Waasi wa Sudan Kusini wanawashikilia mateka marubani wawili wa ndege kutoka Kenya na wanasema hawatawaachilia huru hadi pale watakapotoa fidia kwa familia ya raia aliyeuawa wakati ndege yao ilipoanguka wakati wa kutua.
Ndege hiyo ilianguka katika mji wa Akobo, katika eneo la Greater Upper Nile, zaidi ya wiki mbili zilizopita, amesema Lam Paul Gabriel naibu msemaji wa waasi.
Ameongeza kuwa, wakati ndege hiyo ilipoanguka ikikaribia kutua, ilimuaa mwanamke na mifugo kadhaa. Amesema jamaa wa mwanamke huyo na wenye mifugo wanataka walipwe fidia.
Msemaji wa waasi hao amesema, viongozi wa Kenya wanapaswa kumwandikia barua Riek Machar, kiongozi wa waasi ili atoe amri ya kuwaachili huru marubani hao.
Machar, makamu wa zamani wa Rais wa Sudan Kusini, ni kiongozi wa mrengo mkubwa zaidi wa waasi Sudan Kusini na amekuwa akiishi uhamishoni Afrika Kusini tokea mwaka 2016.
Msemaji wa Jeshi la Sudan Kusini, Brigedia Jenerali Lul Ruai Koang amethibitisha kushikiliwa mateka marubaini hao wawili Wakenya.
Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kuipindua serikali yake.
No comments:
Post a Comment