkwama; Wilaya ya Musoma Mjini ni Robert Sylvester, Magiri Maregesi, Amina Nyamgambwa na Daud Misango.

CCM imesema wateule wa Musoma Vijijini ni Gerald Kasonyi, Kananda Hamisi Kananda na Nyabukika Bwire Nyabukika.

Polepole katika taarifa hiyo amesema Kamati Kuu imeagiza mikutano mikuu ya uchaguzi ya wilaya za Makete, Musoma Vijijini na Musoma Mjini ifanyike Novemba 25 na 26,2017.

Kwa wilaya za Moshi Mjini, Hai na Siha mikutano hiyo itafanyika Desemba Mosi na 2, 2017.

20 November 2017,Upimaji Afya bure wazua sintofahamu Jijini Dar es salaam

Wakazi wa Dar es salaam wanufaika na huduma ya upimaji  Afya bure  unaofanywa na madaktari kutoka China katika Bandari ya Dar es Salaam na wakiadhika na msongamano wa magari  unaotokana na zoezi hilo.

Upimaji wa afya unafanyika kwenye meli iliyotia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam.

Katika Barabara ya Kilwa, magari yanayoelekea Posta na Gerezani yamekuwa yakitembea mwendo wa taratibu na kusimama kwa takriban kwa dakika 20 kabla ya kusogea.

Kondakta wa daladala linalofanya safari kati ya Mbagala Rangi Tatu na Stesheni, Yasin Yusuph amesema leo Jumatatu Novemba 20 kuwa wametumia zaidi ya saa mbili kwa safari.

"Sisi tumetoka Mbagala saa 1:30 hadi sasa saa 3:40 hatujafika na mwendo ni huuhuu unaouona wa taratibu. Magari yakishasimama unasahau.

Tatizo ni kuwa hakuna utaratibu maalumu, watu wamejaa kila sehemu na wanaruhusu magari njia mbili," amesema Yusuph.

Amesema ni vyema lingetafutwa eneo kubwa ambalo watu wanaweza kukaa na kusubiri huduma badala ya kusimamishwa pembezoni mwa barabara.

"Watu ni wengi, eneo la kupumzika hakuna. Hapa hakuna miti ya kutosha jua likiwa kali litawachoma," amesema.

Sunday, November 19, 2017

19 November 2017, Yanga yaiadhibu vibaya Mbeya city huku ikitoa hat-trick moja katika mchezo huo

Yanga yaiadhibu  Mbeya city ,huku staika wake  Mzambia Obrey Chirwa ameendelea 'kung'ara' katika Ligi Kuu Bara baada ya kufunga 'Hat -trick' yake ya kwanza msimu huu kwenye ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Mbeya City, leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Chirwa, ambaye ni Mchezaji Bora wa Kigi Kuu kwa mwezi Oktoba, alifunga mabao hayo dakika ya 19, 49 na 59, wakati Emmanuel Martine alifunga mawili dakika ya 22 na 80 na kufanya matokeo kuwa 5-0.

Hiyo ni Hat-trick ya kwanza kwa Chirwa tangu aliposajiliwa na Yanga msimu uliopita na hat-trick ya pili msimu huu, ya kwanza ikifungwa na Emmanuel Okwi wa Simba.

Katika mchezo huo uliochezwa uwanjani hapo, Yanga walicheza kwa umakini na kupata matokeo hayo yanayowabakisha nafasi ya tatu na pointi 21, nyumba ya Simba inayoongoza na pointi 22 ambazo ni sawa na za Azam wanaoshika nafasi ya tatu.

Matokeo ya mechi nyingine, Azam imewatambia Njombe Mji kwao baada ya kuwachapa bao 1-0, lililopachikwa na Aggrey Morris.
Wakata miwa wa Mtibwa Sugar, wameshindwa kutamba kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Manungu, Morogoro, wakichapwa kwa bao 1-0 na Kagera Sugar, lililofungwa na Edward Christopher katika dakika 85.

19 November 2017,Wagonjwa watajwa kuwa njia ya kuingiza dawa za kulevya nchini

Wabunge wametaja njia zinazotumika kuingizwa dawa za kulevya nchini na kusafi rishwa nje ya nchi, ikiwemo wagonjwa kubebeshwa dawa hizo na kupita katika viwanja vya ndege.

Sambamba na hilo, imeelezwa kuwa dawa hizo pia huingizwa nchini kupitia viwanja vya ndege ‘bubu’ , bandari bubu na uwanja wa ndege sehemu ya watu mashuhuri.

Wabunge walibainisha njia hizo jana wakati wakichangia Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wa mwaka 2017 ambao uliwasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama.

Marekebisho ya muswada huo yalipitishwa. Mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbarouk (CUF) alisema sasa hivi wagonjwa wanabebwa kwenye baiskeli maalumu za wagonjwa huku wakisindikizwa na ndugu zao wenye mizigo na wanapofika sehemu ya kukaguliwa wanaelezwa lifti imeharibika na kupitishwa eneo lisilokuwa na ukaguzi.

Alisema mgonjwa huyo na waliomsindikiza wanakuwa wamebebeshwa dawa za kulevya na kuingiza nchini ama kusafirishwa nje.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Lulida (CUF) alisema Tanzania ina viwanja vya ndege 58 na kati ya hivyo tisa pekee ndivyo vilivyo na maofisa wa serikali huku vilivyobaki vipo kwenye mbuga na maeneo mengine ya siri kama ukanda wa pwani ambapo hutumika kuingiza dawa za kulevya nchini.

“Wanaoingiza dawa za kulevya wanapitishwa kule VIP (sehemu ya watu mashuhuri), pale uwanja wa ndege Dar es Salaam (JNIA) watu wachovu tu wanapita pale bila kukaguliwa lakini sisi kwenye nchi za nje hatuthaminiwi hata kupita VIP zao, bandari bubu zinaingiza dawa za kulevya na ukanda wa Pwani ndiyo umeathirika zaidi,” alisema.

Kwa upande wake Mbunge wa Mjimkongwe, Ally Saleh (CUF) aliitaka serikali kufuatilia uuzaji wa dawa za kulevya kupitia mitandao ya kijamii kwani kwa sasa mitandao hiyo inatumika kwenye biashara ya kuuza ngono ambapo mtu anaelekezwa wapi atapata huduma hizo.

Alitaka sheria isiangalie kuadhibu zaidi wanaotumia dawa za kulevya kwani wanapokuwa gerezani wanapata maradhi kama virusi vya Ukimwi hivyo akashauri ni vema kutiwa mkazo kuwapatia elimu watumiaji wa dawa hizo.

Naye Mbunge wa Muheza, Adadi Rajabu (CCM) alisema makosa ya kukutwa na bangi na mirungi kilo 50 na adhabu yake ya kifungo cha maisha ni adhabu kubwa kwani kiwango hicho ni kidogo, hivyo kitasababisha watu wengi kufungwa na kuleta msongamano magerezani.

Akijibu hoja za wabunge; Waziri Mhagama alisema ameiagiza Mamlaka za Kupambana na Dawa za Kulevya za Zanzibar na Tanzania Bara kukutana kupanga mikakati ya kupambana na vita hiyo ya dawa hizo.

“Adhabu ikiwa kubwa ndiyo vizuri itafanya biashara iwe ghali na hiyo itasaidia kuokoa Watanzania wengi na tunaamini sheria hii itapunguza matumizi na biashara hii,” alisema.

Alisema serikali itafungua vituo vya tiba ya methadone kwa watumiaji wa dawa za kulevya katika mikoa ya Dodoma, Mbeya na Mwanza.Kwa sasa kuna vituo vitatu na vyote vipo mkoani Dar es Salaam.

Alisema serikali inanunua kilo moja ya methadone kati ya dola za Marekani 650 na 1,500 na sasa imeanza kununua nchini India.

“Mwaka 2016 tulinunua kilo 120 za methadone kwa dola za Marekani 180,000 na mwaka huu tumenunua kilo 300 kwa dola za Marekani 450,000,” alisema

19 November 2017,Mkuu wa mkoa apinga bomoa bomoa

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amepiga marufuku uamuzi wa kubomolewa nyumba 300 za mtaa wa Maisaka mjini Babati, uliotolewa na Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya mji huo.

Pia, Mnyeti ametishia kulifungia shughuli zake baraza la madiwani wa halmashauri ya mji huo kutokana na kutoa uamuzi ambao hauna maslahi kwa jamii.

Akizungumza leo na Novemba 19 na wananchi wa mtaa wa Maisaka, amesema hakubaliani na sababu za kuvunja nyumba hizo za wananchi wa Maisaka zilizotolewa na mkurugenzi wa mji huo Fortunatus Fwema.

Amesema maamuzi hayo mabovu yanasababisha wananchi waichukie serikali yao, ila yeye akiwa mkuu wa mkoa huo hatakubaliana na kitendo hicho.

"Siwezi kukubaliana na maamuzi ya kipuuzi yanayotolewa na madiwani kwa lengo la kuwagombanisha wananchi na serikali yao," amesema Mnyeti na kuongeza.

"Mnataka kubomoa nyumba za watu wanyonge kisha mnasimama majukwaani na kusema eti haya ni maelekezo ya Rais wenu ameagiza mbomolewe nyumba zenu na kusababisha wananchi waichukie serikali."

Amesema anasitisha zoezi hilo kwani yeye hakubaliani na sababu zilizotolewa na Fwema na kusababisha nyumba hizo ziwekwe alama ya X na kutaka kubomolewa.

Amesema sababu zilizotolewa za ujenzi holela kwenye eneo hilo hakubaliani nazo kutokana na watumishi wa halmashauri hiyo nao wamechangia kwani walipaswa kuchukua hatua tangu awali kwenye msingi kabla ya wananchi hao hawajajenga.

"Watu wanajenga nyumba wewe mkurugenzi na watumishi wa ardhi mlikuwa wapi, hii tabia ya kujifungia chumbani na kufanya maamuzi ya kuumiza watu, naipiga marufuku," amesema Mnyeti.

Amesema pia, atafuatilia baadhi ya maamuzi ya vikao vya baraza la madiwani ambayo yamekuwa yakiumiza wananchi wa Babati kwa kufanya mzaha na maisha ya watu.

Awali, Mkurugenzi wa mji huo Fortunatus Fwema alisema vikao vitatu halali viliridhia nyumba hizo kuwekewa alama ya X na kutaka kubomolewa.

Fwema alitoa sababu ya kubomolewa ni ujenzi holela kwani wananchi hao walijenga bila kupata vibali kutoka halmashauri ya mji huo.

Amesema uamuzi huo ulipitishwa kwenye vikao vya baraza la madiwani, kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.

Mmoja kati ya wananchi wa mtaa wa Maisaka, Hassan Juma ambaye nyumba yake iliwekewa alama ya X alitoa shukrani kwa mkuu huyo wa mkoa aliyepiga marufuku nyumba zao kubomolewa.

Juma amesema  japokuwa madiwani wa halmashauri hiyo ndiyo viongozi wao waliowachagua kwa kuwapa kura, lakini wameshindwa kuwatetea hivyo kuwashangaza kwa kukubali nyumba zao kuvunjwa.

Mkazi mwingine Mary Ombay amesema yeye na familia yake walishikwa na sintofahamu ya mustakabali wa maisha yao baada ya nyumba yao kuwekewa alama ya X.

"Sisi tulijinyima kwa muda mrefu ili tuweze kujenga nyumba yetu lakini mwisho wa siku inawekewa alama ya X kwa ajili ya kubomolewa, tunamshukuru mkuu wa mkoa kwa uamuzi wake wa kusitisha zoezi hilo," amesema Ombay.

Saturday, November 18, 2017

18 November 2017,Matokeo ya EPL michezoni leo jumamosi

Arsenal ilifunga mabao mawili ya kipindi cha kwanza na kuwalaza wapinzani wao wa jadi mjini London Tottenham kwa mara ya kwanza katika mechi saba za ligi ya Uingereza.

Beki Shkrodan Mustafi alifunga kichwa kizuri kutoka kwa krosi iliopigwa na Mesut Ozil , lakini Spurs wanadai kwamba mpira wa adhabu uliopigwa baada ya Davinson kumchezea visivyo Alexis Sanchez ulikuwa uamuzi mkali.
The Gunners waliongeza bao la pili dakika tano baadaye , baada ya mshambuliaji wa Chile Sanchez kufunga krosi iliopigwa na Alexandre Lacazzette akiwa amekaribia goli.

Sanchez alikuwa na fursa ya kuongeza bao la tatu lakini shambulio lake likapanguliwa na Hugo Lloris.

Fursa nzuri ya wageni hao ilimwangukia kiungo wa kati Christian Eriksen katika kipindi cha kwanza lakini shambulio la kimo cha paka la raia huyo wa Denmark liligonga chuma cha goli huku kipa Petr Cech akiruka na kuokoa kichwa kilichopigwa na Eric Dier.

Ushindi huo sasa umeifanya Arsenal kupanda hadi katika nafasi ya tano katika jedwali la ligi wakiwa na pointi moja juu ya kikosi cha Mauricio Pochettino.

Katika mchezo mwingine Manchester City ilionyesha  uwezo mzuri katika ushindi dhidi ya Leicester ambao umeimarisha uongozi wake katika kilele cha jedwali la ligi ya Uingereza.

Kikosi cha Pep Guradiola kiliendeleza msururu wake wa matokeo mazuri baada ya likizo ya mechi za kimataifa kwa kujipatia ushindi wa 16 mfululizo katika mashindano yote kupitia uongozi wa mshambuliaji wao Gabriel Jesus kabla ya kiungo wa kati De Bryuine kufunga mkwaju mkali ambao kipa wa Leicester alishindwa kuuona.

Wakati huohuo mabingwa watetezi Chelsea walipata ushindi rahisi dhidi ya West Brom na kumuongezea presha kocha wa West Brom Tony Pulis.

Alvaro Morata alifunga bao lake la nane katika ligi baada ya kufunga mpira uliopanguliwa na kipa Ben Foster kufuatia shambulio la Eden Harzard.

Hazard alifunga bao la pili muda mfupi baadaye wakati alipochukua pasi ya kisigino ya Morata, akamchenga Foster na kucheka na wavu kabla ya Marcos Alonzo kufunga bao la tatu kutoka mkwaju wa adhabu wa Cesc Fabregas.

Katika kipindi cha pili Harzard alifunga bao lake la pili kutoka maguu 18 baada ya kupata pasi nzuri kutoka kwa fabregas.

Kwengineko Mohamed Salah aliendeleza umahiri wake kwa kuipatia Liverpool mabao mawili huku timu hiyo ikiilaza Southampton kwa urahisi na kujipatia ushindi wa tatu mfululizo kwa mara ya kwanza 2017.

Baada kuonyesha mchezo mzuri kutoka dakika za kwanza ,mshambuliaji wa Misri Salah alifunga bao zuri kutoka miguu 18 ,baada ya Dusan Tadic kufanya masihara na kupoteza mpira karibu na eneo hatari.

Mshambuliaji huyo aliipatia timu hiyo ya nyumbani bao la pili kufuatia pasi ya Phillipe Coutinho.

Hakuna mchezaji wa ligi ya Uingereza mwenye mabao mengi katika mashindano yote kama Salah msimu huu na ijapokuwa alitulia baada ya kipindi cha kwanza Coutinho alichukua uongozi na kufunga kufuatia mpira uliopanguliwa na kipa baada ya shambulizi la Roberto Firmino.

18 November 2017, Muungano wa upinzani Burundi wapinga kushiriki mazungumzo yajayo ya Arusha

Muungano wa upinzani wa Burundi ulioko uhamishoni umetangaza kuwa, hautashiriki duru ijayo ya mazungumzo ya amani yaliyopangwa kufanyika tarehe 26 mwezi huu wa Novemba hadi tarehe 8 Disemba mwezi ujao huko Arusha kaskazini mwa Tanzania.

Pancrace Cimpaye msemaji wa muungano huo wa CNARED amenukuliwa akisema kuwa, muungano huo hautashiriki katika duru ijayo ya mazungumzo ya amani ya Burundi kwani mpatanishi wa mgogoro huo Benjamin Mkapa amekuwa akiegemea upande wa serikali.

Taarifa ya muungano huo wa upinzani ulioko uhamishoni imekuja siku moja tu baada ya kutangazwa tarehe ya kufanyika duru ijayo ya mazungumzo ya amani ya Burundi.

Tarehe ya kufanyika duru ijayo ya mazungumzo hayo imetangazwa na Benjamin William Mkapa, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni mpatanishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mgogoro wa kisiasa wa Burundi.

Burundi ilitumbukia katika machafuko mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka 2015 baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza, kugombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita kwa mara ya tatu mfululizo, machafuko ambayo yalishika kasi zaidi mjini Bujumbura.

Wapinzani waliitaja hatua ya Rais Nkurunziza kushiriki katika uchaguzi huo kwamba ilikiuka katiba na hati ya makubaliano ya amani ya Arusha lakini serikali ya Bujumbura ilisema haijakiuka sheria.

Hayo yanajiri huku serikali ya Burundi ikiendelea kutuhumiwa na taasisi mbalimbali za kieneo na kimataifa kwamba, imekuwa ikikiuka haki za binadamu na kuwakandamiza wapinzani, tuhuma ambazo zimekuwa zikikanushwa na serikali ya Bujumbura.

18 November 2017,Ubalozi wa Saudia Arabia nchini kwa kushirikiana na (KKCI)wahudumia wagonjwa 33 wa moyo MUHIMBILI

Balozi wa Saudia Arabia nchini, Mohamed bin Mansour Al-Malik amesema Serikali ya Tanzania na Saudia zinaendelea kuimarisha uhusiano wake kupitia ushiriki wa huduma mbalimbali kwa watanzania wasiokuwa na uwezo wa kulipia gharama ikiwamo za mahitaji ya afya.

Balozi Al-Malik ametoa kauli leo Jumamosi(Novemba 18, 2017) jijini Dar es Salaam wakati wa tukio la kufunga huduma ya bure ya upasuaji wa kuzibua mishipa ya moyo iliyoziba kwa kutumia mshipa wa damu wa mkono (Catheterization) iliyotolewa na madaktari watatu kutoka Saudia Arabia.

Huduma hiyo inayotolewa kupitia ushirikiano wa  Madaktari bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete(KKCI) ,tayari imehudumia wagonjwa 33 kati 50 wanaotarajia kufikiwa huduma hiyo.

"Ni jambo la kujivunia katika mahusiano yetu na Tanzania, hii inatafsiri uhusiano unaolenga kuokoa maisha ya watanzania na Saudí Arabia haitaishia hapa, huu ni mwanzo tu, tutajielekeza huduma zetu katika sekta nyingine za kijamii ili kuimarisha uhusiano," amesema Balozi Al-Malik.

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada(IIRO),Ofisi za Tanzania ambao ni wafadhili waliowaleta Madaktari hao, Hassan Ahmed Katungunya amesema gharama za matibabu hayo Kwa mgonjwa mmoja ni wastani wa Sh30milioni.

"Kuhusu gharama za kuwaleta Madaktari hao kwa sasa sina taarifa zake lakini, gharama zote zinasimamiwa na IIRO, "amesema.

Katika tukio hiyo, Balozi Al-Malik alikuwa ameongozana na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar   Zuberi, uwakilishi kutoka Wizara ya Afya pamoja na uongozi wa JKCI.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi amesema fedha nyingi zingetumika kulipia gharama za matibabu hayo endapo huduma hiyo isingetolewa kupitia Madaktari hao.

Profesa Janabi amesema upasuaji uliofanyika ni kuwezesha mgonjwa kutoka chumba cha upasuaji akiwa anatembea.

"Na baada ya saa nane kama hali yake itaendelea vizuri anaweza kuruhusiwa, tofauti na upasuaji wa kutumia mshipa wa paja ambao tulikuwa tunafanya, ilikuwa baada ya upasuaji mgonjwa ni lazima akae hospitali kwa zaidi ya saa 24 kuangalia maendeleo yake, "amesema.

Profesa Janabi amesema mbali na huduma hiyo, kambi hiyo ya Madaktari ilihusika na utoaji elimu na kubadilishana ujuzi wa kazi kati ya wafanyakazi wa taasisi hizo mbili.

"Lakini hata wageni pia wamejifunza vitu vingi na uzoefu mpya wa baadhi ya magonjwa na mambo ya kiteknolojia wasiokuwa nayo kwenye nchi zao, lakini niwaombe wananchi wajenge utamaduni wa Kupima afya zao mara kwa mara,"amesema.

Katika tukio hilo, zawadi na tuzo zilizoandaliwa kwa ajili ya kutambua mchango huo, zimetolewa kwa Wizara ya Afya, JKCI, Madaktari na Uongozi wa IIRO.

18 November 2017,Serikali yatumia bilioni 11.9 kukarabati mabweni ya vyuo kumi vya Ualimu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imetumia Sh11.9 bilioni kukarabati miundombinu ya kufundishia, kujifunzia na mabweni katika vyuo 10 vya ualimu nchini.

Amevitaja vyuo hivyo kuwa ni Morogoro, Mpwapwa, Butimba, Kasulu, Songea, Tukuyu, Marangu, Kleruu, Korogwe na Tabora.

“Ukarabati huu umewezesha wanachuo 5,920 waliokuwa wanasoma Stashahada maalumu ya Sayansi, Hisabati na Tehama katika Chuo Kikuu cha Dodoma -Udom kuhamishiwa katika vyuo hivyo,” amesema.

Waziri Mkuu Majaliwa alitoa kauli hiyo jana Ijumaa, Novemba 17,2017 bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa tisa wa Bunge la 11 ambalo limeahirishwa hadi Januari 30, 2018.

Amesema ili kuongeza fursa za wanafunzi kusomea ualimu, Serikali imepanga kujenga na kukarabati vyuo vya ualimu vya Kitangali, Ndala, Mpuguso na Shinyanga kwa thamani ya Sh36.47 bilioni.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema mradi huo ambao utatekelezwa kwa miaka mitatu kuanzia 2016/17 hadi 2018/19, unalenga kuongeza fursa kwa wanafunzi wenye sifa kupata nafasi ya kujiunga na elimu ya ualimu.

“Ujenzi na ukarabati huu utasaidia kuongeza udahili katika vyuo vya ualimu vya Serikali kutoka wanachuo 20,535 katika mwaka 2017 hadi kufikia wanachuo 23,835 katika mwaka 2019, ikiwa ni ongezeko la wanachuo 3,300,” amesema.

Wakati huohuo, waziri mkuu amesema Serikali imeanza maandalizi ya awamu ya pili ya ukarabati wa vyuo saba vya ualimu vya Serikali.

Amevitaja vyuo hivyo kuwa ni Tandala, Nachingwea, Tarime, Kinampanda, Mandaka, Patandi na Ilonga.

Amesema vyuo vya ualimu vya Murutunguru, Kabanga na Mhonda vitalazimika kujengwa upya baada ya wahandisi kubaini kuwa vyuo hivyo havifai kukarabatiwa kutokana na uchakavu mkubwa wa majengo yake.

Friday, November 17, 2017

17 November 2017,Walimu saba na familia zao wamejikuta wamelala nje,wawili kati yao wamenyolewa nywele wilayani SENGEREMA

Walimu saba wanaofundisha Shule ya Msingi Soswa wilayani Sengerema wamejikuta wamelala nje pamoja na familia zao huku wawili kati yao wakiwa wamenyolewa nywele kichwani na sehemu za siri.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Soswa, Petro Lukas amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamukia leo Jumatano ambapo walimu hao walipokuwa wamelala ndani ya nyumba zao na walipotahamaki usiku walijikuta wamelala nje.

Amesema palipokucha walimu hao walizinduka na kutokuamini kilichotokea na walipoingia ndani ya nyumba zao walikuta damu zimetapakaa vyumbani na sebuleni pia vibuyu vikiwa vimevalishwa shanga nyeupe vikiwa kitandani na chini kitendo kiliwafanya kuhaha kuomba msaada kwa jamii inayowazuguka.

Mwalmu Lukas amesema kati ya walimu hao wawili wameathirika zaidi na tukio hilo na kwa kupata mshituko ambao ni Wape Kisumo aliyenyolewa nywele kichwani pmaoja na Daud Shule ambaye alinyolewa nywele sehemu za siri.

Kutokana na mshtuko huo Kisumo alipelekwa kituo cha afya cha Mwangika kwa matibabu na mwalimu Shule yeye anaendelea na matibabu ya tiba na hali zao zinaendelea vizuri.

Mganga Mkuu Halmashauri ya Buchosa, Dk Ernest Chacha amekiri kumpokea mwalimu Kisumo katika kituo cha afya Mwangika na kwa sasa anaendelea kupatiwa matibabu na baada ya uchunguzi wa kitaalamu kukamilika watatoa taarifa lakini alipofika kituoni alikuwa haongei ila baada ya kupatiwa huduma ya kwanza ameanza kuongea kidogo.

Akizungumzia mkasa huo mwalimu Shule amesema kuwa wao baada ya kupata chakula cha usiku walilala ndani nyumba zao na ilipofika usiku wa manane wakasikia mwalimu mwenzao Wape Kisumo akilia na kulalamika kichwa kinamuuma.

Amesema walipotahamaki walijikuta wakiwa nje watupu na kuona kuwa wamedhalilishwa na kitendo hicho hivyo wanaiomba Serikali iwasaidie kumaliza tatizo hilo.

Mmoja wa wananchi wa Kisiwa cha Soswa, Sumari Diplospa amesema kitendo hicho kinapaswa kukemewa kwa kuwa walimu hao wanasaidia kufundisha watoto wao.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Bulyaheke Musa Mwilomba amesema kuwa tukio hilo ni tatu kutokea  katika shule hiyo ambapo mwaka jana mwezi nne walimu walipondwa mawe nyumba zao wakiwa wamelala.

Pia Mei 5 mwaka huu nyumba za walimu zilipondwa tena mawe na usiku wa kuamkia leo wamejikuta wamelala nje na baadhi yao kunyolewa nywele sehemu za siri kitendo ambacho kinapaswa kukemewa.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Msingi Halmashauri ya Buchosa, Magareth Kapolesya amesema amepata taarifa ya tukio hilo na kusikitishwa na kitendo hicho na wao kama wasimamizi wa elimu watalishughulikia na kupata ufumbuzi juu ya suala hilo kwa kuwa linawanyima raha walimu na kukosa morali ya kufundisha.

 

17 November 2017,Zitto apaza sauti za wakulima wa tumbaku kwa serikali

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ametaka Serikali kununua tumbaku yote ya wakulima iliyoshindikana kununuliwa wilayani URAMBO

Akihutubia wananchi leo Ijumaa katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kijiji cha Kalemela A, Kata ya Muungano wilayani Urambo Zitto ameishangaa Serikali kutumia fedha nyingi kununua ndege aina ya bombardier zinazopakia watu wachache badala ya kuwekeza kwenye kilimo kinachoajiri wananchi wengi.

Zitto amesema katika ziara yake amezunguka vijijini na kushuhudia nyuso za huzuni, huku wananchi wakimwambia tumbaku ya mwaka jana haijauzwa na msimu mpya umeanza.

“Serikali makini ingefanya nini kwenye kadhia hii ya tumbaku? Sisi ACT- Wazalendo tungekuwa madarakani tungenunua tumbaku yote ya ziada ya wakulima kwa kutumia kasma ya fedha za dharura kwenye Fungu la 50 Wizara ya Fedha,” amesema.

Amesema Serikali iliwahimiza wananchi kufanya kazi kwa bidii, lakini baada ya kuzalisha kwa wingi wanaadhibiwa kwa kukosa masoko.

Zitto ameshauri Serikali kutafuta soko kwa mfumo uliosema ni wa G to G (Government to Government) na kuuza tumbaku hiyo na kurejesha fedha hizo kwenye mfuko wa dharura.

Amesema wakati asilimia 65 ya Watanzania wanategemea kilimo kama ajira, kilimo kimekuwa kikishuka na kusababisha wakulima kuendelea kuwa masikini na kukosa chakula.

“Tunazalisha watu zaidi kuliko chakula, ni dhahiri tunaelekea kubaya,” amesema Zitto.
Amesema katika hali hiyo ya kudumaa kwa kilimo bado wakulima wa Tabora hawajafutwa machozi na zao lao la tumbaku wakati ndilo linaloingiza fedha za kigeni kuliko korosho.

“Serikali ipo tayari kutumia Sh1 trilioni kulipia ndege ambazo ni Watanzania asilimia tano wanapanda kuliko kuokoa wakulima 1.4 milioni wa tumbaku nchi nzima kwa Sh150 bilioni tu, tena ikiwa fedha hizo zinarudi ndani ya muda mfupi,” amesema Zitto.

Amewataka wananchi wa kijiji hicho kuchagua mgombea udiwani wa chama hicho ili apambane kuhakikisha tumbaku ya mwaka jana inanunuliwa.

Amesema Ilani ya Uchaguzi ya ACT -Wazalendo ilitangazwa na Taasisi ya Mviwata (Muungano wa vikundi vya wakulima) kuwa ilani bora zaidi kuhusu masuala ya kilimo kuliko ilani za vyama vyote katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kuwa ilipendekeza kuwapo kwa Hifadhi ya Jamii kwa Wakulima.