Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema kuwa, alihisi uchungu mwingi baada ya Mahkama ya Kilele nchini humo kufuta ushindi wake katika uchaguzi uliopita wa tarehe Nane Agosti mwaka huu.
Aidha Rais Kenyatta amesema kuwa, hana chuki na jamii ya Wakisii ambayo anatokea Jaji Mkuu David Maraga aliyefuta ushindi wake, ingawa amesisitiza kwamba, anapinga uamuzi wa jaji huyo.
"Hebu chukulia kama umenunua ng'ombe kisha akaibwa, hatimaye polisi wakampata na walipompeleka mahakamani jaji akasema kwa sababu fomu ya 'P3' haikujazwa hivyo ng'ombe huyo anatakiwa arejeshwe kwa mwizi."
Akisisitiza kuwa hana chuki na jamii ya Kisii Rais Uhuru Kenyatta amesema: "Sina shida kamwe na jamii ya Kisii lakini nina shida na mahakama na huyo mzee kwa uamuzi wake. Nikikosa kujitetea watu watadhani ni kweli niliiba.
Lazima nijitetee, hata wewe ukifanyiwa dhambi sharti ujitetee. Lakini pia hatutaki siasa za ukabila.
Hatutaki kurudi huko tena, tulipoteza uhai wa Wakenya na mali zetu.
Tukashifu siasa zinazoendeshwa kwa msingi wa ukabila," Alisema Rais Kenyatta .
Awali Muungano wa National Super Alliance (NASA) ulipinga ushindi wa Rais Kenyatta aliyepeperusha bendera ya chama cha Jubilee katika uchaguzi wa Agosti nane, ambapo hata hivyo Mahakama ya Kilele ya nchi hiyo ilikubali malalamiko ya muungano huo wa upinzani na kufuta ushindi wake.
Katika malalamiko yake mahakamani NASA ilihoji fomu 34A na 34B kwamba zilikuwa na dosari kwa kutotiwa sahihi na mawakala huku zingine zikikosa kujazwa matokeo kando na kutokuwa na alama za usalama.
No comments:
Post a Comment