Upande wa mashtaka umewasilisha maombi ya kukata rufaa dhidi ya dhamana ya mshtakiwa Boniface Mbilinyi (32), anayekabiliwa na kosa la kutamka uongo wa kiasi cha fedha alichokuwa nacho akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), akijiandaa kwenda Dubai.
Mbilinyi ambaye ni mfanyabiashara wa vifaa vya magari anadaiwa kutamka uongo kuwa alikuwa na dola 40,000 za Marekani lakini ilibainika alikuwa na dola 123,000.
Maombi hayo yamewasilishwa leo Februari 7, 2018 na Wakili wa Serikali, Awamu Mbagwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Huruma Shaidi shauri hilo lilipofikishwa mahakamani kwa ajili ya kutajwa.
"Kwa sasa tunasubiri kupewa nakala ya uamuzi kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, lakini kesi ya msingi itaendelea kama kawaida na leo ilikuja kwa ajili ya kutajwa," alidai Mbagwa.
Alidai waliwasilisha maombi kupinga dhamana dhidi ya mshtakiwa Januari 26, 2018 katika Mahakama hiyo na baada ya kuzipata nyaraka wataziwasilisha Mahakama Kuu.
Hata hivyo, wakili Mbagwa alidai upelelezi wa shauri hilo umekamilika na wako tayari kumsomea mshtakiwa hoja za awali.
Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hadi Februari 21,2018 itakapotajwa kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa hoja za awali.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Januari 13,2018 alipokuwa akisafiri kutoka Tanzania kwenda Dubai.
Mbilinyi anayetetewa na wakili Ndigwaho Joel alikana shtaka linalomkabili baada ya kusomewa na yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua ya utambulisho kutoka taasisi inayotambulika kisheria.
Hakimu Shaidi aliruhusu kiasi cha fedha alizokamatwa nazo ambazo zipo katika akaunti maalumu zitumike kama dhamana.
Admit Mwananchi
No comments:
Post a Comment