RIPOTI maalumu ya Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu usalama kwenye barabara nchini Uganda inaonesha kuwa, ajali za pikipiki 'bodaboda' zinaua takribani 10 kila siku jijini Kampala.
Mratibu Mkazi wa UN nchini humo, Rosa Malango amesema, kiwango hicho cha ajali ni kikubwa zaidi Afrika Mashariki na kinaigharimu Uganda shilingi trilioni 4.4 za nchi hiyo kila mwaka.
“Huu utafiti umefanywa muda muafaka.
Usalama barabarani ni changamoto kubwa Uganda lakini haijapewa zito unaostahili.
Kila siku Uganda inapoteza watu 10, idadi kubwa zaidi Afrika Mashariki ikimaanisha tunapoteza watoto na nguvukazi inayokadiriwa kuwa na thamani ya shilingi trilioni 4.4 ambazo ni asilimia tano ya pato ghafi la taifa (GDP)” amesema Malango.
Waziri wa Nchi wa Usafirishaji, Aggrey Bagiire ameipokea ripoti hiyo na kuomba UN kufanya utafiti kuhusu sababu za kutokea ajali nyingi kwenye barabara za Uganda.
“Nilipojiunga kwenye hii Wizara nilitaka kuukataa uteuzi kwa sababu ningekuwa najulishwa usiku sana kuhusu ajali mbaya lakini tumejaribu na tunaendelea” amesema.
Ripoti imetaja vyanzo vya ajali kuwa ni pamoja na kutokuwepo kwa vituo vya ukaguzi, kuwepo baraza la usalama lisilofanya kazi, madereva wasio na mafunzo mwafaka, barabara kujengwa chini ya kiwango, na upungufu wa takwimu sahihi kuhusu ajali.
Waziri Bagiire ametaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa kumaliza tatizo hilo kuwa ni usajili na utoaji leseni kwa madereva wote wa mabasi, kuyaondoa mabasi kutoka katikati ya jiji, kuzuia malori yaliyobeba miwa kwenye barabara kuu ya Jinja- Kampala, na kodi kubwa kwa magari yaliyotumika.
“Tumemaliza jinamizi, madereva wa mabasi, na wanapofuata ni madereva wa teksi, tunataka wote wasajiliwe na wawe na leseni”amesema.
No comments:
Post a Comment