Thursday, September 14, 2017

14 September 2017, "Iran ndio muungaji mkono wa kweli kwa Waislamu wa Myanmar",_Jumuiya ya Waislamu wa Suni Pakistan

Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu wa Suni nchini Pakistan amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni muungaji mkono wa kweli kwa Waislamu wa Rohingya wanaokandamizwa nchini Myanmar.

Pir Syed Riaz Hussain Shah, amesema kuwa hakuna nchi nyingine iliyochukuwa hatua ya maana kuwasaidia Waislamu wa Rohingya, ispokuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki.

Allamah Syed Riaz Hussain Shah ameongeza kuwa, hata Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) iliishia tu kutoa tamko la kulaani mauaji yanayofanywa na jeshi la Myanmar bila kuchukua hatua yoyote ya maana.

Msomi huyo mkubwa wa Kisuni nchini Pakistan amesema kuwa, ni lazima nchi za Kiislamu zichukue hatua ya maana kwa ajili ya kuwatete Waislamu wa Rohingya sambamba na kuiwekea vikwazo serikali ya Myanmar.

Hii ni katika hali ambayo raia wa Pakistan wamefanya maandamano katika miji 70 ya nchi hiyo kulaani jinai dhidi ya binaadamu zinazofanywa na jeshi la Myanmar kwa kushirikiana na Mabudha magaidi kuwalenga Waislamu wasio na ulinzi wa Myanmar.

Katika maandamano hayo mbali na kulaani mauaji ya umati dhidi ya Waislamu, waandamanaji wamezichoma moto bendera za Myanmar.

Kadhalika waandamanaji sambamba na kutanganza mshikamano wao na Waislamu madhlumu wa Myanmar, wamezitaka jumuiya za kimataifa kuwachukulia hatua kali viongozi wa Myanmar wanaotekeleza mauaji hayo ya halaiki dhidi ya Waislamu wasio na hatia yoyote.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbali na kutuma misaada ya kibinaadamu kwenda kwa Waislamu wa Rohingya walioko nchini Bangladesh, imezitaka nchi zote za Kiislamu kuiwajibisha serikali ya Myanmar haraka iwezekanavyo kutokana na hatua yake hiyo.

No comments: