Waziri wa Ulinzi wa Uholanzi ametangaza kujiuzulu wadhifa wake baada ya ripoti kufichua udhaifu mkubwa wa idara iliyokuwa chini yake wakati wa operesheni ya Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA.
Jeanine Hennis amejiuzulu baada ya Bodi ya Usalama ya nchi hiyo kufichua katika ripoti yake kuwa, mnamo Juni 6, mwaka jana 2016, askari wawili wa nchi hiyo waliokuwa wakihudumu chini ya askari wa kofia buluu wa UN nchini Mali walipoteza maisha baada ya roketi kuwalipukia kwa bahati mbaya, licha ya wizara yake kulihakikishia taifa kuwa ilikuwa mefanya mikakati yote ya kulinda usalama wa askari hao wakiwa kazini sambamba na kuhakikisha wanapata matibabu ya viwango vya juu wanapojeruhiwa.
Kadhalika waziri huyo amesema Jenerali Tom Middendorp, Mkuu wa Majeshi ya Uholanzi atajiuzulu karibuni hivi kutokana na suala hilo.
Uholanzi imekuwa katika harakati ya kuwaondoa askari wake nchini Mali na idadi ya askari hao inatazamiwa kupungua hadi 300 hivi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, wanajeshi watatu wa Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA waliuawa katika mripuko wa bomu uliotokea kaskazini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa wakiwemo wanajeshi wa Ufaransa, ambavyo vimekuwa nchini humo tangu mwaka 2013 vimeshindwa kukomesha machafuko na vitisho vya ugaidi nchini humo.
No comments:
Post a Comment