Zaidi ya ng’ombe 4,000 kutoka Tanzania zinashikiliwa na jamii ya Maasai ya Kenya katika Kaunti ya Kajiado baada ya kuingizwa na wafugaji nchini humo.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni wiki mbili zimepita tangu Serikali ya nchini hapa kukamata ng’ombe zaidi ya 1,305 katika Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro kwa madai ziliingizwa kinyume na utaratibu.
Kwa mujibu wa BBC Dira ya Dunia imeeleza pamoja na kuwa wafugaji wa eneo hilo lililopo Kusini mwa Kenya kuonekana kuendeleza kisasi, viongozi wameendelea na juhudi za kuzuia ukamataji wa mifugo.
Kamishna wa eneo hilo, Harsama Kello aliiambia BBC kuwa anaendelea na jitihada za kuzuia ukamataji wa mifugo ya kitanzania kwa kuwa hali hiyo inaharibu taswira ya nchi hizo majirani.
“Wafugaji wamepanga kunyang’anya mifugo yote itakayoingia kutoka Tanzania kwenda Kenya, lakini najaribu kwa nguvu zangu zote kulizuia jambo hili,” alisema Kello
“Hakuna namna tunaweza kuruhusu suala hili kuendelea. Ni hatua mbaya kwa diplomasia na mahusiano ya nchi ambazo ni majirani na tunashirikiana kwa mambo mengi,” alisema
Jamii ya Masai wa eneo hilo wamekuwa wakivuka mipaka kwa ajili ya kutafuta malisho kutokana na upungufu wa malisho.
Hatahivyo serikali nchini humo imeeleza kuwa uhaba huo unatokana na athari za shughuli za kibinadamu ikiwamo kumiliki mifugo mingi, mmomonyoko wa udongo na pia migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akizungumzia suala hilo alisema Serikali haina taarifa ya kuchukuliwa kwa ng’ombe hao akisisitiza sheria zifuatwe.
No comments:
Post a Comment