Monday, September 11, 2017

11 September 2017, Rais Uhuru Kenyatta: Tutamsaili na kumuondoa madarakani Odinga kama atashinda

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema kuwa, hata kama mgombea wa upinzani wa Muungano wa NASA Raila Odinga ataibuka mshindi katika uchaguzi wa marudio wa tarehe 17 ya mwezi ujao wa Oktoba, chama chake cha Jubilee kina wingi mkubwa Bungeni wa kuweza kumsaili ndani ya muda wa chini ya miezi mitatu na kumuondoa madarakani.

Akizungumza leo katika ikulu ya Rais mjini Nairobi na viongozi wa kabila la Kamba, Rais Kenyatta amesisitiza kwamba, chama cha Jubilee kina wingi wa viti katika Bunge na Baraza la Seneti na kwamba, hata kama Raila Odinga atashinda kiti cha Urais anaweza kusailiwa na kuondolewa madarakani katika kipindi cha chini ya miezi mitatu.

Rais wa Kenya ambaye hata hivyo hakubainisha wala kufafanua sababu za zitakazopelekea kumsaili Bwana Odinga kama atashinda kiti cha Urais katika ujao wa marudio mwezi ujao amesisitiza kwamba, wingi wa viti vya Jubilee katika Bunge la Taifa na Baraza la Seneti unakipa uwezo chama chake hata wa kubadilisha katiba.

Rais Kenyatta ambaye amekuwa akiendelea na kampeni za uchaguzi amehoji  kama ninavyomnukuu: kama Raila Odinga akichaguliwa kuwa Rais katika uchaguzi ujao wa marudio ataongoza vipi nchi? Katika Baraza la Seneti lililopita hatukuweza kupitisha miswada... lakini hivi sasa tunaweza kufanya mambo bila kuhitaji hata mjumbe mmoja wa NASA.

Wakati huo huo, wajumbe wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC) wanakutana mjini Naivasha katika kikao cha faragha kujadili tofauti zinazoshuhudiwa miongoni mwao lakini pia kupanga mipango ya uchaguzi mpya utakaofanyika tarehe 17 mwezi ujao.

Kikao hicho kinafanyika wakati huu ambapo mashinikizo yameendelea kutolewa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo Ezra Chiloba kumtaka ajiuzulu.

No comments: