Friday, February 16, 2018

16 February 2018,Moto wasambaratisha vifaa vya kusomea vya wanafunzi wa Shule ya Sekondari KIPOKE mkoni Mbeya

Bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Kipoke wilayani Rungwe mkoani Mbeya limeteketea kwa moto uliounguza magodoro, nguo, vitabu na madaftari ya wanafunzi hao.

Tukio hilo limetokea leo Februari 16, 2018 wakati wanafunzi wakiwa darasani wakiendelea na masomo yao.

Meneja wa shule hiyo, Gervas Mwanyila amesema bado hawajajua chanzo cha moto huo licha ya kufanikiwa kuuzima na kwamba hakuna mwanafunzi aliyepoteza maisha.

“Asubuhi tu mwanafunzi mmoja alitoka darasani kwenda bwenini ghafla akarudi huku akipiga kelele kwamba bweni linaungua na hakukua na mtu yeyote ndani ya bweni hilo,” amesema.

Amesema baadhi ya magodoro, na vitu vingine vichache vya wanafunzi walifanikiwa kuviokoa lakini vitu vingi viliteketea kwa moto na wanafunzi waliokuwa wakitumia bweni hilo walikosa sehemu ya kujihifadhi.

Mwanyila amesema bweni hilo lilikuwa likitumiwa na wanafunzi 64 na kwamba wanafunzi hao hawana mtindo wa kutumia pasi au simu kwenye mabweni yao hivyo wanaendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama wilaya humo kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Julius Chalya alipopigiwa simu yake ya mkononi haikupokelewa, lakini Mwanyila amesema mkuu huyo wa wilaya alikuwepo eneo la tukio.

No comments: