Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu imelaani vikali mauaji na jinai dhidi ya Waislamu Warohingya wa nchini Myanmar.
Ayatullah Mohsen Araki, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amesisitiza katika taarifa yake kwamba, jumuiya za kimataifa, asasi za haki za binadamu, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na warekebishaji wote ulimwenguni wana jukumu na masuuliya kwa Waislamu wanaokandamizwa wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar.
Sambamba na kulaani jinai hizo, Ayatulllah Araki amesema bayana kwamba, kiwango cha mauaji ya kikatili ya Waislamu wa Rohingya wa jimbo la Rakhine huko Myanmar yanayofanywa na mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada wakipata himaya na uungaji mkono wa serikali na jeshi la nchi hiyo mbele ya kimya cha kimataifa chenye kutia shaka ni jambo lisilotaswirika.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amesisitiza kuwa, jumuiya hiyo inazitaka nchi zote za Kiislamu zisimame na kuwatetea Waislamu madhulumu wa Myanmar.
Wimbi jipya la mauaji ya Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa Myanmar lilianza tarehe 25 Agosti mwaka huu.
Hadi hivi sasa maelfu ya Waislamu hao wameshauawa na kujeruhiwa na karibu laki tatu wengine wamekimbia makazi yao.
Serikali ya kibudha ya Myanmar inawanyima Waislamu hao hata haki zao za kimsingi kabisa kama vile uraia.
No comments:
Post a Comment