Sunday, September 10, 2017

10 September 2017, Waziri Zarif:Viongozi wa nchi za Kiislamu kuzungumzia jinai dhidi ya Waislamu wa Myanamr

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema viongozi wa nchi za Kiislamu wanaokutana katika kikao cha Sayansi na Teknolojia nchini Kazakhstan watazungumzia pia jinai zinazoendelea kufanywa dhidi ya Waislamu wa Myanmar.

Mohammad Javad Zarif ambaye amefuatana na Rais Hassan Rouhani katika safari yake nchini Kazkhstan kushiriki kikao cha viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) amewaeleza waandishi wa habari kuwa katika kipindi cha siku chache zilizopita amewasiliana na kufanya mashauriano ya kina na mawaziri wenzake wa mambo ya nje wa nchi nyengine za Kiislamu na imepangwa kuwa katika kikao cha Sayansi na Teknolojia cha viongozi wa nchi wanachama wa OIC kitakachofanyika nchini Kazakhstan jinai wanazofanyiwa Waislamu wa Myanmar zitajadiliwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa tokea awali Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikifuatilia suala la kuitishwa kikao cha kujadili jinai wanazotendewa Waislamu wa Myanmar katika kikao cha Astana nchini Kazakhstan na kufafanua kwamba kwa pendekezo lililotolewa na baadhi ya nchi washiriki, Kazakhstan ambayo ni nchi mwenyeji wa kikao na Uturuki ambayo ni mwenyekiti wa sasa wa OIC zitafuatilia uitishaji wa kikao hicho.

Aidha amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itajitahidi kuhakikisha kwamba nchi za Kiislamu zinachukua msimamo mmoja kukabiliana na jinai dhidi ya binadamu wanazofanyiwa Waislamu wa Myanmar.

Tangu Ijumaa ya tarehe 25 Agosti Waislamu wasiopungua 6,334 wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar wameuawa na wengine 349 wamejeruhiwa katika wimbi jipya la mashambulizi na ukandamizaji unaofanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu katika mkoa wa Rakhine.

Waislamu wa eneo hilo la Rakhine wamekuwa wakishambuliwa na kuuawa na Mabudha wenye misimamo mikali wakisaidiwa na jeshi la Myanmar tangu mwaka 2010.../

No comments: