Thursday, December 14, 2017

14 December 2017,Takukuru jino kwa Jino na CCM

Vitendo vya rushwa katika uchaguzi ndani ya CCM na jumuiya zake vimeonekana kukithiri ndani ya chama hicho huku Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ikiwadaka baadhi ya makada kwa tuhuma hizo.

Vitendo hivyo vimejitokeza katika chaguzi ngazi za wilaya, mikoa na Taifa huku viongozi wake wakuu wakikemea na kusema wale watakaobainika kushinda kwa kutoa rushwa wataondolewa na uchaguzi kurudiwa hatua ambayo imechukuliwa juzi katika Jimbo la Singida Kaskazini.

Katika uchaguzi uliomalizika juzi, ngazi ya Jumuiya ya Wazazi uliotanguliwa na Umoja wa Wanawake CCM Tanzania (UWT) na Umoja wa Vijana (UVCCM), Mwenyekiti CCM, Rais John Magufuli alikemea vikali vitendo hivyo vya rushwa.

Akifungua mikutano ya jumuiya hizo ambayo yote ilifanyikia Dodoma, Rais Magufuli alikemea wale wote wanaojihusisha na rushwa na kusisitiza kwamba hawatamfumbia macho yeyote atakayebainika na hata kama atakuwa ameshinda, uchaguzi utarudiwa.

Mwanasiasa mkongwe, Njelu Kasaka akizungumzia rushwa katika chaguzi hizo alisema, “Hiyo ni ishara mbaya kuwa viongozi wanachaguliwa kwa rushwa na jamii imetekwa na vitendo hivyo.

Unapofika wakati wa uchaguzi watu wanaangalia fedha si ubora.”
Kasaka aliyekuwa miongoni mwa wabunge 55 walioasisi Kundi la G55 lililotaka kuundwa Serikali ya Tanganyika mwaka 1993, alisema anachokifanya Rais Magufuli ni kizuri lakini hataweza kukomesha rushwa bali ataidhibiti.

Vitendo vya kujihusisha na rushwa vimemweka matatizoni, mwenyekiti wa UVCCM aliyemaliza muda wake, Sadifa Juma Khamis ambaye amefikishwa mahakamani na kupelekwa rumande mjini Dodoma akituhumiwa kwa rushwa huku matokeo ya kura ya maoni Jimbo la Singida Kaskazini yakifutwa na Haider Gulamali aliyeibuka mshindi akishikiliwa na Takukuru.

Mashtaka yanayomkabili Sadifa ambaye pia ni mbunge wa Donge (CCM) ni kuwahonga wanachama ili wamchague Rashid Mohamed Rashid ambaye alikuwa akiwania nafasi ya makamu mwenyekiti katika uchaguzi wa umoja huo.

Pili, anadaiwa kuwaahidi kuwalipia gharama za usafiri wanachama wa umoja huo kwa kuwasafirisha kutoka Dodoma hadi Kagera kama zawadi ili wamchague Rashid.

Gulamali anashikiliwa na Takukuru mkoani Singida tangu juzi na uchaguzi wa marudio wa kumpata mgombea wa CCM katika jimbo hilo unafanyika leo huku yeye akizuiwa.

Hatima yake itajulikana uchunguzi utakapokamilika huku Sadifa aliyekamatwa siku moja kabla ya uchaguzi wa UVCCM akiendelea kuwa rumande hadi Desemba 19 dhamana yake itakapojulikana.

Uchaguzi wa Singida Kaskazini unafanyika ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Lazaro Nyalandu aliyetimkia Chadema mwezi uliopita.

Akizungumzia vitendo hivyo vya rushwa, Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Benson Bana alisema vyombo vya dola vimeonyesha kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kuwashughulikia wale wote wanaojihusisha na rushwa.

“Ushindi unatakiwa kupatikana kwa haki na tukienda hivi tutafika na hiki kilichofanyika kwa CCM kiwe mfano kwa vyama vingine vya siasa pindi vinapofanya chaguzi, uwazi utawale na kuwachukulia hatua hata kuwaondoa wanaobainika kutoa rushwa,” alisema Profesa Bana.

Sakata la rushwa pia lilimkumba Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo ambaye gari lake lilipekuliwa na Takukuru akiwa visiwani Ukerewehuku baadhi ya makada wengine waking’ang’aniwa kwa tuhuma za kujihusisha na rushwa.

Kitendo hicho kilimkera Diallo ambaye wakati akiwashukuru wajumbe baada ya kumchagua tena Desemba 3 alisema Serikali inapaswa kutoingilia masuala ya uchaguzi katika chama, bali iangalie na kuwaongoza wanapokosea.

“Kuna umuhimu wa kutengeneza kiapo kitakachosaidia Serikali kutoingilia masuala ya uchaguzi, bali waangalie na kutuongoza pale tunapoenda kinyume. Kitendo cha gari langu kusimamishwa na maofisa wa polisi na kuanza kupekuliwa hakijanifurahisha kwani hata mimi najua rushwa ni adui wa haki.”

Makada wa CCM mkoani Morogoro wamekaririwa wakisema wagombea wenye uwezo bado wanatumia fedha kupata nafasi za uongozi.
Katibu wa CCM mkoa huo, Kulwa Milonge amekiri kuwapo malalamiko hayo lakini akasema hakuna waliothibitika kutoa rushwa.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Morogoro, Beutoz Mbwiga alisema amepokea malalamiko hayo na wamewahoji baadhi ya wagombea na wanachama.

Wilayani Musoma, Mara Takukuru ilitangaza kumsaka mmoja wa wagombea wa uenyekiti kwa mahojiano kuhusu tuhuma za rushwa wakati wa uchaguzi huku CCM mkoani humo ikitangaza kuwachukulia hatua za kinidhamu wote watakaobainika.


Admit Mwananchi

No comments: