Monday, September 11, 2017

11 September 2017, Korea Kaskazini: Tutaizidishia mateso na machungu Marekani

Serikali ya Korea Kaskazini imetangaza kuwa, ikiwa Marekani itaendeleza njama zake ili kuongeza vikwazo dhidi yake katika Umoja wa Mataifa, basi Pyongyang itaizidishia Washington machungu na taabu.

Asubuhi ya leo Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini imetoa taarifa ilifafanua kuwa, ikiwa Marekani itaendeleza uhasama wake dhidi ya Pyongyang, Korea Kaskazini itachukua hatua ambayo kamwe Marekani haijawahi kuifikiria sambamba na kuilazimisha Washington kutii matakwa yake.

Inafaa kuashiria kuwa, Marekani ilikuwa imependekeza kupigigiwa kura ya kupasisha muswada wa azimio ambalo kwa mujibu wake ungeiwekea vikwazo vikali Korea Kaskazini Jumatatu ya leo.

Hadi sasa Umoja wa Mataifa kupitia mashinikizo ya Marekani na washirika wake imeshaiwekea vikwazo nchi hiyo ya Asia kwa duru sita.

Hayo yanajiri katika hali ambayo tarehe nane Agosti mwaka huu, Rais Donald Trump wa Marekani alitishia kuishambulia kijeshi Korea Kaskazini.

Hata hivyo tarehe tatu mwezi huu serikali ya Korea Kaskazini ililifanyia kwa mafanikio bomu lake la nyuklia aina ya Hydrogen lenye uwezo mkubwa wa uharibifu , hatua ambayo imekabiliwa na radiamali hasi na Marekani na washirika wake.

Korea Kaskazini imekuwa ikisisitiza kuwa, inalazimika kumiliki silaha za nyuklia kwa lengo la kujihami kutokana na vitisho vya Marekani vya kuivamia kijeshi nchi hiyo kwa mabomu ya nyuklia.

Marekani imekuwa ikifanya mazoezi ya kijeshi mara kwa mara na Korea Kusini, mazoezi ambayo Korea Kaskazini inayaona kuwa tishio.

No comments: