Sunday, February 11, 2018

11 February 2018,Waliotaifisha gari la sukari Namanga Mkoani Arusha kuchukuliwa hatua za kisheria

Serikali imetaifisha tani moja ya sukari iliyoingizwa nchini kwa njia ya magendo katika mpaka wa Namanga kutoka nchini Kenya.

Kwa mujibu wa Mwananchi leo Jumapili Februari 11,2018 Mkurugenzi wa Huduma ya Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo amesema sukari hiyo ilikamatwa jana Februari 10,2018 mpakani Namanga mkoani Arusha.

Kayombo amesema pia gari lililokuwa limebeba sukari hiyo limetaifishwa na watu wawili wanashikiliwa kwa hatua zaidi za kisheria.

Amesema sukari hiyo imefungashwa kwenye mifuko yenye nembo ya Azania na Azam.

“Sina hakika kama Azania au Azam ni wahusika, hilo litajulikana baadaye hatua za kisheria zitakapochukuliwa,” amesema.

Kayombo amesema licha ya kuwa sukari hiyo imeingizwa kimagendo, shehena hiyo haikuwa imelipiwa kodi na haikuwa na kibali cha aina yoyote kuruhusu kuingia nchini.

Ametoa rai kwa wananchi kujiepusha na biashara haramu akisema wamejizatiti vilivyo kukabiliana na magendo.

Kayombo amesema maofisa wa mamlaka hiyo pia walikamata mirungi iliyokuwa ikiingizwa nchini kutoka Kenya.

Amesema watu wawili wanashikiliwa na gari lililobeba mirungi hiyo aina ya Toyota Noah limetaifishwa.

Amesema wasafirishaji wa mirungi hiyo waliiweka sehemu ya mbele ya gari eneo la injini.

“Huwezi kufikiria kama kuna mzigo unaweza kuficha huko lakini maofisa wetu walibaini mbinu hiyo na kuwakamata,” amesema.

No comments: