Tuesday, October 3, 2017

3 October 2017, Waasi 91 katika jimbo la Bieh nchini Sudan wameuawa na Jeshi la Kusini mwa nchi hio

Jeshi la Sudan Kusini limetangaza kuwa kufuatia kuanza wimbi jipya la mapigano katika eneo la Waat katika jimbo la Bieh, jumla ya waasi 91 wameuawa na jeshi hilo huku wengine wakijeruhiwa.

Hayo yameelezwa na Lul Ruai Koang, Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini na kuongeza kuwa, mapigano yaliyoanza siku ya Jumapili iliyopita na kuendelea, yanaweza kusababisha uharibifu zaidi wa roho na mali.

Kwa mujibu wa Koang, katika shambulizi la kundi la waasi dhidi ya ngome za jeshi la serikali siku ya Jumapili, askari wanne waliuawa. Aidha ameashiria mwenendo wa mazungumzo ya amani ya viongozi wa eneo sambamba na kujiri mashambulizi ya waasi na kusema, waasi hao wanajaribu kuipotosha jamii ya kimataifa kwa ajili ya kupata nafasi zaidi.

Sudan Kusini ilitumbukia katika machafuko ya ndani tangu mwezi Disemba mwaka 2013, baada ya Rais Salva Kiir Mayardit kumtuhumu aliyekuwa makamu wake Riek Machar kwamba aliongoza njama za kutaka kumpindua madarakani.

Baada ya mapigano makali yaliyosababisha maelfu ya watu kuuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi, hatimaye mwezi Agoti mwaka 2015, vinara hao hasimu walikubaliana kusitisha vita baina yao ingawa hata hivyo pande hizo zimeshindwa kutekeleza makubaliano hayo.

No comments: