Burundi imekuwa nchi ya kwanza kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) inayotuhumiwa na viongozi wa Kiafrika kwamba, imekuwa ikiwaandama viongozi wa bara la Afrika tu.
Msemaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC yenye makao yake mjini The Hague Uholanzi amethibitisha kujitoa Burundi katika mahakama hiyo na kueleza kwamba, kujitoa huko kumeanza kutekelezwa rasmi leo Ijumaa ikiwa ni mwaka mmoja tangu nchi hiyo ya Afrika Mashariki ilipomuandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ikimjulisha kuhusu uamuzi wake huo.
Kwa muktadha huo, Burundi inakuwa nchi ya kwanza kujiondoa rasmi katika mkataba wa Rome uliounda mahakama hiyo ya kimataifa ya jinai ICC.
Nchi nyingine ambazo ziko katika mchakato wa kujitoa katika mahakama hiyo ni Afrika Kusini ambayo iliwasilisha barua yake ya kujitoa katika mahakama hiyo Machi mwaka huu na Gambia ambayo iliandika barua Februari mwaka huu pia.
Burundi kama zilivyo Afrika Kusini na Gambia inaituhumu Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kwamba, imekuwa ikiwaandama viongozi wa Afrika tu katika utendaji wake.
Burundi inajitoa rasmi katika mahakama hiyo ya ICC katika hali ambayo, serikali ya Bujumbura imekuwa ikituhumiwa na asasi mbalimbali za kutetea haki za binadamu kwamba, imekuwa ikikiuka haki za bindamu na kuwakandamiza wapinzani.
Zaidi ya watu 700 wameuawa na wengine wanaokadiriwa kufikia laki nne wamekimbilia katika nchi jirani tangu Rais Pierre Nkurunziza alipogombea urais kwa mara ya tatu mfululizo licha ya upinzani mkubwa wa vyama vya upinzani ambavyo vilisema ni kinyume cha katiba na makubaliano ya Arusha Tanzania.
No comments:
Post a Comment