Wednesday, March 21, 2018

21 March 2018,Madereva wa daladala wagoma kutoa huduma ya usafiri mjini Musoma

Madereva wa magari yanayotoa huduma ya usafiri kati ya Musoma na wilaya za Mkoa wa Mara wamegoma leo Machi 21, wakishinikiza mamlaka husika kubadilisha bei elekezi ili kuendana gharama za uendeshaji.

Pia, daladala zinazofanya safari zake katikati ya mji wa Musoma zimegoma kutoa huduma hiyo kwa madai kuwa zinaingiliwa katika njia zao za usafiri na pikipiki zenye miguu mitatu maarufu bajaji.

Wakizungumza na gazeti hili katika maeneo tofauti mjini hapa, baadhi ya wamiliki wa magari hayo wamesema wamgoma hadi malalamiko yao yatakapopata ufumbuzi wa kudumu.

Mmoja wa wamiliki hao, Marejesho Elia amesema wameamua kugoma baada ya Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi kavu (Sumatra) mkoani Mara kuwaamuru wamiliki wa magari hayo kutumia nauli elekezi iliyotolewa na mamlaka hiyo miaka minne iliyopita.

“Kwa kipindi hicho mamlaka hiyo ilitoa nauli elekezi ambayo haiendani na gharama za uendeshaji,” amsema.
Elia amesema baada ya kukutana walikubalina na  Sumatra kutoa nauli elekezi mpya, lakini mamlaka hiyo haikufanya hivyo ingawa wamiliki hao waliendelea kutumia nauli walizokubalina kwenye kikao hicho.

“Kutokana na nauli hizo kutokuwa kwenye maandishi wamiliki wamekuwa wakiomba mamlaka hiyo kuweka nauli hizo katika maandishi ili kutumika kihalali, lakini Sumatra imeshindwa kutekeleza huku tukitakiwa kutumia nauli ya miaka minne iliyopita” amesema.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wasafirishaji wilayani Musoma, Gabriel Adam amesema wanachama wake hawapo tayari kuendelea kutoa huduma kwa nauli hizo elekezi, badala yake waruhusiwe kutumia walizokubaliana kwenye kikao.

Kwa mujibu wa Sumatra, nauli kutoka Musoma kwenda Tarime ni Sh2,800 badala ya Sh4,000 inayotozwa kwa sasa, Musoma- Serengeti Sh4,000 badala ya Sh6,000 na Musoma-Majita Sh4,000 badala ya Sh6,000.

Akizungumza na wamiliki hao, mkuu wa polisi wilayani Musoma, Sylvester Njau amewataka wamiliki hao kuendelea kutoa huduma kwa bei ya awali, huku akiahidi kufanyika kwa kikao kati ya wamiliki, polisi na Sumatra.

Ofisa Sumatra mkoani Mara, Halima Lutavi amesema nauli elekezi hutolewa kwa mujibu wa sheria na kanuni na kwamba, wafanyabiashara hao wanapaswa kutii sheria.

No comments: