Friday, April 20, 2018

20 APRIL 2018, SERIKALI YAMTAKA MUWEKEZAJI ALIYEUZIWA KIWANDA CHA NYAMA KINYEMELA KUJITOKEZA


Responsive imageSerikali imepokea hati ya kiwanda cha nyama cha Shinyanga kutoka kwa mwekezaji aliyeuziwa kiwanda hicho kinyemela huku pia ikitoa siku 14 kwa mwekezaji aliyeuza eneo hilo kujitokeza kabla ya kuchukuliwa hatua.

Akizungumza jijini Dar es salaam wakati akishuhudia makabidhiano ya hati hizo,Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesema kurejeshwa kwa hati hiyo ni muhimu kwani serikali itapata wawekezaji sahihi watakaosaidia kukuza sekta ya nyama na kuchangia pato la Taifa.
Baada ya mwekezaji TRIPLE S, kushindwa kuendeleza kiwanda hicho, aliuza kiwanda hicho  kinyume na taratibu  kwa mwekezaji mwingine na kumpatia hati zote, ambazo zimerejeshwa kwa serikali na mwakilishi wa kampuni ya ASB investments iliyouziwa kiwanda hicho.
Aidha kampuni hiyo ya ASB ,imeipongeza serikali ya awamu ya tano kwa hatua inazochukua ili kufanikisha Tanzania ya viwanda na kusema kuwa wako tayari kuendelea kuwekeza Tanzania katika sekta ya viwanda na kilimo.
Baada  ya makabidhiano ya hati hizo,Waziri wa Mifugo  na Uvuvi Luhaga Mpina  ametoa siku 14 kwa mwekezaji TRIPLE S, kujisalimisha kwa serikali kwa ajili ya mahojiano,kabla ya hatua kali hazijachukuliwa dhidi yao na kuipongeza kampuni ya ASB Investments  kwa kujitokeza na kurejesha hati hizo..
Aidha baada ya kurejeshewa kiwanda hicho, Serikali inatarajia kukitangaza kiwanda hicho pamoja na  kiwanda cha nyama cha mbeya, na kiwanda cha ngozi cha mwanza ili kupata wazabuni watakaoviendesha viwanda hivyo na kuleta tija.

No comments: