Saturday, December 2, 2017

2 December 2017, Kanda ya ziwa kunufaika na mpango wa serikali wa uboreshaji upatikanaji wa maji safi na salama

Sh245 bilioni zinatarajiwa kutumika kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama katika mikoa na miji inayozunguka Ziwa Victoria.

Akizungumza wakati wa kukabidhi magari matatu na pikipiki sita zitazotumika kutekeleza miradi ya maji katika halmashauri tatu za mikoa ya Mwanza na Simiyu juzi, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe alisema huo ni utekelezaji wa sera ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji umbali usiozidi mita 100.

Alitaja baadhi ya miji itakayonufaika na mradi huo kuwa ni jiji la Mwanza, Magu na Misungwi, yote ya mkoani Mwanza, pamoja na Lamadi (Simiyu) na Musoma (Mara).

Waziri Kamwelwe alisema miradi hiyo inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji, ni sehemu ya utekelezaji wa miradi wa Maji na Usafi wa Mazingira katika Ukanda wa Ziwa Victoria (LVWATSAN).

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Mwauwasa), Anthony Sanga ambaye mamlaka yake ni moja ya wanufaika wa mradi huo aliishukuru Serikali kwa magari na pikipiki hizo alizosema zitasaidia shughuli za uendeshaji wa utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kuhusu huduma katika maeneo ya miinuko na milimani jijini Mwanza, Sanga alisema Mwauwasa imeanzisha mfumo maalumu wa kusambaza majisafi na salama na kuondoa majitaka maeneo ya milimani na miinuko.

“Licha ya changamoto ya kijiografia kutokana na Jiji la Mwanza kuwa na maeneo ya milima na miinuko, Mwauwasa tumejitahidi kuboresha huduma ya miundombinu ya maji machafu ambayo ni ya kwanza nchini,” alisema.

Alitaja maeneo ya milima na miinuko yanayonufaika na huduma hiyo kuwa ni Kilimahewa, Nyamanoro, Mbugani, Mabatini na Igogo wilayani Kwimba.

No comments: