Wednesday, September 20, 2017

20 September 2017,Afrika yaongoza kuwa na watumwa wengi kati ya watumwa Milioni 40 duniani

Uchunguzi mpya uliofanyika kote duniani umeonesha kuwa, watu zaidi ya milioni 40 wanaishi katika utumwa katika maeneo mbalimbali ya dunia hususan barani Afrika.

Ripoti iliyotolewa jana na Shirika la Kazi Duniani (ILO) na taasisi ya Walk Free imesema kuwa, watu wanaokadiriwa kuwa milioni 40.3 wanaume, wanawake na watoto wadogo, walikuwa wahanga wa utumwa mamboleo katika mwaka uliopita wa 2016.

Uchunguzi huo umefanyika katika nchi 48 na kuwahoji watu zaidi ya 71 elfu.

Uchunguzi huo unasema kuwa, karibu watumwa 3 kati ya kila wanne ni wanawake na wasichana, na kwamba milioni 10 miongoni mwao ni watoto .

Imesema kesi nyingi za utumwa mamboleo zimesajiliwa Afrika, Asia na Pacific.

Ripoti ya ILO na Walk Free Foundation imesema kuwa, karibu watu milioni 5 kote duniani walikuwa watumwa wa ngono katika mwaka uliopita wa 2016.

Mwenyekiti wa jumuiya ya Walk Free, Andrew Forrest amesema kuwa ni fedheha na aibu kwa dunia yetu ya sasa kuwa na watumwa mamboleo milioni 40.

Ripoti hiyo pia imesisitiza udharura wa kuimarishwa haki za wafanyakazi, kuboreshwa masuala ya jinsi ya kushughulikia masuala ya wahamiaji na kuchukua hatua za kushughulikia chanzo cha kuwafanya watu kuwa watumwa kutokana na kulemewa na madeni.

No comments: