Sunday, October 15, 2017

15 October 2017 ,Umasikini waongezeka nchini Ufaransa

Takwimu zilizotangazwa na Asasi ya Kimataifa ya Kupambana na Umasikini nchini Ufaransa zinaonyesha kuwa, tatizo la kijamii la umasikini limeongezeka mjini katika nchi hiyo ya bara Ulaya katika kipindi cha miaka kumi ya hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Radio ya Kimataifa ya Ufaransa ya RFI takwimu zilizotolewa kuhusiana na hali ya umasikini nchini Ufaransa zinaonyesha kuwa, tatizo hili la kijamii limekuwa likiongezeka miongoni mwa wananchi wa nchi hiyo na kuwafanya wakabiliwe na matatizo tofauti.

Ripoti ya Asasi ya Kimataifa ya Kupambana na Umasikini nchini Ufaransa inaonyesha kuwa, idadi ya watu ambao hivi sasa wanaishi chini ya mstari wa umasikini nchini humo imefikia milioni nane na laki tisa.

Claire Hédon, Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Kupambana na Umasikini Ulimwenguni amesema kuwa, idadi ya watu walioongezeka katika orodha ya watu masikini nchini Ufaransa kuanzia 2005 hadi 2015 imefikia milioni moja.

Amesema kuwa, hivi sasa kuna watu milioni mbili na laki tatu nchini Ufaransa ambao wanaishi kwa kipato cha chini ya Euro 670 kwa mwezi ambapo waathirika wengi zaidi wa umasikini katika nchi hiyo ya barani Ulaya ni wanawake na watoto.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, mwezi uliopita, Shirika la Uchunguzi wa Maoni na Utafiti wa Masoko Duniani (IPSOS) lilieleza katika ripoti yake ya kila mwaka kuwa, zaidi ya asilimia 30 kati ya Wafaransa wote milioni 67 wanaishi kwenye umasikini na wengine asilimia 20 wanakaribia mstari wa umasikini.

No comments: