Tuesday, November 7, 2017

7 November 2017,Rais Magufuli kutengua uteuzi wa Wakurugenzi Bukoba

RAIS John Magufuli ametangaza kutengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Erasto Mfugale na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini, Mwantumu Dau.

Alitangaza kufanya hivyo jana jioni mara baada ya mkutano wa hadhara alioufanya mjini Bukoba wakati wa uzinduzi wa mradi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Bukoba.

Rais Magufuli jana alikuwa katika siku yake ya kwanza ya ziara ya siku nne mkoani Kagera. Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Gerson Msigwa, Mfugale na Mwantumu sasa watapangiwa kazi nyingine.

Aidha, kufuatia hatua hiyo uteuzi wa Wakurugenzi wa Halmashauri hizo utafanywa baadaye.

Ilivyokuwa Wakati akihutubia mkutano huo, Rais Magufuli aliwabana wakurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya na Manispaa ya Bukoba akitaka kujua matumizi ya fedha za mfuko wa barabara zilizopelekwa huku baadhi ya viongozi wakishindwa kutoa majibu.

Kutokana na kukosa majibu ya uhakika, alisema anashangazwa kuona viongozi aliowateua wanakosa majibu juu ya fedha za Serikali.

Kama ilivyo kawaida yake, Rais Magufuli alianza kwa kuwaeleza wananchi juu ya mabadiliko aliyoyafanya tangu aingie madarakani ikiwamo udhibiti wa watumishi hewa na vyeti feki akisema mambo hayo yameigharimu nchi.

Baada ya kuzungumza masuala hayo aliwaita viongozi wa halmashauri ya Bukoba kwenye mkoa huo akitaka kueleza ni kiasi gani cha fedha za mfuko wa barabara walizopokea pamoja na matumizi yake.

“Serikali huwa inaleta fedha kwa ajili ya maendeleo ya kila manispaa na hata hapa tumeshaleta.

Mkurugenzi wa Manispaa, tumeleta kiasi gani hapa? bajeti ya manispaa ya Bukoba ni kiasi gani?” alihoji na kwamba anataka watu wajue matumizi yake.

Akijibu, Mfugale alisema hadi sasa alikuwa amepokea Sh bilioni 33 ikiwa ni bajeti ya jumla huku akishindwa kutolea majibu fedha za mfuko wa barabara.

“Katika fedha hizo kuna fedha ambazo ni mishahara Sh bilioni 19 kwa mwaka,” alisema.

Kabla hajamaliza, Rais alimuuliza “fedha za road fund (mfuko wa barabara) ni kiasi gani, nasema hivi kwa sababu zinapoteaga poteaga tu nataka uziseme hapahapa,” alisisitiza.

Mkurugenzi huyo Alishindwa kutoa majibu juu ya suala hilo ambalo rais ameliita ni kucheza na fedha za Serikali.

Naye Mwantumu alivyosimama kutoa majibu alisema hakumbuki ni kiasi gani suala ambalo limeonekana kumkasirisha Rais.

“Hapana mheshimiwa Rais labda aje mtunza hazina, mimi nina idara nyingi siwezi kukumbuka,” alisema.

Rais alisema anashangaa kuona viongozi aliowateua hawajui kuhusu fedha za Serikali.

“Nani anafahamu hela za mfuko wa barabara manispaa ya Bukoba kwa sababu viongozi niliowateua hawajui, pengine naweza nikateua Mkurugenzi sasa hivi,” alisema.

No comments: