Friday, February 9, 2018

9 February 2018,Serikali yawahakikishia ulaji wakulima wa pamba

SERIKALI imeweka mkakati mahususi kuhakikisha pamba yote iliyozalishwa na wakulima wa zao hilo baada kuhamasishwa, itatununuliwa na wanunuzi wa ndani na nje ya nchi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema hayo wakati akijibu swali la papo kwa hapo la Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM) aliyetaka kujua serikali imejipanga vipi kununua pamba yote ya wakulima baada ya wakulima kuwahamasishwa na kuzalisha kwa wingi zao hilo.

Ndassa alisema, wakulima wa zao hilo katika mikoa inayolima pamba ya Mwanza, Simiyu na Mara, wamehamasishwa na kuzalisha kwa wingi zao hilo kutoka kilo 6,000 hadi kilo milioni 30, na serikali imejipanga vipi, endapo wanunuzi watashindwa kumaliza kununa pamba yote.

Mbunge huyo pia alimuuliza Waziri Mkuu, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha dawa za kuua wadudu wanaoshambulia mimea ya zao hilo, inapatikana kwa urahisi na kwa wakati katika mikoa hiyo.

Majaliwa alisema, kama wanunuzi wa ndani, watakuwa wamebakiza pamba iliyozalishwa kwa wingi katika mikoa hiyo, serikali inafanya mchakato wa kutafuta wanunuzi wa zao hilo nje ya nchi kupitia wizara ya kilimo inayoshughulikia jambo hilo.

“Ni kweli kwamba serikali imehamasisha wakulima wa mazao mbalimbali nchini kufufua mazao hayo kwa kuanzia na mazao ya pamba, korosho, chai, tumbaku na kahawa ambayo yalianza kufifia kutokana na wakulima kuyaacha kwenye mashamba,” alisema.

Waziri Mkuu aliwapongeza wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri, kwa kuitikia mwito wa serikali katika kusimamia uzalishaji wa mazao hayo kitalaamu. Alisema lengo la kufufua mazao hayo ni kutaka kuongeza pato la taifa.

Katika kuweka mikakati mahususi ya zao, hilo Waziri Mkuu alisema serikali itakutana na wadau wa zao hilo jijini Mwanza kuanzia Februari 15 hadi Februari 17 kwa ajili ya kuweka mipango mahususi na endelevu ya kukuza zao hilo kuanzia na uzalishaji hadi uuzaji wake.

Majaliwa alisema katika mkutano huo wa wadau mbalimbali wa zao hilo, serikali itazungumza na wadau wa pamba wakiwemo wazalishaji, wanaochambua nyuzi na wanaofanya shughuli nyingine ili kuweka mipango endelevu ya zao hilo.

No comments: