Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika kanda ya Afrika Magharibi amesema lazima Togo ifuate njia yaliyopita mataifa mengine ya Afrika Magharibi na kuweka haraka kikomo cha vipindi viwili vya urais ikiwa inataka kuepusha malalamiko yanayopamba moto yasigeuke kuwa mgogoro wa kisiasa.
Mohamed Ibn Chambas amesema inavyoonekana ni jambo lisiloweza kuepukika kwa Togo kujiunga na nchi zilizosalia za Afrika Magharibi katika kuwa na vikomo vya urais.
Mjumbe huyo wa UN katika eneo la Maghairbi mwa Afrika na Sahel amesema mtazamo wao mkuu ni kuwashauri Watogo wachukue hatua hiyo ili kuepusha malalamiko kupamba moto zaidi.
Amesema hatua iliyochukuliwa wiki hii na serikali ya Rais Faure Gnassingbe ya kupendekeza mswada wa kuifanyia marekebisho katiba na kurejesha tena sheria ya kikomo cha vipindi vya urais inakaribishwa. Hata hivyo upinzani umeukataa mswada huo ukisema utamwezesha kiongozi huyo kubakia madarakani hadi mwaka 2030.
Chambas amesema wanasubiri kuona kile hasa kilichomo ndani ya mswada huo ingawa amesisitiza kuwa katika mazungumzo aliyofanya siku ya Ijumaa na Gnassingbe, kiongozi huyo alimhakikishia kuwa "ameisikia sauti ya wananchi".
Maelfu ya watu wamemiminika mabarabarani katika kipindi cha siku tatu zilizopita nchini Togo kutaka Rais Faure Gnassingbe ang'atuke madarakani katika kile kinachoonekana kama changamoto kubwa zaidi kuukabili utawala wa miaka 50 wa ukoo wake tangu kifo cha baba yake kilichotokea mwaka 2005.
Katika maandamano hayo, polisi wameripotiwa kutumia gesi ya kutoa machozi tu ili kuepusha umwagaji damu uliotia doa maandamano yaliyopita. Aidha kumekuwepo na udhibiti wa matumizi ya intaneti na simu za mkononi.
Japokuwa jana Jumamosi hakukuripotiwa maandamano yoyote ya upinzani na moto wa malalamiko umeonekana kupoa, lakini mrengo wa upinzani umesema utaendeleza maandamano mpaka Gnassingbe aondoke madarakani.
Tangu aliyekuwa Rais wa Gambia Yahya Jammeh alipolazimishwa kuachia hatamu za uongozi wa nchi baada ya kushindwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Desemba mwaka jana, nchi zote za Magharibi mwa Afrika ukiondoa Togo zimekubali kuweka sheria ya kikomo cha vipindi viwili vya urais.../
No comments:
Post a Comment