Tuesday, November 7, 2017

7 November 2017,Jeshi la polisi lafanya upekuzi makao makuu ya Chama cha ACT

Jeshi la Polisi Jijini Dar es salaam limefanya upekuzi Makao Makuu ya Chama cha ACT- Wazalendo na kuchukua nyaraka, vifaa vya kiilektonikia vilivyotumika kuandaa taarifa ya kusinyaa kwa uchumi wa nchi.

Mbali na kufanya upekuzi, Jeshi hilo linaishikilia simu ya mkononi ya Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe kwa upelelezi huku yeye akisema mawasiliano aliyokuwa akiyafanya yamezingatia uhuru ulipo katika Katiba.

Upekuzi huo ulifanyika leo mchana muda mfupi baada ya Zitto kwenda kuripoti Kitengo cha Uhalifu wa Makosa ya Kifedha-Kamata jijini humo na kutakiwa kurejea tena Novemba 21.

Akizungumza na Mwananchi, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Ado Shaibu amesema ‘’polisi wamefika hapa saa 6 na wameondoka sasa (ilikuwa saa 10), wamefanya upekuzi na wamechukua flash, laptop (kompyuta mpakato) na nyaraka ambazo ni taarifa kwa umma iliyotolewa kuwa tutakutana kujadili hali ya uchumi.”

Ado amesema upekuzi huo umetumia muda mrefu baada ya polisi hao aliodai walikuwa wanne kufika na Katibu Mkuu wa chama hicho, Doroth Semu kutomkuta hivyo wakaamua kumfuata nyumbani kwake Tabata.

“Wamesema watakwenda kufanyia kazi vifaa hivyo na watavirejesha haraka ila hawajasema hasa ni lini...wale polisi mmoja alivaa sare na watatu walivaa kiraia ,”

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz kwa njia ya simu lakini hakupatikana na alipotafutwa Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa alisema, ‘’uchungizi utakuwa unaendelea lakini hilo atafutwe DCI na si Kamanda wa kanda Maalum wa Dar es Salaam.’’

Awali leo asubuhi, Zitto ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini mara baada ya kutoka kuripo Kitengo cha Uhalifu wa Makosa ya Kifedha alisema ‘’nimetakiwa kurudi tena Novemba 21 lakini wamechukua simu yangu na watakwenda kufanya upekuzi katoka ofisi yetu.”

"Kwa sasa sitapatikana, watu waliokuwa wananitafuta hawatanipata, kwa hiyo ndio hivyo wameamua wao lakini niwahakikishie tu kuwa mawasiliano niliyokuwa nayafanya yanalinda uhuru wangu wa Kikatiba," ameongeza
Amesema wanachokifikiria ni kwamba simu yake ilitumika kusambaza taarifa za uongo huhusu hali ya uchumi jambo ambalo alilipinga na kudai, suala lake linapaswa kufikishwa mahakamani.

“Nitafurahi suala hili likifikishwa mahakamani, kule tutaeleza kwa kina hata yale ambayo hatukuyasema kule tutayasema kwani uhuru utakuwa mkubwa,” alisema Zitto

Zitto anakabiliwa na tuhuma za kutumia kufanya makosa kinyume cha Sheria ya Makosa ya Mitandao na Takwimu ambapo Mwenyekiti wa chama hicho, Yeremia Mganja na Katibu Mkuu Doroth Semu wameunganishwa na juzi walifika kuhojiwa na kutakiwa kurejea tena Novemba 26.

No comments: