Saturday, December 16, 2017

16 December 2017,Rais wa Zimbabwe:Kuinua uchumi wa nchi hio

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amewaeleza wanachama wa chama chake tawala cha ZANU-PF kuwa wanapaswa kuurekebisha uchumi ikiwa wanataka wawe na nafasi ya kushinda uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.

Mnangagwa ameyasema hayo katika mkutano wa chama hicho uliomvua uongozi aliyekuwa kiongozi mkongwe wa chama na Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe pamoja na kumtimua mkewe Grace pamoja na waungaji mkono wake sambamba na kumuidhinisha yeye Mnangagwa kuwa mkuu mpya wa chama na mgombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2018.

"Tutashinda uchaguzi ikiwa tu tutaweza kuonyesha ishara kwamba tunafufua uchumi na wakati huohuo tutaweza kupata mafanikio ya kiuchumi ikiwa tutaweza kuhakikisha tunashinda tena uchaguzi",

amesema Mnangagwa.
Uchumi wa Zimbabwe uliporomoka katika nusu ya pili ya kipindi cha utawala wa Mugabe hasa baada ya unyang'anyi uliofanywa kwa maelfu ya mashamba ya kibiashara yaliyokuwa yakimilikiwa na raia wazungu ulioandamana na fujo na utumiaji nguvu.

Mnangagwa alitangaza wiki hii kwamba taifa hilo la kusini mwa Afrika linaweza kuitisha uchaguzi mwezi Machi mwakani, miezi mitano tu tangu yalipofanyika mapinduzi baridi ya kijeshi yaliyohitimisha utawala wa miaka 37 wa Robert Mugabe.

Katika hotuba yake mbele ya hadhara ya wanachama wa chama chake tawala hapo jana, Rais Emmerson Mnangagwa alisisitiza kuwa demokrasia inaitaka Zanu-pf kama chama cha siasa kichuane na vyama vya upinzani katika uchaguzi ambao inapasa uwe huru, wa haki, wa wazi na wenye itibari.

Katika kile kinachoonekana kama ishara ya kutumia jeshi ili kuimarisha nguvu zake za kisiasa, Mnangagwa amewateua majenerali watatu wa jeshi kuwa wajumbe wa ofisi ya utendaji ya kisiasa, ambayo ni chombo cha juu kabisa cha upitishaji maamuzi ndani ya ZANU-PF.

Rais mpya wa Zimbabwe aidha amesema atatangaza manaibu wake wawili hivi karibuni.

Kamanda wa Vikosi vya Ulinzi Jenerali Constantino Chiwenga anapewa nafasi kubwa ya kushika moja kati ya nyadhifa hizo ikielezwa kuwa ni bakhshishi atayopewa kwa kuongoza mapinduzi baridi ya kijeshi yaliyomlazimisha Mugabe kutangaza kujiuzulu na kung'atuka madarakani..

No comments: