Friday, December 15, 2017

15 December 2017,Watoto waliotumiwa vitani Nchini Kongo wazawadiwa fidia ya dola milioni kumi

Watoto waliotumiwa vitani Kongo wazawadiwa fidia ya dola milioni 10
Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi leo wamewapatia fidia ya dola milioni kumi watoto waliosajiliwa kama askari nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ya mbabe wa kivita Thomas Lubanga.

Mahakama ya ICC imesema kuwa Lubanga alipasa kisheria kulipa kiasi hicho chote cha fedha kwa watoto aliowasajili kama askari vitani na familia zao. Hata hivyo imesema ilitambua kuwa mbabe huyo wa kivita asingeweza kulipa fidia hiyo

Imeongeza kuwa, sehemu ya fidia hiyo itatolewa na Mfuko wa Fedha wa Kuwahudumia Wahanga wa mahakama hiyo na kwamba mfuko huo pia utaomba mchango kutoka serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mwaka 2012 Thomas Lubanga alipatikana na hatia ya kutenda jinai za kivita wakati kulipojiri mapigano katika mkoa tajiri kwa madini wa Ituri kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuanzia mwaka 2002 hadi 2003.

Mashirika ya misaada yanakadiria kuwa watu milioni 5.4 waliaga dunia kutokana na vita na athari zake huko Kongo DR kati ya mwaka 1998 na 2007, kiwango ambacho ni cha juu zaidi kuwahi kushuhudia tangu Vita vya Pili vya Dunia.

Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai imesema kuwa, malipo hayo ya fidia yatatumika katika kutoa huduma za kisaokolojia na miradi ya mafunzo ya ajira kwa wahanga 427 waliotambuliwa katika mchakato uliofanyika.

No comments: