Jana jioni jeshi la polisi nchini Kenya lilikabiliana na magenge ya wafanya fujo katika eneo la Kawangware jijini Nairobi ambapo magenge hayo yalikuwa yanapora maduka na nyumba za raia na kuchoma moto maeneo ya biashara.
Kwa mujibu wa gazeti la kila siku la Daily Nation la nchini Kenya, magenge hayo ambayo yanadaiwa kufanya fujo kulalamikia marudio ya uchaguzi wa rais uliofanyika juzi Alkhamisi, wamewashambulia na kuwajeruhi vibaya raia.
Gazeti hilo limeongeza kuwa, wafanya fujo hao wamekuwa wakifukuzana na polisi tangu siku ya Alkhamisi.
Wakazi wa eneo hilo wamesema kuwa, watu watatu wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika fujo hizo wakiwemo wanafunzi watatu wa Shule ya Msingi ya Ndurarua ambao wanauguza majeraha waliyoyapata kutokana na fujo hizo.
Gazeti hilo limewanukuu watu walioshuhudia wakisema kuwa wameona kundi la takriban vijana 100 wakiingia katika eneo la Kawangware kutokea majimbo ya uchaguzi ya Waithaka na Dagoretti Kusini.
Limeandika: Nyumba na maduka yamevunjwa na mali zilizokuwemo kuporwa huku sauti za risasi zikisikika kila mahali.
Maduka yote ya barabara za 56 na 46 yakiwemo mabucha, hoteli na saluni yamevunjwa.
Hayo yamejiri huko viongozi wa muungano wa NASA wakiwataka wafuasi wao kutofanya fujo na kujiweka mbali na risasi.
Kwa upande wake, tume ya uchaguzi ya Kenya IEBC imesema inafanya jitihada kubwa za kuhakikisha inamaliza haraka zoezi la kuhesabu kura na kutangaza matokeo ambapo ni wazi kwamba mshindi wa uchaguzi huo wa marudio atakuwa ni Rais Uhuru Kenyatta baada ya mpinzani wake mkuu Raila Odinga kuususia.
No comments:
Post a Comment