Serikali ya India imewasilisha ombi katika Mahakama
ya Juu ya nchi hiyo la kutaka kutimuliwa makumi ya maelfu ya wakimbizi
Waislamu wa kabila la Rohingya, waliokimbilia usalama wao nchini humo
kutokana na kushadidi mashambulizi ya jeshi la Myanmar likishirikiana na
Mabudha wenye misimamo mikali dhidi yao.
Hatima ya wakimbizi hao wapatao 40 elfu wanaosemekana kuwasili
nchini humo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita itajulikana leo Jumatatu.
Hoja ya serikali ya India ya kutaka kutimuliwa nchini humo wakimbizi hao raia wa Myanmar ni wanahatarisha usalama wa taifa.
Zeid Raad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa
Mataifa amekosoa vikali hatua ya serikali ya India ya kuwasilisha kesi
mahakamani kutaka wakimbizi hao watimuliwe.
Wakati huo huo, Ram Krishna Subedi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nepal amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema kuwa,
vyombo vya usalama nchini humo vimeimarisha usalama katika maeneo ya
mipakani ili kuzuia wakimbizi wa Rohingya kuingia nchini humo.
Umoja wa Mataifa unasema kuwa zaidi ya Waislamu laki nne wa
jamii ya Rohingya wamelazimishwa kukimbia miji na makazi yao tangu
tarehe 25 mwezi uliopita wa Agosti, baada ya kuanza wimbi jipya la
mashambulizi ya Mabudha wenye misimamo ya kuchupa mipaka
wakishirikiana na jeshi la Myanmar dhidi yao.

No comments:
Post a Comment