Shirika la Kazi Duniani (ILO) limeripoti kuwa, zaidi ya watoto milioni 150 wanafanyishwa kazi kwa lazima kote duniani.
Ripoti iliyotolewa na ILO imesema kuwa, karibu nusu ya watoto wanaofanyishwa kazi kwa lazima wanatumika katika kazi zenye hatari kubwa, na zaidi ya thuluthi moja miongoni mwao hawaendi mashuleni.
Mtaalamu wa masuala ya kiufundi anayeshughulikia kazi za kulazimishwa wa shirika la Kazi Duniani mjini Geneva, Houtan Homayounpour amesema makadirio yanaonesha kuwa, watoto milioni 121 wataendelea kufanyishwa kazi za kulazimishwa hadi mwaka 2025 na kwa msingi huo dunia haitaweza kukomesha vitendo vya kuwatumikisha watoto katika kazi za kulazimishwa katika kipindi cha miaka 8 ijayo.
Ripoti mpya zinasema kuwa, watoto milioni 64 wa kike na milioni 88 wa kiume wanafanyishwa kazi za kulazimishwa na kwamba idadi kubwa ya watoto hao iko Afrika, Asia na kanda ya Oceania.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, eneo la Afrika chini ya jangwa na Sahara limeshuhudia ongezeko la idadi ya watoto wadogo wanaofanyishwa kazi za kulazimishwa katika kipindi cha mwaka 2012 hadi 2016.
Wataalamu wanafungamanisha suala hilo na vita, migogoro na maafa ya kimaumbile ambayo yanawafanya watu wengi kukosa kazi, makazi na kuwa wakimbizi.
No comments:
Post a Comment