Muungano wa upinzani wa Burundi ulioko uhamishoni umetangaza kuwa, hautashiriki duru ijayo ya mazungumzo ya amani yaliyopangwa kufanyika tarehe 26 mwezi huu wa Novemba hadi tarehe 8 Disemba mwezi ujao huko Arusha kaskazini mwa Tanzania.
Pancrace Cimpaye msemaji wa muungano huo wa CNARED amenukuliwa akisema kuwa, muungano huo hautashiriki katika duru ijayo ya mazungumzo ya amani ya Burundi kwani mpatanishi wa mgogoro huo Benjamin Mkapa amekuwa akiegemea upande wa serikali.
Taarifa ya muungano huo wa upinzani ulioko uhamishoni imekuja siku moja tu baada ya kutangazwa tarehe ya kufanyika duru ijayo ya mazungumzo ya amani ya Burundi.
Tarehe ya kufanyika duru ijayo ya mazungumzo hayo imetangazwa na Benjamin William Mkapa, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni mpatanishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mgogoro wa kisiasa wa Burundi.
Burundi ilitumbukia katika machafuko mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka 2015 baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza, kugombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita kwa mara ya tatu mfululizo, machafuko ambayo yalishika kasi zaidi mjini Bujumbura.
Wapinzani waliitaja hatua ya Rais Nkurunziza kushiriki katika uchaguzi huo kwamba ilikiuka katiba na hati ya makubaliano ya amani ya Arusha lakini serikali ya Bujumbura ilisema haijakiuka sheria.
Hayo yanajiri huku serikali ya Burundi ikiendelea kutuhumiwa na taasisi mbalimbali za kieneo na kimataifa kwamba, imekuwa ikikiuka haki za binadamu na kuwakandamiza wapinzani, tuhuma ambazo zimekuwa zikikanushwa na serikali ya Bujumbura.
No comments:
Post a Comment