Friday, October 27, 2017

27 October 2017, Mvua yasababisha uharibifu mkubwa katika mikoa ya Pwani

Mvua kubwa ya vuli ambayo imekuwa ikinyesha katika maeneo mengi pwani ya Tanzania imesababisha mafuriko na uharibifu mkubwa.

Ripoti kutoka Dar es Salaam zinasema kuwa, mvua hizo zimesababisha hasara na madhara makubwa katika mikoa mbalimbali ikiwemo ya Pwani na Dar es Salaam kiasi cha barabara kufungwa, mabasi yaendayo kwa kasi kusimamisha huduma kwa muda, watu wawili kufa na saba kunusurika kusombwa na maji.

Aidha  kwa mara ya kwanza kituo cha kupimia mvua cha Kibaha mkoani Pwani kimetumia saa 24 kupima milimita 177.9 za mvua tangu kilipoanzishwa mwaka 1964, upimaji huo umeanzia juzi saa tatu asubuhi mpaka jana muda huo, hivyo kuweka rekodi.

Jijini Dar es Salaam, kutokana na mvua zilizonyesha katika maeneo mbalimbali kwa siku mbili mfululizo, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kimefunga kwa muda baadhi ya barabara ili kuzuia maafa zaidi yasitokee.

Kutokana na mvua hizo, vijana wawili wanasemekana kupoteza maisha katika maeneo ya Tabata Kimanga na Mbezi Luis kutokana na kusombwa na mafuriko.

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Musilimu alitaja maeneo yaliyofungwa kwa muda kuwa ni Barabara ya Morogoro eneo la Jangwani, Kibaha Mizani na Barabara ya Mwai Kibaki karibu na Daraja la Malecela.

Aidha, kutokana na hilo, wananchi wanaotokea Morogoro kwenda Chalinze hadi Dar es Salaam, jana walishauriwa kutumia Barabara ya Bagamoyo na wanaotumia Barabara ya Mwai Kibaki watumie Barabara ya Coca-Cola kwenda Mwenge.

No comments: